Saturday, March 15, 2014

WATANZANIA WATANO WAULA SHIRIKISHO LA SOKA AFRIKA.




Watanzania watano wameteuliwa kuingia kwenye jopo la makamishna watakaosimamia mechi mbalimbali za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa mwaka 2014 hadi 2016.

Kwa mujibu wa orodha iliyotumwa na CAF kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Watanzania hao ni Alfred Kishongole Rwiza wa Mwanza na Hafidh Ali Tahir wa Zanzibar ambao wamerejeshwa tena kwenye jopo hilo.

Rwiza na Tahir ambao ni waamuzi wastaafu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na wakufunzi wa uamuzi walikuwepo kwenye jopo lililopita la 2012 hadi 2014.

Makamishna wapya kwa upande wa wanawake ni Elizabeth Mwanguku Kalinga wa Mbeya na Isabellah Hussein Kapera wa Dar es Salaam.

 Kamishna mwingine mpya kwa upande wa wanaume ni Muhsin Ali Rajab kutoka Zanzibar.
Wakati huo huo, CAF imeandaa semina kwa makamishna wanaume itakayofanyika jijini Cairo, Misri kuanzia Aprili 3 hadi 4 mwaka huu.

Watoa mada kwenye semina hiyo ya siku mbili ni Katibu Mkuu wa CAF, Hicham El Amrani, Mkurugenzi wa Mashindano wa CAF, Shereen Arafa na Naibu Mkurugenzi wa Mashindano wa CAF, Khaled Nassar.

0 Responses to “ WATANZANIA WATANO WAULA SHIRIKISHO LA SOKA AFRIKA.”

Post a Comment

More to Read