Monday, May 12, 2014

MADIWANI WAMTAKA WAZIRI MKUU "AMTIMUE" MKURUGENZI WA HALMASHAURI YAO.




BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani, limemtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda kumtafutia kituo kingine cha kazi Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Samweli Sarianga, kutokana na kushindwa kutimiza majukumu yake.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao cha Baraza la Madiwani hivi karibuni, Mwenyekiti wa baraza hilo, Shukuru Mbatto, alisema wamemuomba Waziri Mkuu kumtafutia kituo kingine mkurugenzi huyo kutokana na kushindwa kuonyesha ushirikiano kwa madiwani.

Alisema sababu nyingine ni kushindwa kutimiza majukumu yake na kuwasimamia watendaji walio chini yake katika kituo chake cha kazi.

Mwenyekiti huyo alisema kwa muda mrefu madiwani hao wameshaandika barua kadhaa kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, kuingilia kati mgogoro uliopo baina ya madiwani na mkurugenzi huyo, ili kuweza kutekeleza miradi ya maendeleo kama ilivyopangwa.

Awali katika kikao hicho, madiwani hao walikataa kupitisha taarifa ya robo ya tatu ya mapato na matumizi ya halmashauri hiyo mwaka 2012/13 kwa madai kuwa imejaa ufisadi na kuiomba Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Pwani kutuma timu ya wakaguzi, ili kufanya ukaguzi wa hesabu kwenye halmashauri hiyo.

Mbatto aliongeza kusema kilichofanywa na watendaji wa halmashauri hiyo ni dharau, kwani pamoja na madiwani kugomea taarifa hiyo katika kikao kilichowahi kufanyika huko nyuma, bado taarifa imewasilishwa mbele ya kikao hicho ikiwa imevurugwa na kujaa shaka.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Sarianga alikiri kuwapo kwa makosa katika taarifa hiyo na kuwaomba radhi madiwani hao na kuahidi kuangalia makosa yaliyopo na kuifanyia marekebisho.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Sarianga ilikataliwa na madiwani hao ambao walisisitiza kutumwa kwa wakaguzi maalumu kutoka Ofisi ya Katibu Tawala kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa fedha za miradi na mapato na matumizi ya halmashauri hiyo kabla ya madiwani hao hawajamchukulia hatua.

0 Responses to “ MADIWANI WAMTAKA WAZIRI MKUU "AMTIMUE" MKURUGENZI WA HALMASHAURI YAO.”

Post a Comment

More to Read