Friday, June 27, 2014
UGOMVI WA JAJI WEREMA NA DAVID KAFULILA WACHUKUA SURA MPYA BAADA YA WAWILI HAO KUKATAA KUPATANISHWA
Do you like this story?
Mvutano kati ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG), Jaji Frederick Werema na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi),
David Kafulila umechukua sura mpya baada ya mwanasheria huyo kugoma
kupatanishwa huku akitishia ‘kumshughulikia’ mbunge huyo.
Ugomvi baina yao uliendelea jana
asubuhi nje ya Ukumbi wa Bunge muda mfupi baada ya Naibu Spika, Job Ndugai
kuahirisha kikao cha Bunge hadi leo.
Licha ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa
Azzan Zungu kumwita Jaji Werema na Kafulila akiwataka kupeana mikono kama
ishara ya kuzika tofauti zao, Jaji Werema alikataa na nusura amvamie mbunge
huyo.
Wakati akizungumza na mwandishi mara
baada ya Bunge kuahirishwa jana, Jaji Werema alikutana uso kwa uso na Kafulila
katika Viwanja vya Bunge na kuanza kumlalamikia mbunge huyo kwa kitendo chake
cha kumwita mwizi.
“Unamuona huyo jana (juzi), aliniita
mimi mwizi. Yaani mtu mzima kama mimi naitwa mwizi, kwa kweli sikupendezwa
kabisa na kauli yake,” alisema Jaji Werema huku akimfuata
Kafulila ambaye alitembea harakaharaka kumkwepa mwanasheria huyo.
Jaji Werema alisema juzi alishikwa na
jazba baada ya kuitwa mwizi lakini akasema hakuwa na nia ya kumpiga ndani ya
Ukumbi wa Bunge.
Wakati Jaji Werema akiendelea
kumlalamikia Kafulila, alitokea Zungu na kumtaka mwanasheria huyo kumsamehe
mbunge huyo... “Mheshimiwa naomba mpeane tu mikono kama ishara ya
kusameheana, yale mambo ya jana (juzi) yamekwisha.”
Lakini badala ya kukubaliana na ombi la
Zungu, Jaji Werema alihamaki huku akitaka tena kumvamia Kafulila... “Mimi
nakwambia Kafulila nitakukata kichwa, we subiri tu labda ukiniomba msamaha.”
Kafulila naye alijibu mapigo... “Huwezi
kunikata kichwa Werema, huwezi, yaani uniue, hapana huwezi tena
nakwambia huwezi.”
Wakati wakiendelea kurushiana maneno,
Zungu alikuwa katikati yao, huku akiwasihi wapeane mkono na kusameheana bila
mafanikio... “Haya mambo yamekwisha jamani, malizeni tofauti hizi.”
Kama vile alijua kuwa kauli ya kuua
ilimchanganya Kafulila, Jaji Werema huku akitembea kuelekea katika Jengo la
Utawala la Bunge alisema: “Siwezi kukuua kwa maana hiyo unayodhani, maana
kufa utakufa kwa mapenzi ya Mungu, ila tutapambana tu, nitakuonyesha.”
Kauli ya Kafulila
Akizungumza baadaye, Kafulila alisema: “Kutokana
na hali ilivyo sasa, nimeandika barua Ofisi ya Spika juu ya vitisho nilivyopewa
na Jaji Werema, kwanza jana (juzi) alitaka kunivamia pale bungeni na kunipiga,
leo (jana) asubuhi amenitishia kuwa atanikata kichwa.”
Kafulila alisema barua hiyo pia
ataipeleka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa maelezo kuwa siku za hivi
karibuni yamekuwa yakitokea matukio ya watu kutekwa, kuteswa na kutupwa
porini... “Kwa nafasi yake, Werema anaweza kufanya lolote, hivyo barua hizo
zinalenga kueleza alichokusudia kunifanyia.”
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John
Joel alipoulizwa kuhusu mvutano uliotokea juzi bungeni na barua za Kafulila
alisema Ofisi ya Bunge haijapata malalamiko yoyote.
“Jana sikuwapo bungeni lakini mpaka
sasa hakuna malalamiko yoyote yaliyoletwa katika Ofisi ya Bunge. Kama
wangeshikana mashati ndani ya Bunge hilo lingekuwa kosa la kufanya fujo
bungeni na adhabu zake zipo wazi,” alisema Joel.
