Tuesday, July 22, 2014
MWAMBUSI AJIANDAA KUCHEZA `FAINALI 26` LIGI KUU BARA.
Do you like this story?
MSIMU uliopita wa ligi kuu soka
Tanzania bara, Juma Mwambusi wa Mbeya City fc alichaguliwa kuwa kocha bora wa
msimu baada ya kuiongoza klabu hiyo mpya kushika nafasi ya tatu katika msimamo.
Mbeya City fc walizisumbua klabu kubwa
za Simba na Yanga, hata mabingwa Azam fc. Walimaliza nafasi ya tatu mbele ya
mnyama Simba kwa kujikusanyia pointi 49 kibindoni.
Walishinda mechi 13, wakatoka sare
mechi 10 na kufungwa mechi 3. Walikula kipigo cha kwanza cha bao 1-0 kutoka kwa
Yanga ndani ya uwanja wa Taifa. Wakalala 2-0 dhidi ya Wagosi wa Kaya, Coastal
Union, Mkwakwani Tanga. Na mechi ya tatu kufungwa ni ile ya 2-1 dhidi ya Azam
fc.
Mechi hii ilipigwa uwanja wa Sokoine na
kimsingi ndio iliamua ubingwa kutua mikononi mwa wana Lambalamba.
Mwambusi ni kocha maarufu nchini, kila
timu anayoifundisha inapata mafanikio. Kumbuka alipokuwa na wajelajela Tanzania
Prisons hali ilikuwaje.
Msimu uliopita, Mwambusi alikuja na
kikosi chenye wachezaji wapya kabisa katika michuano ya ligi. Walikuwa vijana
wadogo wasio na uzoefu, lakini aliwaamini kwasababu alitoka nao ligi daraja la
kwanza ambapo alipanda kucheza ligi kuu bila kufungwa mchezo wowote.
Mwambusi ni mtu wa kuthubutu na
ukizingatia nyuma yale alikuwepo msaidizi imara, Maka Andrew Mwalwisyi, ingawa
kocha huyu mwenye leseni B ya CAF ameamua kuachana na klabu hiyo.
Anapotajwa kuwa kocha bora wa msimu,
manake aliwazidi wenzake mbinu . Mwambusi alikuwa na timu changa na alipambana
na makocha wenye timu kubwa kama Hans van Pluijm (aliyekuwa kocha wa Yanga),
Joseph Marius Omog wa Azam na Zdravko Logarusic wa Simba.
Wakati Omog, Pluijm, na Loga wakiwa na
wachezaji wa kimataifa katika vikosi vyao, Mwambusi alikuwa na vijana wa
Kitanzani, tena wengi wao wanatoka nyanda za juu kusini, hususani Mbeya.
Kwa mafanikio aliyopata kuzingatia timu
aliyokuwa nayo, tuzo ya kocha bora ilimfaa.
Lakini Mwambusi anatambua ugumu uliopo
mbele yake baada ya kuwa kocha bora msimu uliopita?
Kocha huyu anasema msimu ujao utakuwa
na changamoto kubwa kwake kwasabababu timu zote zinajiandaa na yeye ataingia
kama mshindani wa ubingwa, huku akiamini kuwa timu zitacheza naye kwa nguvu
kama ilivyo kwa Simba, Yanga na Azam fc.
Mwambusi aliongeza kuwa maandalizi ya
msimu mpya yanakwenda vizuri na atapiga kambi nje ya nchi ambapo atacheza mechi
kadhaa za kirafiki.
Tayari uongozi wa klabu hiyo ulishapewa
programu ya kocha wao, na mwenyekiti wake, Mussa Mapunda alisema watakwenda
Malawi na Zambia ambapo watacheza angalau mechi mbili mbili za kujipima ubavu.
Kocha Mwambusi alisema: “Ligi msimu
ujao itakuwa ngumu na mbele yetu kuna changamoto kubwa, lakini siku zote
tunajiandaa kwa mechi zote 26. Kila mchezo kwetu huwa unakuwa muhimu, kwahiyo
tunajiandaa vizuri”.
“Falsafa yetu sio kusajili majina
makubwa, tunawaamini vijana wetu. Timu yangu imebaki vilevile, ingawa
nimeongeza wachezaji wawili watatu”. Aliongeza Mwambusi.
Kocha huyo alisema hatishiki na makocha
wa kizungu kwasababu mbinu za mpira ni zile zile, hivyo anajiandaa vizuri
kukabiliana na changamoto hizo.
Msimu ujao, wachezaji wa Mbeya City
wanaweza kufanya vizuri ukizingatia watakuwa na uzoefu wa msimu mmoja.
Kuongezeka kwa Them Felix `Mnyama` aliyesajiliwa kutoka Kagera Sugar kutaifanya
safu ya ushambuliaji kuwa na nguvu zaidi.
Them atafanya kazi na akina Mwegane
Yeya, Paul Nonga, Deus Kaseke na Peter Mapunda.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MWAMBUSI AJIANDAA KUCHEZA `FAINALI 26` LIGI KUU BARA.”
Post a Comment