Monday, April 28, 2014
WANAFUNZI WAPATIWA MAFUNZO YA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI NA BARABARANI.
Do you like this story?
Kampuni ya
mawasiliano ya simu ya Vodacom Tanzania kwa kushirikiana na jeshi la Polisi
Kanda ya mkoa wa Kinondoni wamewapatia mafunzo ya usalama sehemu za kazi kwa
wanafunzi wa shule za msingi Msasani, Mbuyuni na Oysterbay zote za wilaya ya
Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wa
Vodacom wao wametoa mafunzo ya usalama sehemu za kazi kwa wanafunzi hao
wakiamini kuwa wao ndio wafanyakazi wa baadae ambao ndio tegemeo la kukua kwa
uchumi wetu.
Akizungumzia juu ya mafunzo hayo Mkuu wa Idara ya Afya na Usalama,Karen Lwakatare amebainisha kuwa wao watatoa elimu na mafunzo juu ya usalama mahala pa kazi lengo ikiwa ni kufafanua umuhimu wake.
“Mafunzo haya yanalenga kwanza kabisa kuwafafanulia nini maana ya usalama mahala pa kazi, wakishaelewa hivyo basi zoezi la kutoa elimu kwetu litakuwa ni kazi rahisi. Wanafunzi wanauelewa mkubwa na ni rahisi kushika mambo, mbali na hapo wanaishi katika mazingira ambayo ni lazima wafahamu vitu hivi.” Alisema Lwakatare na kuongezea kuwa, “Kwa mfano wanafunzi ambao tunawapa mafunzo hapa shule zao zipo katikati ya jiji na kuzungukwa na barabara kuu hivyo basi lazima wapewe mafunzo haya.” Lwakatare aliendelea kwa kusema kuwa mafunzo hayo yametolewa kwa wanafunzi wa darasa la tatu, nne na tano kutoka kila shule ambazo zimetajwa hapo awali. Wanafunzi hawa wataelezwa ni kwa nini kuna umuhimu wakuzingatia mafunzo hayo kwani hata wao miaka ya baadae watakuja kuwa wafanyakazi na lazima watakuja kukumbana nazo.
“Tunategemea wanafunzi hawa siku za baadae wamalize masomo yao waje kuwa wafanyakazi na wengine wanaweza kubahatika na kuajiriwa na Vodacom. Mafunzo haya ya mara kwa mara yana faida kubwa na pia nina amini wao ndio watakuwa mabalozi kwa wanafunzi wenzao, marafiki, wazazi na hata ndugu na jamaa huko waendapo.” Alimalizia Lwakatare Kwa upande wa jeshi la polisi mkoa wa Kinondoni wao watatoa mafunzo kwa wanafunzi hao juu ya kutumia vifaa mbali mbali vya kiusalama na usalama barabarani ili kuwapa uelewa zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari kamanda wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Kinondoni, Kamanda Mohammed Mpinga amesema kuwa wanafunzi hawa wengi wao wanatumia barabara wakati wa kuja shuleni na kurudi nyumbani.
“Tumeona kuna umuhimu kwa wanafunzi hawa kujua alama mbali mbali za barabarani pamoja na matumizi yake mbali na kuishia kuziona tu kwa macho. Kama suala la usalama barabarani lazima lipewe kipaumbele kwani kama tujuavyo jiji la Dar es Salaam lina changamoto nyingi ukizingatia magari sasa yamekuwa mengi kitu ambacho kunakuwa na mikanganyiko mingi.” Alimalizia Kamanda Mpinga.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WANAFUNZI WAPATIWA MAFUNZO YA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI NA BARABARANI.”
Post a Comment