Thursday, April 2, 2015
HOTUBA YA WAZIRI MKUU PINDA WAKATI AKIHARISHA MKUTANO WA BUNGE,DODOMA
Do you like this story?
HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA 19 WA
BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 01 APRILI, 2015
I: UTANGULIZI
(a)
Masuala ya jumla
Mheshimiwa Spika,
1.
Leo
tunahitimisha shughuli zilizopangwa za Mkutano wa 19 wa Bunge lako Tukufu. Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye
wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo.
Mheshimiwa Spika,
2.
Tarehe 17
Machi, 2015 wakati tunaanza Mkutano huu, ulitoa taarifa ya kusikitisha ya
kumpoteza Mbunge mwenzetu Mheshimiwa Hayati
Kapteni John Damian Komba, Mbunge wa Mbinga Mashariki aliyefariki tarehe 28
Februari, 2015 na kuzikwa nyumbani kwake Lituhi tarehe 03 Machi, 2015. Napenda nitumie fursa hii kuungana na Waheshimiwa
Wabunge wote kutoa pole kwako, Wananchi wa Mbinga Mashariki na kwa Watanzania
wote kwa kuondokewa na ndugu yetu mpendwa Hayati
John Damian Komba. Kwetu sisi
tulioko ndani ya Bunge lako Tukufu hakuna asiyejua sifa za Mheshimiwa Hayati Kapteni
John Komba. Sote tutaendelea kumkumbuka
kwa yale yote aliyoyafanya kwa faida na maendeleo ya Nchi yetu.
Mheshimiwa Spika,
3.
Vilevile
katika kipindi hiki tangu Mkutano wa mwisho kulitokea majanga na ajali mbaya za
Barabarani ambazo watu wengi wamepoteza maisha.
Nitumie nafasi hii ya awali kabisa kuwapa pole ndugu, jamaa na marafiki
ambao wote wameguswa na misiba hiyo.
Tuwaombee kwa Mwenyezi Mungu roho za Marehemu zilale mahala pema peponi.
Kwa wale waliopata majeraha, tunawaombea wapone haraka.
Mheshimiwa Spika,
4.
Nitumie pia
fursa hii ya mwanzo kuwapongeza Mheshimiwa Dkt.
Grace Khwaya Puja na Mheshimiwa Innocent Rwabushaija Sebba kwa
kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Uteuzi wao unaonesha imani
kubwa aliyonayo Mheshimiwa Rais katika utendaji wao. Pamoja na kuwakaribisha Bungeni, tunawaahidi
ushirikiano wetu katika kutekeleza majukumu yao.
b) Maswali
Mheshimiwa Spika,
5.
Katika
Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kuuliza
maswali ya kawaida na jumla 156 ya
msingi na 425 ya nyongeza na
kujibiwa na Serikali.
(c) Miswada
Mheshimiwa Spika,
6.
Katika Mkutano huu, jumla ya Miswada 21 ilipangwa kujadiliwa katika Mkutano
wa 19. Miswada iliyowasilishwa na kupitishwa katika
hatua zote ni 14 ambayo ni kama ifuatavyo:
i)
Muswada wa
Sheria ya Udhibiti wa Ajira za Wageni wa mwaka 2014 (The Non-Citizens Employement Regulation Bill, 2014);
ii)
Muswada wa
Sheria ya Kudhibiti Silaha wa Mwaka 2014 (The
Firearms and Ammunition Control Bill, 2014);
iii)
Muswada wa
Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Uhamiaji wa Mwaka 2014 [The Immigration (Amendment) Bill, 2014];
iv)
Muswada wa
Sheria ya Usimamizi wa Kodi wa Mwaka 2014 (The
Tax Aministration Bill, 2014);
v)
Muswada wa
Sheria ya Takwimu wa Mwaka 2014 (The
Statistics Bill, 2014);
vi)
Muswada wa
Sheria ya Usimamizi wa Maafa wa Mwaka 2014 [The
Disaster Management Bill, 2014];
vii)
Muswada wa
Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Stakabadhi Ghalani wa Mwaka 2014 [The Wharehouse Receipts (Amendment)
Bill, 2014];
viii)
Muswada wa
Sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa wa Mwaka 2015 (The National Payment Systems Bill, 2015);
ix)
Muswada wa
Sheria ya Udhibiti na Usimamizi wa Dawa za Kulevya wa Mwaka 2014 [The Drug Control and Enforcement Bill, 2014];
x)
Muswada wa
Sheria ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI wa Mwaka 2014 [The Tanzania Commision for AIDS (Amendment) Bill, 2014];
xi)
Muswada wa
Sheria ya Bajeti ya Mwaka 2014 (The
Budget Bill, 2014);
xii)
Muswada wa
Sheria ya Baraza la Vijana Tanzania wa Mwaka 2015 [The Youth Council of Tanzania Bill, 2015];
xiii)
Muswada wa
Sheria ya Miamala ya Kielektroniki wa Mwaka 2014 (The Electronic Transaction Bill, 2015); na
xiv)
Muswada wa
Sheria ya Makosa ya Mtandao wa Mwaka 2015 (The
Computer and Cyber Crimes Bill, 2015).
