Friday, September 26, 2014

UDA YAWAFUKUZA KAZI MADEREVA 12





SHIRIKA la Usafiri Dar es Salaam (UDA) limewafukuza kazi madereva wake 42 kwa makosa mbalimbali, yakiwemo utovu wa nidhamu.

Makosa mengine yaliyosababisha wafukuzwe kazi ni, kuvunja sheria za barabarani kwa makusudi, kukatisha njia kinyume cha taratibu na kutoza nauli zisizo rasmi tofauti na zilizopo kwenye tiketi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Msemaji wa Uda, George Maziku alisema wamefukuzwa kutoka vituo vya kazi vya shirika ambavyo ni Gongo la Mboto, Mbagala, Kamata na Boko 2.
Alisema shirika limefikia uamuzi huo baada ya kuridhishwa na matokeo ya uchunguzi uliofanywa na kikosi kazi chake cha kufuatilia mwenendo wa madereva wawapo barabarani.

Alitaja makosa mengine ni kufanya kazi wakiwa wamelewa, kutoa lugha chafu kwa askari wa usalama barabarani na kwa abiria pamoja na kukithiri kwa uchafu.

“Sisi tumewafukuza kazi kutokana na makosa ambayo nimeyasema hapo mwanzo, UDA hatuwezi kuvumilia watu wa namna hii wanaofanya makosa makusudi bila kuzingatia taratibu na kanuni zilizopo za usafiri usafiri wa umma,” alisema Maziku.

Kwa mujibu wa Maziku, lengo la Uda ni kuboresha sekta ya usafiri wa umma katika jiji la Dar es Salaam na kuwaondolea wateja kadhia.

Aidha alisema shirika limekuwa likichafuliwa na madereva wazembe wenye tabia mbovu kiutendaji, wanaoonesha sifa mbaya kwa jamii.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi mkoa wa kipolisi wa Ilala jijini Dar es Salaam, kwa kushirikiana na mkufunzi wa chuo cha udereva cha Lumumba, Tilya Condrad wametoa mafunzo ya usalama barabarani kwa madereva 40 wa UDA.

Mafunzo hayo yalitolewa jana ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani.

Mkufunzi huyo alipongeza shirika kwa kujali abiria wake kwa kutilia uzito mafunzo ya usalama barabarani kwa madereva wao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti madereva hao walisema kuwa ni mpango mzuri unaofanywa kuwajengea ufahamu juu ya umuhimu wa usalama barabarani.

0 Responses to “UDA YAWAFUKUZA KAZI MADEREVA 12 ”

Post a Comment

More to Read