Tuesday, May 20, 2014

BUNGE LAINGILIA KATI SUALA LA UDA




Dar es Salaam. Wakati mjadala kuhusu umiliki wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) ukiendelea kuwa tata, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imemwita Msajili wa Hazina na mwendeshaji wa shirika hilo ili kujadili suala hilo na kumaliza mgogoro wake.

Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alisema jana kuwa hatua hiyo itamaliza suala hilo ambalo limezua malumbano bungeni baina ya Serikali na baadhi ya wabunge juu ya umikili wa kampuni hiyo.
Mgogoro wa umiliki wa shirika hilo uliibuka wiki iliyopita bungeni na Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima alisema bado linamilikiwa na Serikali kwa asilimia 49 na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam asilimia 51, wakati Kampuni ya Simon Group ikisema ilishanunua asilimia 76 ya hisa za shirika hilo.

Wakati mgogoro huo ukiwa haujafikia mwisho, UDA imetangaza kuagiza mabasi 2,000 yanayotarajiwa kuingia nchini Agosti mwaka huu kwa ajili ya kuboresha huduma ya usafiri huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Simon Group, Robert Kisena amesema, “Tuna mkakati wa kununua mabasi 2,000 mwaka huu ambayo tayari tumeshayaagiza na mpaka Agosti yatakuwa yameingia. Mpaka sasa tunayo mabasi 300 yanayofanya kazi huku mengine 200 yakiwa bado yapo ‘yard’ yakisubiri kukamilika kwa taratibu za kuyatoa,” alisema Kisena.

Mabasi hayo mapya yatagharimu Sh300 bilioni na kuinua uwezo wa shirika hilo kusafirisha abiria wengi zaidi ukilinganisha na hali ilivyo sasa, huku uongozi ukijipanga kushughulikia changamoto zilizopo.
Mkurugenzi huyo aliyesisitiza kuwa anamiliki kihalali shirika hilo, aliongeza kuwa mchakato wa kusajili shirika hilo katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) unaendelea.

Akizungumza juu ya utata uliojitokeza bungeni kuhusu uhalali wa kampuni yake kuendesha na kusimamia shughuli za shirika hilo, Kisena alisema kuwa anafanya hayo yote kama mkataba unavyosema na akawashangaa wabunge wanaoonyesha kutofahamu kinachoendelea.

Kisena aliongeza kuwa katika vikao vya wanahisa na hata vile vya uongozi wa jiji vya kuiuzia kampuni yake hisa za UDA, wabunge walikuwapo na walikubaliana na ajenda zilizofikiwa kabla ya utekelezaji wake.

0 Responses to “ BUNGE LAINGILIA KATI SUALA LA UDA”

Post a Comment

More to Read