Saturday, April 18, 2015

AJALI TATU VIFO 40 NDANI YA SIKU SITA.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Mohamed Msangi.




MSHITUKO wa matukio ya mfululizo ya ajali, umeendelea kugubika nchi, baada ya watu 20 kupoteza maisha katika ajali ya basi dogo aina ya Toyota Hiace, iliyotokea jana wilayani Rungwe mkoani Mbeya.
Ajali hiyo ambayo taarifa na picha zake zilisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii, imesababisha taharuki kutokana na ukaribu wake na matukio mengine ya ajali yaliyotokea wiki hii.
Tangu Jumapili iliyopita mpaka jana, siku zisizozidi sita kumetokea ajali kubwa tatu zilizohusisha mabasi ya abiria na kuteketeza maisha ya watu 40.
Mbali na ajali hizo, wiki hii Kamanda wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga alitoa takwimu zilizosababisha huzuni kwa Watanzania, kwamba kati ya Januari mosi na Aprili 12 sawa na siku 102, watu 969 walipoteza maisha katika ajali za barabarani.

Jumatano wiki hii, basi la Air Jordan lililokuwa likitokea mkoani Mwanza kwenda Arusha, lilipata ajali na kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi 20.
Ajali hiyo ilitokea wakati Watanzania wakiwa na kumbukumbu ya ajali iliyotokea Jumapili ya wiki jana, ambapo watu 19 waliteketea kwa moto, baada ya basi la Kampuni ya Nganga Express na lori aina ya Fuso kugongana uso kwa uso na kuwaka moto katika eneo la Iyovi, Milima ya Udzungwa, mkoani Morogoro.

Akizungumza jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Mohamed Msangi, alisema ajali hiyo mpya imetokea katika eneo la Ilongo ambalo limebatizwa jina la Uwanja wa Ndege karibu na Kiwira, ambapo watu 18 walipoteza maisha papo hapo.
“Watu wanne waliojeruhiwa, mmoja alikuwa katika hali mbaya na kwa bahati mbaya alifia njiani wakati akipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Rungwe kwa matibabu,” alisema Kamanda Msangi.
Kamanda Msangi alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na dereva kutokuwa makini katika uendeshaji wake. Taarifa zilizotufikia baadae, zilieleza kuwa abiria mwingine aliyekuwa akipatiwa matibabu, alifariki akiwa hospitalini.

Mashuhuda wa ajali hiyo walidai kuwa chanzo cha ajali ni mwendokasi uliosababisha dereva ashindwe kumudu gari hilo katika mteremko wenye kona, akajikuta gari likimshinda na kutumbukia katika Mto Kiwira.
Walidai kuna uwezekano dereva huyo alikuwa akikimbizwa na baadhi ya madereva wa mabasi aina ya Toyota Coaster, yanayofanya safari zake kati ya Mbeya, Tukuyu na Kyela.

0 Responses to “ AJALI TATU VIFO 40 NDANI YA SIKU SITA.”

Post a Comment

More to Read