Saturday, August 2, 2014
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA UGONJWA WA EBOLA.
Do you like this story?
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
Mnamo mwezi wa Machi 2014 Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilipokea
taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu ugonjwa wa Ebola katika
nchi za Afrika Magharibi ambao ulianzia katika ya Guinea na kusambaa katika
nchi za Siera Leone, Liberia na Nigeria. Hadi tarehe 31 Julai, 2014 idadi ya
wagonjwa ilikuwa 1323 na vifo 729.
Ugonjwa wa Ebola husababishwa na virusi vya Ebola. Dalili zake ni homa
kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kuuma kichwa, na vidonda
kooni. Mara nyingi dalili hizo hufuatiwa na kutapika, kuharisha, vipele vya
ngozi, figo na ini kushindwa kufanya kazi na kwa baadhi ya wagonjwa kutokwa
damu ndani na nje mwilini. Kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa ni kati
ya siku 2 hadi 21 baada ya kupata maambukizi.
Ugonjwa wa Ebola unaambukiza kwa kasi na unaenea kati ya mtu na mtu
kwa:
o kugusa damu na
majimaji kutoka mwilini mwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo
o kugusa maiti wakati
ya mtu aliyekufa kwa ugonjwa huu.
o kugusa wanyama
walioambukizwa Mizoga na wazima kama vile sokwe na swala wa msitu.
Aidha Ugonjwa wa Ebola hauna tiba wala chanjo.
Hadi sasa hapa nchini Tanzania hakuna mgonjwa
yoyote aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa virusi vya Ebola.
Wizara ya Afya na ustawi wa Jamii imeandaa mikakati ya kuzuia
ugojnwa huu usiingie hapa nchini na ikiwa utaiingia uweze kudhibitiwa kabla
haujasambaa. Mikakati hiyo ni pamoja na:
o Kuunda kikosi kazi
(Task Force) kinachohusisha wajumbe mbalimbali wakiwemo wadau wa
maendeleo ikiwa ni pamoja na WHO, UNICEF, USAID na CDC kwa ajili ya
kuweka mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huu ikwa ni pamoja na kusimamia
utekelezaji wa mpango wa dharura wa kukabiliana na Ebola ambao tayari umeandaliwa.
o Kutoa taarifa ya
tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Makatibu Tawala na Waganga Wakuu wote wa
Mikoa. Aidha taarifa hii pia imejumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa
(Ainisho la Ugonjwa), “Fact sheet” ya ugonjwa, Mwongozo kwa watumishi wa
afya wa namna ya kuchukua sampuli, na na namna ya kuwahudumia wagonjwa.
o Kuboresha ufuatiliaji
na utambuzi wa ugonjwa katika maeneo ya viwanja vya ndege na mipakani ili
kuweza kubaini wasafiri watakaoonyesha dalili za ugonjwa au wenye viashiria
hatari. .
o Miongozo ya utoaji
elimu imeandaliwa ikiwemo Vipeperushi. Aidha watalaamu wa Afya wanaendelea
kutoa elimu kwa wananchi kuhusu dalili za ugonjwa huu kupitia vyombo mbalimbali
vya habari ili endapo ugonjwa huo ukitokea uweze kutolewa taarifa mapema
o Vifaa kinga (Personal Protective Gears) vipo vya
kutosha na Wizara imeanza kuvisambaza kutoka bohari za kanda za MSD na
kuzipeleka kwenye vituo vya kutoa huduma za afya ili watumishi wa afya waweze
kutumia iwapo mgonjwa atajitokeza. Aidha idadi itaongezwa kadiri ya mahitaji
yatakavyojitokeza.
o Wizara imebainisha
vituo vya kutolea huduma kwa mikoa yote iwapo endapo ugonjwa huu utatokea hapa
nchini. Aidha katika vituo hivi, vifaa kinga pamoja na madawa vimeshaandaliwa.
o Kuwasiliana na wadau
mbalimbali ikiwemo wadau wa maendeleo ili kuweza kupata msaada wa mahitaji
mbalimbali kama yalivyoainishwa kwenye mpango wa dharura wa kukabliana na Ebola
ulioandaliwa.
Hitimisho
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu ila kuendelea kuchukua tahadhari
za kujikinga na ugonjwa huu. Ugonjwa wa
Ebola unaweza kuzuilika. Njia kuu za kujikinga na ugonjwa huu ni:-
o Kuepuka kugusa au
kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho, kinyesi, machozi na majimaji
mengine yanayotoka mwilini mwa mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola
o Wananchi
wanatahadharishwa kuepuka kushughulikia maiti ya mtu aliyekufa akiwa na
dalili za Ebola; badala yake watoe taarifa kwa uongozi wa kituo cha huduma za
Afya kwa ushauri.
o Wananchi waepuke mila
na desturi zinazoweza kuchelewesha kupata huduma muhimu na kuzidi kueneza
ugonjwa wa Ebola.
o Zingatia
usafi wa mwili tabia
na kiroho.
o Kutoa taarifa mapema
kwa viongozi wa Serikali na wa huduma za Afya katika ngazi zote pale anapotokea
mtu mwenye dalili za Ebola.
o Kuwahi katika vituo
vya huduma za Afya pale mtu anapoona dalili za ugonjwa huu.
Wizara itaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali kuimarisha
ufuatiliaji ili kudhibiti ugonjwa huu usiingie nchini.
Charles A. Pallangyo
Katibu Mkuu
01 Augus,t 2014
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA UGONJWA WA EBOLA.”
Post a Comment