Mheshimiwa Spika,
7.
Miswada iliyoachwa
kwa sababu mbalimbali ni:
xv)
Muswada wa
Sheria ya Wataalam wa Kemia wa Mwaka 2014 (The
Chemist Professionals Bill, 2014);
xvi)
Muswada wa
Sheria ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2014 (The Government Chemistry Laboratory Bill,
2014); na
xvii) Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali
(Na. 2) wa Mwaka 2014 [The Written Laws
(Miscellaneous Amendements) (No. 2) Bill 2014].
Mheshimiwa Spika,
8.
Miswada
ifuatavyo ilisomwa kwa mara ya Kwanza.
xviii)
Muswada wa
Sheria ya kupata Habari wa Mwaka 2015 (The
Access to Information Bill, 2015);
xix) Muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari wa Mwaka 2015 (The Media Services Bill, 2015);
xx)
Muswada wa
Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ushindani wa Mwaka 2015 [The Fair Competition (Amendment) Bill, 2015];
na
xxi)
Muswada wa
Sheria ya Tume ya Walimu wa Mwaka 2015 [The
Teachers Servce Commission Bill, 2015].
d) Maazimio
Mheshimiwa Spika,
9.
Katika
Mkutano huu, pia Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kujadili na kuridhia
Maazimio mawili yafuatavyo:
i)
Azimio la
kuridhia Mkataba wa Msingi na Kanuni za Utumishi wa Umma na Utawala Barani
Afrika Mwaka 2011 (The African Charter
and Principal of Public Service and Administration, 2011); na
ii)
Azimio la
Kuridhia Makubaliano ya Msingi ya Ushirikiano katika Bonde la Mto Nile (Agreement on the Nile River Basin Co-operative
Framework – CFA);
10.
Napenda
kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa kazi kubwa iliyofanyika ya kujadili
miswada mingi kiasi hiki na kuipitisha pamoja na kuridhia maazimio yote
yaliyowasilishwa.
II: MAAFA
YALIYOJITOKEZA
a)
Dhoruba ya Mtwara
Mheshimiwa Spika,
11.
Usiku wa kuamkia tarehe 14 Januari 2015 kulitokea
mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali katika eneo la Mnazi Bay, Mtwara; hali
ambayo ilisababisha eneo la Nchi kavu takribani mita 105 upana na mita 1,100 urefu kumeguka na kuwa sehemu ya
maji ya bahari. Eneo hili limejengwa miundombinu ya gesi asilia kama
ifuatavyo:-
i)
Kiwanda cha
kuchakata gesi asilia cha Maurel &
Prom Tanzania (M&P) kinachozalisha gesi ambayo inatumika kuzalishia
umeme kwenye mitambo ya TANESCO iliyopo Mtwara Mjini. Umeme unaozalishwa
unatumika kwa Mikoa ya Mtwara na Lindi; na
ii)
Bomba la gesi la inchi 16 litakalopeleka gesi asilia isiyosafishwa (raw gas) kutoka visima vilivyopo Mnazi Bay kwenda kiwanda kipya cha
Serikali cha kuchakata gesi asilia kinachojengwa Kijiji cha Madimba.
Mheshimiwa Spika,
12.
Hali hii
ilihatarisha zaidi kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Maurel & Prom
Tanzania (M&P) na kwa
kiasi kikubwa bomba la gesi asilia kama ilivyoelezwa hapo awali. Kiasi kikubwa cha
eneo la Nchi kavu kilimezwa na bahari na kuacha mita 6 tu kulifikia bomba la gesi asilia linalopeleka gesi kiwanda cha
Madimba na mita 29 kukifikia kiwanda
cha kuchakata gesi asilia cha M&P.
