Monday, October 27, 2014

MTIBWA KILELENI MWAMBUSI APEWA ULINZI


Kocha msaidizi wa Timu ya Mbeya City Suleiman Jabir akimtoa nje Mchezaji Paul Nonga mara baada ya mchezo kuisha

Kikosi cha Timu ya Mtibwa

Kikosi cha Timu ya Mbeya City










Mashabiki wa Mbeya City wakikimbia mara baada ya kuanzisha fujo uwanjani




TIMU ya Mtibwa ya mjini Morogoro imeifundisha kabumbu timu ya Mbeya City kwa kuilambisha jumla ya magoli 2-0 katika uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine Jijini Mbeya.

Mbeya City ambayo imepoteza mechi ya pili katika uwanja wa nyumbani baada ya wiki iliyopita kufungwa na Azam 1-0, ilishindwa kuutawala mpira katika dakika zote za mchezo.

Mpira ulianza kwa kasi huku kila timu ikijitahidi kusaka bao lakini dakika ya 21 ya mchezo mpira wa kona uliopigwa na David Luhende na kumkuta Amri Ally aliyeutingisha wavu wa Mbeya City.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Mbeya City walikuwa nyuma kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kama ilivyokuwa katika kipindhi cha kwanza timu zilishambuliana kwa zamu huku, Mtibwa wakilihami goli lao na kutaka kuongeza bao nao Mbeya City wakijitahidi kulishambulia lango la Mtibwa bila mafanikio.

Kila timu ilifanya mabadiliko katika kipindi cha pili ambapo kwa upande wa Mtibwa Mussa Mgosi alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Vicent Barnabas ilhali Mbeya City ilimtoa Saad Kipanga na nafasi yake kuchukuliwa na Mwagane Yeya.

Mabadiliko hayo ya kila timu yalibadilisha kidogo hali ya mchezo ambapo ari na nguvu mpya ya mpira ilianza kuonekana kwa kila upande.

Hata hivyo ilikuwa ni dakika ya 78 ya mchezo mchezaji wa Mtibwa aliyeingia kipindi cha pili Vicent Barnabas aliwainua wapenzi wake kwa kuifungia Mtibwa bao la pili na kuzua kizaazaa kwa upande wa mashabiki wa Mbeya City ambao walianza kuwarushia mawe na chupa za maji wachezaji wa Mtibwa ambao walikuwa wakishangilia bao hilo.


Hali hiyo ilisababisha kikosi cha kutuliza ghasia kuwasha gari lake la washawasha na kutoa alama ya tahadhari kwa kupiga honi na king'ora.

Jukwaa la mashabiki wa Mbeya City lilibaki wazi huku hamasa za kushangilia zikipungua ilhali ndani ya uwanja wachezaji wa Mbeya City walionekana kupanic kwa kucheza mpira wa piga nikupige huku wenzao wa Mtibwa wakituliza mpira chini.

Hadi kipyenga cha mwisho Mtibwa walikuwa wakiongoza kwa bao 2-0 ambapo mashabiki wa timu ya Mbeya City walionekana kutoamini matokeo hayo huku wachezaji wa Mbeya City wakitahayari na kuendelea kubaki katikati ya uwanja.

Katika hatua nyingine wachezaji wa Mbeya City walisusia kupanda gari lao na kutembea kwa miguu kutoka nje ya uwanja kuelekea kambini katika hoteli ya Holiday iliyopo jirani na uwanja huo. Mashabiki wa timu hiyo walisikika wakimlaani wazi wazi kocha wao Juma Mwambusi na kusema kuwa hawamtaki kwa kuwa ameshindwa kuifundisha timu hiyo.

0 Responses to “MTIBWA KILELENI MWAMBUSI APEWA ULINZI”

Post a Comment

More to Read