Wednesday, August 27, 2014
ADA YA SEKONDARI KUFUTWA.....RAIS KIKWETE AAHIDI ELIMU BURE.
Do you like this story?
Serikali inajipanga kufuta ada za
sekondari, ili elimu kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne, itolewe
bure.
Rais Jakaya Kikwete, alisema hayo juzi
katika mkutano wake na wanajumuiya ya Chuo Kikuu cha Mzumbe cha Morogoro, na
wakazi wa vijiji vya jirani na chuo hicho, katika ziara yake inayoendelea
katika Mkoa wa Morogoro iliyoanza Agosti 20.
“Sasa hivi tunaangalia jinsi ya kufuta
karo katika shule zetu zote za sekondari za Serikali, ili kuhakikisha kila
mtoto anayeanza darasa la kwanza, awe na nafasi ya kumaliza sekondari kwa maana
ya kidato cha nne, bila kulazimika kuacha shule kwa sababu ya ada.
“Tunaangalia kuondoa ada hii, ambayo
wazazi wanalipa Sh 20,000 kwa shule za kutwa na Sh 70,000 kwa shule za bweni,
ili watoto wetu waingie darasa la kwanza, na kwenda moja kwa moja hadi kidato
cha nne bila wasiwasi wa kukwamishwa na ada,” alisema Rais Kikwete.
Kwa hatua hiyo, Rais Kikwete alisema
mbali na kulenga kuinua elimu, pia itawapunguzia mzigo wazazi na walezi wa
watoto wanaosoma katika shule hizo za sekondari za Serikali.
Alisema zipo sababu za msingi
zinazokwamisha wanafunzi wengi wa shule za sekondari, kuendelea na masomo yao
kutokana na wazazi wao kushindwa kulipia karo ya shule, kutokana na changamoto
mbalimbali zikiwemo za umasikini.
Rais Kikwete alisema pamoja na kejeli
nyingi zilizoelekezwa kwa shule za sekondari za kata, kiasi cha kuitwa Yeboyebo
katika miaka ya mwanzoni ya shule hizo, bado zimekuwa na mafanikio makubwa,
ambayo ni sehemu ya mafanikio ya Sekta ya Elimu katika miaka karibu tisa ya
uongozi wake.
Akielezea historia ya kuanzishwa kwa
shule za sekondari za kata, Rais Kikwete alisema wakati alipokuwa akiingia
madarakani, hali ya watoto kuingia sekondari kutoka shule za msingi ilikuwa
mbaya.Kwa mujibu wa Rais Kikwete, hali hiyo ilisababisha asilimia kati ya sita
na kumi tu ya wanafunzi waliomaliza darasa la saba, kusonga mbele kwa sababu
shule za sekondari zilikuwa chache.
“Kwa miaka mingi, hatukujenga shule
mpya za sekondari na kama mnavyojua, Wakoloni wa Kiingereza ndio kabisa
hawakujenga shule. Kazi hiyo waliwaachia Wamisionari. Kwa hiyo wakati tunaingia
madarakani, hali ilikuwa mbaya ndiyo maana tukaja na Sera ya Shule za Kata,” alisema Rais
Kikwete.
Alisema takwimu rasmi zinaonesha
kwamba, kulikuwa na shule za sekondari 1,745 mwaka 2005, zikiwemo shule
1,202 za Serikali na sasa ziko shule za sekondari 4,576, zikiwemo shule 3,528
za Serikali.
Mafanikio hayo ya kupanuka kwa sekta ya
elimu, kwa mujibu wa Rais Kikwete, yalileta changamoto hasa ya ukosefu wa
walimu wa masomo ya sayansi. Alisema Serikali imepambana na changamoto hiyo na
zingine zilizojitokeza, ambapo sasa wapo walimu karibu wa kutosha wa masomo
hayo kwa shule za sekondari zote nchini.
Mbali na kusudio la kufuta ada, Rais
pia alisema Serikali inaandaa utaratibu maalumu utakaowezesha kujenga
mabweni katika shule za msingi na sekondari zilizopo maeneo ya jamii ya
wafugaji.
Alisema lengo ni kuwawezesha watoto wa
jamii hiyo, waendelee kusoma hata pale wazazi na walezi wao wanapohama kutoka
eneo moja kwenda jingine kufuata malisho ya mifugo yao.
“Tuna tatizo kubwa katika eneo
hili...watoto wengi wa wafugaji wanakatishwa masomo kutokana na wazazi ama
walezi kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine kufuata malisho...wanaohama
wanaondoka na watoto wao wote na kuwakosesha fursa ya kusoma,” alisema Rais.
Kuhusu elimu ya juu, Rais Kikwete
alisema kwa sasa kuna vyuo vikuu 51, vikiwemo 15 vya umma na pia kuna
ongezeko la fedha za mikopo ya elimu kutoka Sh bilioni 16 mwaka 2005 na kufikia
Sh bilioni 345 kwa sasa.
Mbali na ongezeko la fedha za mikopo ya
elimu ya juu, Rais Kikwete alisema wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya
juu waliongezeka kutoka wanafunzi 16,000 mwaka 2005 hadi kufikia 95,000 kwa
sasa.
Awali Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe,
Profesa Joseph Kuzilwa, alipongeza Serikali kwa kukuza mitaala ya wanafunzi wa
vyuo vikuu na kushauri kuwa ili wanafunzi washindane katika soko la ajira, upo
umihimu wa mitaala kuendelea kuboreshwa.
Alimwomba Rais Kikwete kusaidia
kuboresha miundombinu mbalimbali ya chuo hicho kutokana na uchakavu wa majengo
yake.
Naye Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa
Chuo hicho, Boniface Maiga, alitaja changamoto kubwa zinazowakabili kuwa
ni pamoja na uhaba wa sehemu za malazi uliosababishwa na idadi kubwa ya
wanafunzi wanaodahiliwa na uchakavu wa miundombinu.
Alisema licha ya Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB), kutoa mikopo hiyo kwa wakati, bado
kuna malalamiko mengi kuhusu watoto wa matajiri na wenye uwezo, ambao
wameendelea kupewa mikopo.
Aliiomba serikali kufanyia utafiti
suala hilo na ikibaini hali hiyo, fedha hizo zitolewe kwa watoto wengi
masikini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ADA YA SEKONDARI KUFUTWA.....RAIS KIKWETE AAHIDI ELIMU BURE.”
Post a Comment