13.
Kufuatia hali hii, kikao cha Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Mkoa (KUU) ambacho pia kiliwashirikisha Wataalam wa Mamlaka ya Hali
ya Hewa, JWTZ, TPDC, TANESCO na Kamishna wa Madini wa Kanda kilifanyika tarehe
16 Januari, 2015 kujadili namna ya kukabiliana na tatizo lililojitokeza la
mmomonyoko mkubwa wa udongo uliotokea katika eneo la Mnazibay.
Mheshimiwa Spika,
14.
Kikao cha
Kamati ya Ulinzi kiliazimia kazi ya kuzuia mmomonyoko ianze kufanyika mara moja
alfajiri ya tarehe 17 Januari 2015 kwa kutumia Majeshi yote yaliyopo Mkoani kwa
kushirikiana na Uongozi wa Mkoa. Aidha, Kampuni ya Dangote, TPDC, walishirikiana
na majeshi yetu ya JWTZ, Magereza, Jeshi la Polisi walianza kuimarisha kingo
kwa kutumia viroba vilivyojazwa mchanga, mawe na vifusi vya zege.
Mheshimiwa Spika,
15.
Nachukua
fursa hii kuwapongeza uongozi wa Mkoa wa Mtwara kwa jitihada mlizofanya za
kusimamia zoezi zima la kuzuia mmonyoko wa ardhi katika kingo za bahari, eneo
la Mnazi Bay. Nitakuwa sijatenda haki kama nisipowataja wote
walioshiriki katika shughuli hii ya dharura. Makundi ambayo yamekuwa mstari wa mbele
kushirikiana kukabiliana na janga hilo ni pamoja na Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ), Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza. Wengine ni Kampuni ya Dangote,
Kampuni ya Maurel & Prom Tanzania, Kampuni ya Shideshi Co. Ltd, Shirika la
Petroli Tanzania (TPDC), Wizara ya Nishati na Madini na Wataalam kutoka Mamlaka
ya Hali ya Hewa Tanzania. Aidha, Wakala wa barabara (TANROAD)
Mtwara kwa kushirikiana na Mkandarasi “BQ
Contractors” walitoa vifaa vya uchimbaji wa mawe na kupakia kwenye magari.
Mheshimiwa Spika,
16.
Tayari Wizara ya Nishati imepeleka Wataalam
kufanya tathmini ya kina kujua athari zilizopatikana na jinsi ya kutunza eneo
hilo. Jeshi letu kwa kushirikiana na
Wadau mbalimbali wanaendelea kuimarisha kingo za bahari ili zisilete athari kwa
Kiwanda na Bomba la Gesi Asilia.
17.
Kazi
nzuri iliyofanyika imewezesha kudhibiti kasi ya maji kuendelea kumega sehemu ya
ardhi iliyobaki. Hali halisi iliyopo sasa baada ya jitihada zilizofanywa
kukabiliana na janga hilo, ni kwamba Kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha
Mnazi Bay kinachoendeshwa na Kampuni ya Maurel & Prom, kinaendelea
kuzalisha gesi na Mikoa ya Lindi na Mtwara inaendelea kupata umeme.
b)
Mafuriko
(i)
Wilaya ya Kahama – Mkoa wa Shinyanga
Mheshimiwa Spika,
18.
Usiku wa
kuamkia tarehe 4 Machi, 2015 mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo mkali
ilinyesha katika Vijiji vitatu vya Mwakata, Nhumbi na Maguhung’hwa vya Kata ya
Mwakata, Wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga.
Taarifa zilizotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa zinaonesha kuwa mvua hiyo
ilisababisha vifo 47, majeruhi 112 na nyumba 657 ziliathirika. Ekari 2,393
za mazao ya chakula ziliharibika. Aidha, mifugo mingi ilikufa wakiwemo ng’ombe 35, mbuzi 240, kondoo 50, kuku 1,034 na bata 240. Mifugo hii ilikufa kwa
kupigwa na mawe makubwa ya barafu na kisha kuangukia kwenye maji ya baridi
kali. Vifo hivyo, vya mifugo vimeleta athari kubwa hasa kwa kaya duni ambazo
mifugo ilikuwa ni tegemeo kwa mahitaji muhimu ikiwemo ada za Shule na shughuli
nyingi za kijamii. Vilevile, kulitokea
uharibifu mkubwa wa miundombinu na huduma muhimu za kijamii, kama vile Shule
kufungwa na kukosekana kwa maji safi na salama.
