Wednesday, April 2, 2014

MJUMBE: TUNAJIPANGA KUKWAMOISHA RASIMU.




Vyama vya upinzani vimeanza kutafuta utaratibu wa kuhakikisha theluthi mbili kwa Zanzibar haipatikani katika kupitisha vifungu vya Rasimu ya Katiba vinavyokwenda kinyume na  matakwa ya wananchi.

Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Bunge la Katiba, Hija Hassan Hija alipokuwa akizungumza na gazeti hili bungeni mjini Dodoma.
“Hawawezi kupata theluthi mbili, sisi Wawakilishi na Wabunge kutoka vyama vya CUF na Chadema kutoka Zanzibar  tunafikiria kupiga kura za wazi ili tuweze kudhibiti kura zetu,” alisema Haji, ambaye ni Mwakilishi kutoka Jimbo la Kiwani.

Alisema kama wajumbe wote 67 wanaotoka Zanzibar katika kundi la wajumbe 201 hawatakubali kuburuzwa, CCM bado hawawezi kupata theluthi mbili katika kupitisha uamuzi wa vifungu ambavyo wananchi hawavitaki.

Haji alisema hata kama Rais Jakaya Kikwete atasema kuwa wawape mambo wanayodai kupewa ikiwamo mapato yanayotokana na gesi na haki ya Zanzibar kujiunga na nchi wanazozitaka, hawatakubali kwa sababu wamekuwa wakiahidiwa kwa miaka 50 bila utekelezaji.

“Miaka 50 yote tumekuwa tukitaka kupewa haki zetu za kujiunga na nchi mbalimbali, lakini hatukupewa iwe leo watupe sisi? Hatutakubali Muungano huu, labda waseme wanatupatia muundo wote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

0 Responses to “MJUMBE: TUNAJIPANGA KUKWAMOISHA RASIMU.”

Post a Comment

More to Read