Chanzo za Ugomvi
Juzi kabla ya kutoa kauli hiyo, Werema
alikuwa akitoa ufafanuzi wa muongozo ulioombwa na Kafulila kuhusu fedha
zilizokuwa katika akaunti ya Escrow iliyokuwa Benki Kuu (BoT), ambazo zimelipwa
kampuni ya PAP, inayomiliki mitambo ya Kampuni ya Independent Power
limited(IPTL).
Werema alisema fedha hizo si za
Serikali kama inavyodaiwa na Kafulila kwa kuwa fedha za Serikali hazikai katika
akaunti hiyo.
Aliendelea kufafanua kuwa taarifa
zinazotolewa zinapotosha umma kuwa serikali imetoa fedha kuilipa IPTL, wakati
ukweli ni kuwa fedha hizo ziliwekwa katika akaunti hiyo kutokana na misuguano
baina ya wanahisa wawili waliokuwa wamiliki wa IPTL.
Werema alibainisha kuwa mmoja wa
wanahisa hao, alikuwa akitaka IPTL ifilisiwe huku mwingine akipinga juu ya
jambo hilo mpaka walipouza hisa zao na kumaliza mgogoro huo, ambapo Mahakama
iliruhusu mali za kampuni hizo zipewe kwa mwanahisa mpya, PAP.
Werema alisema kuna watu walileta
bungeni vipeperushi wakidai ni ushahidi kuhusu utoaji wa fedha hizo za
akaunti ya Escrow na kuhusisha na rushwa.
"Kafulila ni miongoni mwa
wanaoeneza taarifa potofu…, kama ni tuhuma au kuna rushwa itakuja kujulikana,
tusubiri uchunguzi wa vyombo husika,” alisema.
Wakati akizungumza, Werema alitumia
mfano wa kabila la Wanyankole, aliosema kuwa wana usemi unaosema kwamba tumbili
hawezi kuamua kesi ya msituni.
Kabla ya kufafanua maana ya msemo huo,
Kafulila bila kuwasha kipaza sauti alikuwa akipiga kelele kumuita Werema kuwa
ni mtuhumiwa hivyo atangaze maslahi yake.
“Naomba nisikilize hata kama ni
mtuhumiwa nina fursa ya kusikilizwa …nisikilize wewe tumbili,” alijikuta akisema
Werema.
Baada ya kusema hivyo, Kafulila
hakukubali na yeye bila kuwasha kipaza sauti alisema: “wewe (Werema) ni
mwizi tu.”
Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa
Bunge, Zungu alimuomba Jaji Werema kukaa chini ili atoe ufafanuzi, huku Mbunge
wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) na Kafulila wakitaka kuzungumza.
Zungu alisema kwa kuwa Bunge
lilishaamua kuwa suala hilo lipelekwe Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa
(Takukuru) na kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ni
vyema kama Kafulila ana ushahidi wowote, apeleke huko.
Baada ya kutoa muongozo huo, ambao
ulisitisha malumbano, Mwenyekiti Zungu alisitisha shughuli za Bunge mpaka jioni
na kuondoka huku akisindikizwa na makatibu wa Bunge na wapambe kama kawaida.
Hatua ya Mwenyekiti wa Bunge kuondoka
katika ukumbi baada ya kusitisha shughuli za Bunge, ilimpa fursa Jaji Werema
kuweka sawa makabrasha yake na kutoka katika kiti chake, ambapo alionekana kama
vile anakwenda kumkabili Kafulila.
Wakati hilo likitokea, Mbunge wa Maswa
Mashariki, Sylvester Kasulumbai (Chadema), alihama katika kiti chake na
kukimbilia alipokuwa amekaa Kafulila.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida,
baadhi ya mawaziri walimzunguka Jaji Werema kabla hajamfikia Kafulila na
Kasulumbai.
Mawaziri hao ni pamoja na Waziri wa
Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na
Uratibu, Stephen Wassira, Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa
Sheria na Katiba, Dk Asha-Rose Migiro, Naibu Waziri wa Afrika Mashariki,
Dk Abdullah Juma Saadalla na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
George Simbachawene.
Nje ya Bunge, Kafulila na Mnyika
waliitisha mkutano na waandishi wa habari, ambapo walidai kuwa na ushahidi wa
kutuhumu baadhi ya mawaziri kusema uongo bungeni kuhusu fedha hizo za Escrow.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “UGOMVI WA JAJI WEREMA NA DAVID KAFULILA WACHUKUA SURA MPYA BAADA YA WAWILI HAO KUKATAA KUPATANISHWA ”
Post a Comment