Mheshimiwa Spika,
19.
Tarehe 5
Machi, 2015 niliweza kutembela baadhi ya maeneo yaliyoathirika na mvua hizo
ikiwa ni pamoja na kuwapa pole waliopoteza ndugu na vifaa mbalimbali kama
nyumba na mifugo. Aidha, tarehe 12 Machi, 2015 Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naye alifanya ziara maalum ya
kutembelea Vijiji vitatu katika Kata ya Mwakata, Wilayani Kahama, Shinyanga ili
kuwapa pole na kuwafariji Wananchi walioathirika na mvua kubwa iliyonyesha
ikiambatana na upepo mkali na mawe.
Tayari Serikali imechukua hatua za dharura kuhakikisha kwamba waathirika
wote wanapatiwa msaada wa haraka ikiwemo vyakula, mahema, mablanketi na dawa za
kuwasaidia. Aidha, wakati nikiwa Shinyanga niliwaomba Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa
Wilaya kuhakikisha kuwa hali ya kawaida inarejeshwa katika maeneo yote
yaliyoathirika.
(i)
Wilaya ya Ilala – Mkoa wa Dar es Salaam
Mheshimiwa Spika,
20.
Wakati huo
huo mvua kubwa zilizonyesha katika Mkoa wa Dar es Salaam kuanzia tarehe 20
Machi, 2015 nazo zimesababisha mafuriko na uharibifu mkubwa wa miundombinu
katika sehemu za Jiji la Dar es Salaam.
Kutokana na mvua hizo Watu 7
walipoteza maisha na wengi kukosa makazi baada ya nyumba zaidi ya 200 eneo la Buguruni kwa Mnyamani
kuzingirwa na maji. Serikali itahakikisha inachukua hatua za kujenga mtaro wa
kutoa maji katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika,
21.
Jitihada za
kukabiliana na maafa hayo zimekuwa na mafanikio makubwa. Kwa vile majanga haya ni makubwa, ni dhahiri
kwamba Serikali peke yake isingeweza kubeba jukumu la kuwasaidia wote
walioathirika na mvua hiyo Watu binafsi, Wafanyabiashara, Mashirika ya Umma na
Yasiyo ya Kiserikali, Taasisi za Dini na Viongozi mbalimbali wameitikia wito wa
kushirikiana na Serikali kusaidia ndugu na jamaa walioathirika na maafa
hayo. Napenda nitumie fursa hii
kuwashukuru wote waliojitolea kwa hali na mali na moyo msaada ambao ulihitajika
sana katika kipindi hiki kigumu. Wito wangu kwa Wananchi wote ni kuwaomba tena kuendelea
kushirikiana kama ishara ya mshikamano kila wakati maafa yanapotokea.
c)
Ajali za Barabarani
Mheshimiwa Spika,
22.
Katika siku
za hivi karibuni, tumeshuhudia ajali za barabarani zikiendelea kupoteza maisha
ya wananchi sambamba na kuwafanya wengi kujeruhiwa na wengine kupata ulemavu wa
kudumu. Katika kipindi cha Januari hadi
Desemba, 2014 kulikuwa na jumla ya matukio 15,420
ya ajali za barabarani ambayo kati ya matukio hayo, ajali 3,106 zilisababisha vifo 3,857.
Aidha, ajali hizo zilisababisha majeruhi 15,230.
Mheshimiwa Spika,
23.
Kwa kipindi
cha Mwezi Januari hadi Februari, 2015 kulikuwa na jumla ya ajali 1,464 zilizosababisha vifo 509 na majeruhi 1,602. Moja ya ajali za kutisha za hivi karibuni ni ile iliyotokea
tarehe 11 Machi, 2015 katika mlima wa Changalawe, Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa
Iringa ambapo Basi la Kampuni ya Majinja Special
toka Mbeya kuelekea Dar es Salaam liligongana uso kwa uso na gari kubwa na
kusababisha vifo vya watu 50 kati
yao Wanawake 13 na Wanaume 37. Katika ajali hiyo, watu 21 walijeruhiwa.
