Tuesday, April 8, 2014
POLISI WA UGANDA WAVAMIA TANZANIA NA KUANZA KUPIGA RISASI OVYO, WATANZANIA WAWILI WAJERUHIWA
Do you like this story?
Askari saba kutoka nchini Uganda
wakiwa na bunduki ambazo idadi yake haijafahamika, wamevamia eneo la Mutukula,
mkoani Kagera, na kuanza kufyatua risasi ovyo.Hali hiyo ilizua hofu na
kusababisha tafrani kubwa miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.
Habari kutoka eneo hilo zinaeleza kuwa
askari hao waliokuwa wamevalia kiraia, walifanya uvamizi huo majira ya saa
11:00 jioni, kwa kile kilichodaiwa kuwa walikuwa wakiwatafuta watuhumiwa wa
wizi wa pikipiki.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo
waliozungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti, walisema katika tafrani hiyo,
wananchi wawili raia wa Tanzania, ambao majina yao hayajapatikana, walijeruhiwa
kwa risasi.
Kwa mujibu wa habari hizo, kati ya
majeruhi hao, mmoja anadaiwa kujeruhiwa kwenye kiganja na mwingine mguuni.
Habari hizo zinaeleza kuwa baada ya
wananchi kuona wenzao wamejeruhiwa, walianza kupambana na askari hao.
Hali hiyo inadaiwa kusababisha baadhi
ya askari hao kukimbia na kuvuka mpaka kuingia nchini kwao.
Hata hivyo, imeelezwa kwamba mmoja kati
ya askari hao w aUganda, alizingirwa na wananchi ambao walikuwa tayari
kujichukulia sheria mkononi.
Walisema baada ya askari huyo kuhofia
kuuawa na wananchi, alikimbia na kujisalimisha katika Kituo cha Polisi
kilichoko Mutukula upande wa Tanzania ambapo alikamatwa na kuwekwa rumande.
Askari huyo ambaye jina lake
halijafahamika hadi sasa, bado anashikiliwa na Polisi Mkoa wa Kagera kwa
mahojiano zaidi.
Aidha, habari zaidi zilidai kuwa askari
waliokimbia na kuingia Uganda waliwakamata raia wawili wa Tanzania na kuondoka
nao.
Kwa mujibu wa habari hizo, ufuatiliaji
wa kujua waliokamatwa na kuchukuliwa na askari hao ni akina nani unaendelea.
Hata hivyo, wananchi wanaoishi Mutukula
walidai kuwa siyo mara ya kwanza askari kutoka Uganda kuvamia eneo hilo na
kukamata Watanzania wanaoishi mpakani na kuondoka nao bila kushirikisha polisi
wa Tanzania.
“Huu siyo utaratibu. Ni ubabe. Hata
kama kuna Watanzania wanawahisi kuhusika na uhalifu katika nchi yao, inabidi
wafuate utaratibu kwa kutoa taarifa ili askari wa Tanzania washiriki kuwatafuta
wahalifu husika,” alisema mwananchi mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa.
Kwa mujibu wa wananchi hao, askari
walioingia nchini na kufanya tukio hilo ni askari polisi kutoka eneo la Mbarari
nchini Uganda.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera,
George Mayunga, alipoulizwa na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na
tukio hilo, alithibitisha, lakini akasema yeye hana mamlaka ya kulizungumzia
zaidi mpaka apate ruhusa kutoka Makao Makuu ya Polisi.
“Hili ni suala la kiusalama
linalohusisha nchi na nchi, siwezi kulizungumzia zaidi, tunachokifanya kama
kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa tunaandaa taarifa tuitume polisi makao
makuu, wenyewe ndiyo wataamua kama ni kuniruhusu mimi nizungumze au wazungumze
wao makao makuu,” alisema Kamanda Mayunga.
Kamanda huyo alisema kuwa kwa kawaida
masuala yanayohusu nchi na nchi serikali huwa inakuwa makini sana
kuyazungumzia, hivyo subira inahitajika ili watoe taarifa iliyo sahihi.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu
jijini Dar es Salaam, Advera Senso, alipoulizwa na NIPASHE jana, alisema
kinachopfanywa na jeshi hilo kwa sasa ni kuchunguza kujua ilikuwaje askari hao
watoke Uganda na kuingia Tanzania bila kuwaarifu polisi wenzao wa Tanzania.
“Tunahitaji kufanya hivyo ili kila nchi
ijiridhishe. Hilo ndilo suala la msingi ki-nchi na kisera. Na hiyo ndiyo maana
ya kuwapo Interpol (Polisi wa Kimataifa). Tuna ushirikiano,” alisema Senso.
Hata hivyo, alisema baada ya undani wa
suala hilo kujulikana, taarifa zitatolewa na jeshi hilo ngazi ya mkoa (Kagera).
CHANZO:
NIPASHE
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “POLISI WA UGANDA WAVAMIA TANZANIA NA KUANZA KUPIGA RISASI OVYO, WATANZANIA WAWILI WAJERUHIWA”
Post a Comment