Tuesday, October 21, 2014
WANAFUNZI WAWILI WATAFUNWA NA MAMBA WALIPOKWENDA KUOGA MTONI
Do you like this story?
WANAFUNZI wawili wa shule za msingi za Nyabisara
(Murito) na Kerende Kata ya Kemambo wilayani Tarime, Mara wameumwa hadi
kuondolewa nyama zao za miguu na mamba walipokwenda kuoga maji ya mto kwa
nyakati tofauti.
Wanafunzi hao ni
Penina Joseph Mangure (11) wa darasa la nne Shule ya Msingi Nyabisara
katika Kijiji cha Murito ambaye ni mtoto wa mwenyekiti wa kijiji hicho, Joseph
Mangure na Stephano Stephano (11) pia wa darasa la nne Shule ya Msingi
Kerende.
Taarifa za madenti
hao kukutwa na mkasa huo zilifikishwa katika Kituo cha Polisi Nyangoto
(Nyamongo) na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime na
Rorya, Lazaro Mambosasa.
Akizungumza hivi
karibuni, baba wa Penina alisema mwanaye aliokolewa na wananchi
baada ya kupiga kelele wakati akiwa ameshikilia nyasi zilizomsaidia kushindwa
kutumbukizwa majini na mamba huyo ambaye alikwenda na kipande cha nyama ya mguu
wa kushoto.
Kwa upande wake mtoto
Stephano alidaiwa kukutwa na tukio hilo alipokuwa akioga maji ya mto huo wakati
akichunga ng’ombe wa nyumbani kwao.
Mtoto huyo
alifanikiwa kuokolewa na wasamaria wema alipokamatwa na mamba huyo baada ya
kupiga kelele na kufanikiwa kumtoa mguu katika mdomo wa mamba lakini akiwa
ameshamnyofoa kipande cha nyama mguu wa kushoto pia.
Mwenyekiti huyo
alisema tangu Januari hadi Oktoba mwaka huu, watu watano wa kijiji chake
wameshapoteza maisha baada ya kuliwa na mamba kwa nyakati tofauti huku wengine
takribani 100 wakijeruhiwa.
Pia mwenyekiti huyo
alisema mto huo kupita katika makazi ya watu ni tatizo na kwamba kila mara
wananchi wanapopatwa na adha hizo huwasilisha taarifa katika Halmashauri ya
Wilayani Tarime kupitia kitengo cha wanyama pori kwa ajili ya kusubiri hatua
zaidi.
Alimuomba Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyarandu kuhakikisha inawafidia wote waliojeruhiwa
au kupotozewa maisha na mamba hao.
Watoto hao bado
wanasota majumbani mwao baada ya tiba ya awali huku wazazi wao wakitafuta fedha
ili wapelekwe Hospitali ya Bugando, Mwanza kwa matibabu zaidi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WANAFUNZI WAWILI WATAFUNWA NA MAMBA WALIPOKWENDA KUOGA MTONI ”
Post a Comment