Friday, June 27, 2014

MBUNGE AHOJI SABABU YA MABASI YA ABIRIA KUKAA KWENYE FOLENI YA MIZANI


MWENYEKITI wa Bunge, Mussa Zungu, amehoji kama ipo sababu ya mabasi ya abiria kukaa foleni ya mizani.

Zungu alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akiongoza kiti cha spika baada ya swali la msingi  la Mbunge wa Kilolo, Profesa Peter Msolla (CCM).

Katika swali lake, Profesa Msolla alitaka kujua serikali ina mkakati gani wa kurekebisha hali ya usumbufu wanaopata abiria kutokana na msongamano mkubwa sehemu ya Kitonga.

“Kumekuwa na msongamano katika Wilaya ya Kilolo katika barabara ya Dar es Salaam kwenda Zambia, hali inayosababishwa na ufunyu wa barabara na mara nyingine kufungwa kabisa kutokana na ajali na kubomolewa barabara kutokana na mafuriko,” alisema.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Gerson Lwenge, alisema mabasi ya abiria kuwa na ulazima wa kupanga foleni inatokana na sheria ya kuyataka magari yote yanayozidi tani tatu na nusu kupitia kwenye mizani.

“Tutaiangalia sheria hiyo, ili tuone kama suala hilo linaweza kutafutiwa ufumbuzi na kubadilishwa,” alisema Lwenge.

Alieleza wizara inatambua umuhimu wa kuboresha usalama na kuondoa usumbufu katika eneo la Mlima Kitonga lenye urefu wa kilomita 8 lililopo mkoani Iringa.

“Juhudi zilizofanywa na serikali ili kuboresha barabara katika eneo la Mlima Kitonga, ni pamoja na ukarabati uliohusisha uimarishaji wa barabara kwa kuweka tabaka la zege uliogharamiwa na Serikali ya Japan kupitia JICA,” alisema.

Alisema barabara hiyo imekuwa ikifanyiwa matengenezo mbalimbali yanayojumuisha uimarishaji wa maeneo ya kuegesha magari wakati wa dharura.

Alifafanua kuwa pamoja na juhudi hizo, ili kupata suluhisho la kudumu wizara imejumuisha mradi wa uimarishaji wa usalama katika Mlima Kitonga kwenye mradi wa uimarishaji wa maeneo korofi yenye matukio mengi ya ajali katika barabara ya TAZAM kuanzia Dar es Salaam hadi Tunduma chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.


0 Responses to “MBUNGE AHOJI SABABU YA MABASI YA ABIRIA KUKAA KWENYE FOLENI YA MIZANI ”

Post a Comment

More to Read