Mheshimiwa Spika,
24.
Mnamo
tarehe 17 Machi, 2015 ajali nyingine ilitokea katika eneo la Hifadhi ya Taifa
ya Mikumi ambapo magari matatu yaligongana na kusababisha vifo vya watu wawili (2) na majeruhi wanne (4). Siku mbili baadaye tarehe 19
Machi, 2015 katika eneo hilohilo la Hifadhi Mikumi Morogoro Mini Bus ya Kampuni
ya Msanga, iligongana uso kwa uso na Basi la Kampuni ya Luwinzo na kusababisha
vifo vya watu 7 na majeruhi 17.
Mheshimiwa Spika,
25.
Wakati huo
huo, tarehe 23 Machi 2015 ajali nyingine ilitokea eneo la Majimazuri Mbeya ambapo Watu 8 walipoteza maisha na wengine
6 kujeruhiwa. Aidha, ajali nyingine ni ile iliyotokea
tarehe 25 Machi 2015, iliyohusisha Basi la Kampuni ya Super Shem liligongana
uso kwa uso na gari la Halmashauri ya Wilaya ya Nzega na kusababisha vifo vya
Watu 6 na wengine 9 kujeruhiwa. Ajali hiyo ilitokea katika barabara ya Mwanza
– Dar es Salaam eneo la Kijiji cha Undomo, Kata ya Uchama, Wilayani Nzega
Mkoani Tabora.
Mheshimiwa Spika,
26.
Kwa maana
hiyo, kati ya Januari na Machi, 2015 jumla ya Watu 73 walipoteza maisha na wengine 57 Walijeruhiwa. Sababu kuu
ya kutokea kwa ajali hizo inatajwa kuwa ni mwendo
kasi na uzembe wa madereva. Ni dhahiri kwamba, Matukio haya ya ajali
hayavumiliki na hayazoeleki. Aidha, hii ni idadi kubwa ya ajali na vifo
vilivyotokea katika kipindi cha muda mfupi.
27.
Nitumie
fursa kuziagiza Wizara ya Mambo Ndani ya Nchi, Wizara ya Uchukuzi Wizara ya
Fedha Wizara ya Katiba na Sheria, Taasisi za Usafiri kama SUMATRA katika
kipindi cha Mwezi mmoja kutoa mapendekezo kuhusu hatua za
dharura za namna ya kukabiliana na ajali hizi.
Vilevile, pale itakapobidi, Wataalam waangalie uzoefu wa Nchi nyingine
kujua hatua walizotumia katika kukabiliana na ajali.
28.
Serikali kwa
kushirikiana na Mamlaka zinazohusika na Uchukuzi na Usafirishaji zitaendelea
kuchukua hatua za makusudi kukabiliana na ajali hizo ikiwemo kuyafungia Makampuni
ya Usafirishaji yaliyokithiri katika matukio ya ajali. Pia, Madereva Wazembe
wataendelea kuadhibiwa kwa Mujibu wa Sheria na ikibidi kufutiwa Leseni zao za
Udereva. Nirudie kuagiza Jeshi letu la Polisi kuongeza juhudi katika kuzuia
ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikipoteza maisha ya Watu wengi na
kusababisha ulemavu na upotevu wa mali.
III. KILIMO
(a)
Hali ya
Chakula
Mheshimiwa Spika,
29.
Hali ya
chakula hapa Nchini kwa mwaka 2014/15 imeendelea kuwa imara kutokana na mavuno
mazuri na ya ziada yaliyopatikana msimu wa kilimo wa 2013/14. Tathmini ya
uzalishaji iliyofanyika mwaka jana, ilibainisha Nchi kuwa na ziada ya chakula
kwa viwango vya utoshelevu vya Asilimia 125. Mikoa 23 kati ya 25 ya Tanzania
Bara ilibainika kuwa na viwango vya ama ziada au utoshelevu. Katika kipindi hicho ni mikoa miwili tu
iliyodhihirika kuwa na uhaba wa chakula na maeneo tete katika Halmashauri 41.
b)
Mwenendo wa
Bei
Mheshimiwa Spika,
30.
