Thursday, October 2, 2014

RAIS KIKWETE ATANGAZA HATUA SABA ZA KUKABILIANA NA MSONGAMANO WA MAGARI JIJINI DAR




Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametaja
hatua saba ambazo Serikali yake imeanza kuzichukua ama inakusudia kuzichukua
ili kukabiliana na msongamano wa magari katika Jiji la Dar Es Salaam.

Aidha,
Rais Kikwete amesema kuwa msongamano wa magari ni ishara ya ubora wa maisha ya
wananchi na ustawi wa Watanzania kwa sababu miaka 20 ama hata 10 iliyopita,
Jiji la Dar Es Salaam halikuwa na msongamano.

“Sasa kila mtu ana gari, naambiwa
nyumba nyingine zina magari matatu – la baba, la mama na la watoto.” alisema.

Hata
hivyo, Rais Kikwete ameonya kuwa, kama ilivyo katika miji yote mikubwa duniani,
ni jambo lisilowezekana kumaliza tatizo la msongamano wa magari katikati ya
Jiji la Dar Es Sslaam (Central Business
District), hasa kwa kutilia maanani kuwa hakuna shaka kuwa watu wataendelea
kununua magari na huwezi kuvunja nyumba zote katikati ya Jiji ili kupanua
barabara.

Rais
Kikwete ambaye alikuwa anazungumza leo, Jumatano, Oktoba Mosi, 2014, wakati
akizindua rasmi Barabara kisasa ya Mwenge -Tegeta kwenye Barabara ya New
Bagamoyo Road, amezitaja hatua hizo za kukabiliana na msongamano wa magari
katika Mji wa Dar Es Salaam kuwa ni pamoja na ujenzi wa njia ya Mabasi Yaendayo
Kasi (DART), ambao awamu yake ya
kwanza inakaribia kukamilika pamoja na uanzishwaji wa huduma za kisasa za
usafiri wa treni katika maeneo mbali mbali ya jiji hilo.

“DART
inalenga kuwashawishi wananchi kupunguza matumizi ya magari binafsi na kutumia
zaidi usafiri wa umma. Na hili litawezekana ikiwa mabasi yenyewe yatakuwa
mazuri na huduma ikawa bora,” amesema Rais
Kikwete na kuongeza:

“Usafiri
wa treni ambao nausema mimi ni usafiri wa treni za kisasa zenye mabehewa ya
kubeba abiria mijini siyo ule wa sasa ambako mabehewa ya kwenda Kigoma na
Mwanza ndiyo yanatumika kubeba abiria kati ya Dar Es Salaam na Tabata.”

Hatua
ya tatu ambayo Rais Kikwete ameitaja ni kujengwa kwa barabara za juu kwa juu (flyovers) katika maeneo ya TAZARA na
Ubungo, yenye msongamano wa watu wengi, na ujenzi wa barabara 12 za kuzunguka
Jiji (Ring Roads) na nyingine za kuunganisha
maeneo ya jiji hilo kama vile upanuzi wa Barabara ya Uhuru kuwa njia mbili kila
upande badala ya njia moja ya sasa.

Aidha,
Rais Kikwete amezitaja hatua nyingine kuwa ni ujenzi wa Daraja jipya la Salender
ambalo litapitia baharini, usafiri wa kivuko kipya kutoka Bagamoyo hadi Dar Es
Salaam na ujenzi wa miji midogo ya kisasa inayojitegemea katika maeneo ya
Kigamboni, Mabwepande na Luguruni.

Rais
Kikwete amesema kuwa baadhi ya hatua hizo zinazochukuliwa ama zinalengwa
kuchukuliwa na Serikali zimekuwa zinakabiliwa na siasa nyingi za kupinga miradi
hiyo kutoka kwa baadhi ya viongozi na wanasiasa nchini ambao amewaita “watu
wenye upeo mfupi”.

“Kiongozi
anayehubiri upinzani wa maendeleo kwa sababu za siasa ni kiongozi mbovu. Huyu
ni mtu mwenye uongozi mbovu, na ana upeo mfupi, usiiona mbali, kwa sababu
kiongozi mzuri hawezi kuhubiri siasa za kupinga maendeleo ya wananchi wake.”




Imetolewa na;

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu
– Dar es Salaam.

1 Oktoba, 2014.

0 Responses to “RAIS KIKWETE ATANGAZA HATUA SABA ZA KUKABILIANA NA MSONGAMANO WA MAGARI JIJINI DAR ”

Post a Comment

More to Read