Tuesday, October 21, 2014
RAIS KIKWETE AANZA ZIARA RASMI YA CHINA LEO
Do you like this story?
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiagwa na maafisa wa Ubalozi wa China
nchini Tanzanioa wakati akiondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere jijini Dar es salaam usiku wa kuamkia leo tayari kuanza
ziara rasmi ya siku sita katika Jamhuri ya Watu wa China kwa mwaliko wa Rais Xi
Jinping. PICHA NA IKULU
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Oktoba 21, 2014, anaanza ziara rasmi ya
siku sita katika Jamhuri ya Watu wa China kwa mwaliko wa Rais Xi
Jinping, ikiwa ni ziara yake ya pili nchini humo akiwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano.
Baada ya China, Rais Kikwete atafanya ziara rasmi ya siku tatu
nchini Vietnam kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo. Wakati wa ziara yake nchini China, Rais
Kikwete ambaye aliondoka
nchini usiku wa jana, Jumatatu, Oktoba 20, 2014, atatembelea majimbo matatu ya nchi hiyo, atafanya mazungumzo na viongozi wakuu wa China, atashuhudia utiaji saini mikataba muhimu ya shughuli za maendeleo, atatunukiwa shahada za heshima na atashiriki katika sherehe za miaka 50 tokea kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya Tanzania na
China.
Rais Kikwete amepangiwa kukutana na kufanya mazungumzo na
mwenyeji wake, Rais Xi Jinping; Waziri Mkuu Mheshimiwa Li Keqiang pamoja
na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Zhang Dejiang. Rais Kikwete pia atashuhudia utiaji saini wa
mikataba ya miradi ya maendeleo ya Tanzania ambayo inasaidiwa ama
inagharimiwa na fedha kutoka China na pia atakutana kwa mazungumzo na
wakuu wa taasisi muhimu zinazogharimia baadhi ya miradi mikubwa ya
maendeleo katika Tanzania zikiwamo China-Africa Development Fund (CADB) na
China Development Bank (CDB).
Akiwa Beijing, Rais Kikwete atakutana na Mabalozi wa Afrika wanaoziwakilisha
nchi zao katika China, atafungua Mkutano wa Tatu wa Biashara na Uwekezaji
kati ya Tanzania na China na atazindua rasmi Kijiji cha Kiafrika.
Aidha, Rais Kikwete atatunukiwa uprofesa wa heshima na Chuo Kikuu
cha Kilimo cha China cha China Agricultural University na Chuo Kikuu
cha East China Normal University na pia atakuwa mwenyeji wa hafla
maalum ya kusherehekea miaka 50 ya uhusiano wa kibalozi kati ya Tanzania
na China.
Uhusiano huo ulitimiza miaka 50, Aprili 26, mwaka huu, siku ambako
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia ilitimiza miaka 50 ya kuzaliwa kwake.
Baada ya kumaliza ziara yake Beijing, Rais Kikwete atatembelea
Jimbo la Jinan ambako atashuhudia maonyesho rasmi ya kijeshi ya Jeshi
la Ukombozi la Wananchi wa China la Chinese People’s Liberation
Army (PLA) lililoandaliwa rasmi kwa heshima yake. Hiyo itakuwa mara
ya kwanza katika historia kwa heshima ya namna hiyo kutolewa kwa kiongozi
wa nchi yoyote duniani, nje ya China.
wa nchi yoyote duniani, nje ya China.
Akiwa Jimbo la Jinan, Rais Kikwete pia atakutana na viongozi wa
Jimbo hilo na pia atakutana kwa mazungumzo na madaktari wa Kichina
ambao wamefanya kazi katika Tanzania katika miaka 50 iliyopita.
Baada ya Jimbo la Jinan, Rais Kikwete atakwenda Jimbo la
Shenzhen ambako atatembelea makao makuu ya taasisi na makampuni makubwa
ya China ya Shenzhen Economic Zones Authority, China Merchants
Holdings International (CMHI), Huawei na ZTE. Shenzhen ndiko Watanzania
wengi wanaonunua bidhaa kutoka China hufanyia biashara zao.
Mara ya mwisho, Rais Kikwete alitembelea China mwaka 2008
wakati alipoliwakilisha Bara la Afrika katika Mkutano wa Kwanza
wa China-Afrika katika nafasi yake wakati huo kama Mwenyekiti wa Umoja
wa Afrika (AU).
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
21 Oktoba,2014
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
21 Oktoba,2014
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “RAIS KIKWETE AANZA ZIARA RASMI YA CHINA LEO”
Post a Comment