Kwa ujumla
hali ya chakula na upatikanaji wa vyakula sokoni unaridhisha katika Mikoa yote
kufuatia mavuno mazuri ya msimu wa kilimo 2013/2014. Bei ya mazao ya chakula
imekuwa ikishuka au kupanda katika eneo moja na jingine. Kwa mfano, bei ya
wastani ya mahindi Kitaifa imeshuka kutoka Shilingi
41,313 mwezi Agosti, 2014 hadi Shilingi 37,355 mwishoni mwa mwezi
Februari, 2015 kwa gunia la kilo 100.
31.
Aidha,
katika kipindi hicho, bei ya mchele imepanda kutoka Shilingi 116,960 hadi Shilingi
150,563; na maharage kutoka Shilingi
139,452 hadi Shilingi 149,777 kwa gunia la kilo 100. Bei hizo ziko chini kuliko
ilivyokuwa kwa kipindi kama hicho mwaka jana na kwa wastani wa miaka mitano
iliyopita. Hata hivyo, hadi mwishoni mwa mwezi Februari 2015, bei ya mahindi
katika baadhi ya masoko ya Miji Mikuu hapa Nchini ilikuwa juu ikilinganishwa na
wastani ya Shilingi 37,355 kwa gunia
la kilo 100. Masoko hayo ni pamoja na Lindi (Shilingi 57,917), Musoma (Shilingi 49,375),
Kigoma (Shilingi 41,625) na Tanga
(Shilingi 37,375).
c) Mwenendo
wa mvua za vuli na upatikanaji wa chakula
Mheshimiwa Spika,
32.
Katika
msimu wa 2014/2015, maeneo yanayopata mvua za vuli hasa maeneo mengi ya Nyanda
za Juu Kaskazini (Arusha, Kilimanjaro, Tanga) yalipata mvua za wastani
zilizoanza Mwezi Septemba, 2014; na maeneo machache ya Kanda ya Ziwa (Kagera na
Mwanza) zilipata pia mvua za wastani. Hali hiyo, imefanya uzalishaji katika
maeneo hayo kutoridhisha hali inayoashiria kupungua kwa mchango wa mvua za vuli
(ambao ni takriban asilimia 27) ya
chakula msimu huu.
d)
Hali ya mazao mashambani
Mheshimiwa Spika,
33.
Tathmini
iliyofanyika tarehe 3 Machi, 2015, inaonesha kuwa mvua za msimu zilianza vibaya
katika Mikoa 11 ya Dar es Salaam, Mara, Morogoro, Pwani, Shinyanga, Tanga,
Lindi, Mbeya, Njombe, Rukwa na Tabora; na kwamba mtawanyiko wa mvua hizi
uliendelea vibaya katika Mikoa tisa (9) ya Arusha, Dar es Salaam, Pwani,
Shinyanga, Simiyu, Tanga, Manyara, Singida; na Tabora. Kutokana na hali hii,
inatarajiwa kuwa mavuno ya msimu wa 2014/2015 yatakuwa chini ya kiwango hivyo
kusababisha kuwepo kwa uhaba wa chakula katika Mikoa sita (6) ya Arusha,
Kilimanjaro, Mara, Pwani, Shinyanga na Tabora.
Mheshimiwa Spika,
34.
Tathmini
hii imeonesha pia kuwa utekelezaji wa malengo ya uzalishaji katika msimu wa
2014/2015 haujafikiwa katika Mikoa 18. Kwa Mikoa inayopata mvua mbili za vuli
na masika (Bimodal rain), nimeeleza kuwa kilimo cha vuli kilishapita bila
mchango mkubwa wa chakula; na kwa vile mvua za masika zitategemewa kunyesha kwa
mtawanyiko wa wastani na kwa kipindi kifupi, ni wazi kuwa uzalishaji utakuwa
pungufu ikilinganishwa na uzalishaji wa mwaka 2013/2014 na hivyo kufanya
upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2015/2016 kuwa chini ikilinganishwa na mwaka
uliopita.
Mheshimiwa Spika,
35.
Kutokana na
uwezekano wa kuwepo kwa upungufu wa chakula katika msimu wa 2015/2016 katika Nchi
yetu, napenda kuchukua fursa hii kuwataka Wakuu wa Mikoa iliyopata mvua hafifu;
na ile yenye akiba kubwa ya chakula wasimamie kwa karibu shughuli za hifadhi ya
mavuno yaliyopatikana katika msimu wa 2013/2014 kwa kuzishirikisha Halmashauri
zote na wananchi. Vile vile, kwa Mikoa yenye mvua chache wachukue hatua
madhubuti na za haraka kwa kushirikiana na Halmashauri zote kuhakikisha kuwa
wananchi wanapata mbegu bora za muda mfupi zinazostahimili ukame kama vile
mtama, uwele, n.k. ili wapande mapema kwa kutumia mvua zinazonyesha sasa.
e)
Hifadhi ya Taifa ya Chakula
Mheshimiwa Spika,
36.
