Friday, May 23, 2014

BIBI ANASWA AKIWA AMEBEBA UNGA" UWANJA WA NDEGE




Bibi mmoja raia wa Nigeria, Olabisi Ibidun Cole (65) amevunja rekodi ya umri wa watu wanaokamatwa wakiwa na dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Cole alikamatwa Jumatatu akiwa amemeza kete 82 aina ya heroini zilizokuwa zimefungwa kwenye karatasi zinazofanana na ganda la sigara, ambazo si rahisi kuonekana katika mitambo.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Alfred Nzowa zimesema pamoja na mbinu zake na kujiamini, mwanamke huyo alikamatwa kutokana na ushirikiano wa vitengo mbalimbali vya uwanja wa ndege.

Kamanda wa Polisi wa Uwanja wa Ndege, Hamisi Selemani alisema mwanamke huyo alikamatwa Mei 19, mwaka huu saa tisa alasiri akijiandaa kwenda Paris, Ufaransa kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia.

Selemani alisema raia huyo aliwasili nchini Mei 15, mwaka huu na alikaa muda wote bila ya kuwa na shughuli yoyote, jambo ambalo lilitiliwa shaka na kumkamata.

Taarifa zaidi zinasema kuwa kutokana na mbinu yake ya ufungaji wa kete, mwanamke huyo alikuwa tayari amevuka hatua ya kwanza ya ukaguzi.

Nzowa alisema baada ya kumhoji, mtuhumiwa huyo alidai kuwa aliingia nchini kwa ajili ya kutafuta soko la kuuza vipodozi na nguo.
“Wakati tukiendelea kumhoji, Kikosi Kazi cha Kuthibiti Dawa za Kulevya kilibaini na kugundua kuwa alikuwa amemeza dawa za kulevya.

Mtuhumiwa huyo aliyekuwa na hati ya kusafiria ya Nigeria, anaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.

0 Responses to “BIBI ANASWA AKIWA AMEBEBA UNGA" UWANJA WA NDEGE ”

Post a Comment

More to Read