Wednesday, October 29, 2014
RAIS WA ZAMBIA MICHAEL SATA AFARIKI DUNIA
Do you like this story?
Familia ya Bwana Sata imesema kuwa Rais wa Zambia,
Michael Sata, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 77 katika hospitali ya
London alikokuwa akitibiwa ugonjwa ambao haujatajwa. Kifo chake kimetokea siku
chache baada ya Zambia kusherehekea miaka 50 ya uhuru wa nchi hiyo.
Mwanasiasa huyo mkongwe aliingia madarakani mwezi Septemba 2011 baada ya
kuongoza chama chake cha Patriotic Front, na kumshinda Rupiah Banda, ambaye
alikuwa rais wakati huo na chama chake cha Movement for Multi-Party Democracy,
kikiwa madarakani kwa miaka ishirini.
Michael Chilufya Sata alizaliwa mwaka 1937 katika mji wa Mpika, eneo
ambalo lilikuwa wakati huo ni Northern Rhodesia. Muumini wa dini ya Kikristo ya
madhehebu ya Katoliki, alifanya kazi kama afisa polisi, mfanyakazi wa reli na
mwanachama wa chama cha wafanyakazi wakati wa utawala wa kikoloni. Baada ya
Zambia kupata uhuru wake, pia aliishi kipindi fulani mjini London, akiwa
mfanyakazi wa reli, na kurejea Zambia, akiwa na kampuni ya teksi.
Akiwa mwenye sauti ya mkwaruzo yakiwa ni matokeo ya kuvuta sigara kwa
muda mrefu, Bwana Sata aliibuka katika siasa na kupata umaarufu katika miaka ya
1980.
Haraka akapata sifa ya kuwa gavana mwenye kuchapa kazi kwa bidii, wakati
akiongoza jimbo la Lusaka na mtu wa utekelezaji kwa vitendo.
Lakini pia alijulikana kama mtu wa kutoa amri, mtu asiyeendekeza urafiki
na mkali- na wapinzani wake walisema jina alilopewa la bandia la "King
Cobra" alikuwa anastahili kuitwa hivyo.
Kwa mara ya kwanza alionekana kama mtu ambaye angetekeleza ahadi za
kupambana na rushwa na kupata ufumbuzi wa tatizo la ajira na kuleta ustawi wa
jamii. Lakini kipindi chake madarakani kiligubikwa na kuuzima upinzani wa
kisiasa na kudorora kwa uchumi.
Bwana Sata ni rais wa pili wa Zambia kufariki dunia akiwa madarakani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ RAIS WA ZAMBIA MICHAEL SATA AFARIKI DUNIA”
Post a Comment