Monday, May 12, 2014

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA FAMILIA DUNIANI ITAKAYOADHIMISHWA TAREHE 15/5/2014.




Siku ya Kimataifa ya Familia huadhimishwa kila mwaka tarehe 15 Mei na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. Maadhimisho hayo yanatokana na tamko la Baraza la Umoja wa Mataifa Na. 47/237 la tarehe 20 Septemba, 1993, linalotaka Jumuiya ya Kimataifa kuwa na siku maalum ya familia.  Tanzania ikiwa ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa huungana na nchi nyingine kila mwaka kuadhimisha siku hii.

Maadhimisho haya yanatoa nafasi ya kuongeza uelewa wa jamii kuhusu masuala yanayozikabili familia za Kitanzania, kijamii, kiuchumi na kiutamaduni na hivyo kuchukua hatua za  kuboresha maadili mema na kutatua changamoto zinazofanya maadili mema kumomonyoka. Kauli mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu ni
“MALEZI BORA YA FAMILIA: MSINGI WA TAIFA IMARA.
Kauli mbiu hii inalenga kutambua wajibu wa wazazi na walezi katika kuimarisha na kuboresha malezi ya familia. Malezi bora ya familia ni msingi wa kuwa na Taifa Imara. Wadau wote wa masuala ya familia wanatakiwa kuangalia upya wajibu wao wa kuendeleza na kuimarisha familia hapa nchini. Aidha, mafanikio ambayo yamepatikana ya kuhakikisha wanafamilia wote wanapata haki zao na kuwa na maadili stahiki kama vile kuwapatia watoto malezi bora, elimu, ulinzi na afya yatakuwa ni mfano bora na hivyo kushirikisha familia nyingine kuiga mafanikio hayo.

Ni vyema wote tukajiuliza Je ni changamoto zipi zinakabili familia za kitanzania  katika malezi? Siku hizi tunashuhudia watoto katika familia nyingi wakifanyiwa ukatili wa kutisha. Na wakati mwingine wazazi hawana uelewa kuwa ukatili huu unafanywa  na ndugu au watu ambao tunaamini kuwa watoto wako salama wakiwa  nao  kama vile; walimu viongozi wa dini n.k.

Ukubwa wa tatizo la ukatili dhidi ya watoto limechangiwa vipi na malezi yetu kwa watoto? Wazazi/walezi wanauelewa gani kuhusu  masuala ya mawasiliano na jinsi watoto wao wanavyoyatumia? Watoto wanafahamu mbinu za kujilinda wenyewe dhidi ya ukatili? Wazazi / Walezi wanauelewa kiasi gani kuhusu sheria na haki za mtoto?  Haya ni maswali ambayo familia pamoja na wadau wanapaswa kuyafanyia kazi ili hatimaye kuwa na malezi bora ambayo yataimarisha Taifa letu. Sasa hivi tunashuhudia wimbi kubwa la watoto wa mitaani.  Je kama Taifa tumejipangaje kukabiliana nalo? Watoto wa kike wanaozwa na kupata mimba wakiwa na umri mdogo sana na hivyo kukosa haki ya kupata elimu na hivyo ndoto ya kuwa na maisha bora inapotea, nini kifanyike?.

Natoa wito kwa  wana familia pamoja na Taasisi zote kushiriki kikamilifu katika kuienzi siku hii muhimu.  Ni matumaini yangu kwamba kupitia maadhimisho haya familia pamoja na wadau wote watakumbushwa wajibu na mchango wao katika maendeleo ya wanafamilia zao na mchango wao katika kuboresha malezi maadili hasa ya watoto wetu.

Aidha, maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani kwa mwaka huu tutayatumia Kuzindua Kampeni Kitaifa ya Kuzuia Ukatili wa Kingono na Kijinsia kwa Wanawake.Kampeni hii inalenga kuhamasisha jamii kuwa unyanyasaji wa kijinsia ni uvunjaji wa haki za binadamu na unafifisha juhudi za kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wanaonyanyaswa.
Kampeni hii inalenga kuhamasisha na kuelimisha jamii kuacha kuwanyanyapaa wahanga wa ukatili wa kijinsia, kuweka na kuimarisha mifumo ya kisheria ili kuondoa ukatili huu na kuboresha maisha ya wahanga na pia kuwawezesha kupata huduma ya kisheria kuhakikisha wanaofanya vitendo vya unyanyasaji wanachukuliwa hatua za kisheria.  Natoa wito kwa watanzania wote tusherehekee maadhimisho haya  ya siku ya familia kwa kutafakari malezi tunayotoa katika familia zetu kama yanaridhisha na kudumisha maadili na utamaduni wetu.
Anna  T.  Maembe
KATIBU MKUU
9/5/2014

0 Responses to “TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA FAMILIA DUNIANI ITAKAYOADHIMISHWA TAREHE 15/5/2014.”

Post a Comment

More to Read