Sunday, October 26, 2014

MOI YATOA TAARIFA, YADAI BODABODA HUUMIZA VICHWA VYA WATU 600 KILA MWEZI




TAASISI ya Tiba ya Mifupa Muhimbili( MOI), imesema kwa mwezi inapokea wagonjwa 600 walioumia vichwa kutokana na ajali za Pikipiki.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa taasisi hiyo, Patrick Mvungi, alisema ajali hizo zinasababishwa na madereva pamoja na abiria kushindwa kuvaa kofia ngumu pindi wanapokuwa barabarani.

Mvungi, alisema taasisi hiyo ikiwa katika kipindi cha mpito cha mageuzi ya utoaji huduma za afya nchini, imefanikiwa kwa asilimia 95 kutoa huduma muhimu za tiba na upasuaji kwa wagonjwa na hivyo kupunguza vifo na rufaa za kusafirisha wagonjwa nje ya nchi.

Alisema zaidi ya wagonjwa 4,500 wa mifupa wamepatiwa huduma kwa kutumia utaalamu wa kufanyiwa upasuaji na kuwekewa kifaa maalum (Sign Nail), kwa wagonjwa waliovunjika mifupa kinachowasaidia kupona mapema na kurudi katika hali zao za kawaida.

“Kwa upande wa Upasuaji Mkubwa wa Nyonga (Total Hip Replacement), zaidi ya wagonjwa 1,256 walipasuliwa salama na wamepona, huku zaidi ya wagonjwa 703 wakifanyiwa upasuaji mkubwa wa kubadilisha viungo vya goti vilivyoharibika (Total Knee Replacement), kwa kuweka vifaa   maalum vya bandia (Artificial Implants), ambapo zaidi ya 95 ya wagonjwa wameweza kutembea na kurudi katika hali zao za kawaida,” alisema.

Mvungi, alisema taasisi hiyo pia imefanikiwa kutoa matibabu kwa wagonjwa ya ubongo (Brain Surger diseases), waliokuwa wakihitaji upasuaji kwa zaidi ya asilimia 80.


0 Responses to “ MOI YATOA TAARIFA, YADAI BODABODA HUUMIZA VICHWA VYA WATU 600 KILA MWEZI ”

Post a Comment

More to Read