Hadi tarehe
11 Machi 2015 Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA)
ulikuwa umenunua Tani 304,514 za
nafaka ziwemo Tani 295,900 za
mahindi, Tani 4,674 za mtama; na Tani
3,940 za mpunga. Kutokana na NFRA
kuwa na akiba ya Tani 188,987 za
mahindi na Tani 506 za mtama wakati
wa kuanza msimu wa ununuzi tarehe 01 Julai, 2014 hadi sasa akiba iliyohifadhiwa katika Kanda mbalimbali
za NFRA ni jumla ya Tani 494,007 ambapo
Tani
484,887 ni za mahindi, Tani 5,180
ni za mtama; na Tani 3,940 ni za mpunga. Tunafahamu kuwa
kuna maeneo kadhaa hapa Nchini yaliyopata mavuno hafifu kutokana na maeneo yao
kukosa mvua ya kutosha. Hivyo, napenda kuliarifu Bunge lako tukufu na wananchi
kuwa Serikali ina akiba ya kutosha ya chakula kwa Wananchi wote watakaokuwa na
matatizo ya njaa. Nichukue fursa hii kuitaka Mikoa na Halmashauri zenye
upungufu wa chakula kufanya tathmini ya haraka kupata takwimu za wananchi wenye
njaa ili wapatiwe chakula mapema bila kuchelewa.
f) Mwenendo wa Malipo ya NFRA
Mheshimiwa Spika,
37. Katika
mwaka wa fedha 2014/2015 Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula
ulipanga kununua Tani 200,000 za nafaka
kwa gharama ya Shilingi Bilioni 109.6.
Hata hivyo kutokana Wananchi kuzalisha kwa wingi na kuiwezesha Nchi kuwa na
ziada ya chakula hasa mahindi, mpunga na mtama kwa takriban Tani Milioni 3.2, Serikali iliongeza lengo la
ununuzi wa nafaka hadi Tani 298,122. kwa
thamani ya Shilingi Bilioni 151.3. Serikali ilichukua hatua hiyo ili kuepuka
kuharibika kwa mazao yaliyokuwa yameletwa na wakulima kuuzwa katika vituo vya
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Aidha, kutokana na fedha za Tani za
ziada kutokuwepo katika Bajeti ya awali, Serikali ilishindwa kuwalipa kwa
wakati wakulima wote waliopeleka nafaka katika vituo hivyo na kusababisha
Serikali kuwa na madeni kwa wakulima hao.
Mheshimiwa
Spika,
38. Hadi
tulipofika Januari 2015, deni lilikuwa limefikia Shilingi Bilioni 89.2 kwa Tani 175,606 za nafaka. Kwa msingi huo hadi tarehe 24 Februari 2015,
Serikali ilikuwa imetoa Shilingi Bilioni 15
na kukopa Shilingi Bilioni 15 kutoka
Benki ya CRDB zilizolipa na kupunguza
madeni ya wakulima. Takwimu za sasa zinaonesha kuwa hadi tarehe 27 Machi, 2015
deni lilikuwa limepungua hadi kufikia Shilingi Bilioni 45 kwa Tani 88,910
za nafaka.
Mheshimiwa Spika,
39. Katika kuendelea
kupunguza malipo ya deni lililobaki, tarehe 31 Machi, 2015 Serikali imetoa
Shilingi Bilioni 20 na kubakiza deni
la Shilingi Bilioni 25. Aidha,
Serikali imepanga kuuza sehemu ya akiba ya nafaka iliyopo katika Wakala wa
Taifa wa Hifadhi ya Chakula kwa Mpango wa Chakula Duniani (World Food Programme) na Jeshi la Magereza ili kupata fedha
zakulipia deni lote lililobaki. Napenda kutoa msisitizo kwa Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Chakula (NFRA) katika kufanya malipo haya kuzingatie maagizo ya
Serikali ya kutoa kipaumbele cha kufanya malipo kwa wakulima wadogo wadogo,
mmoja mmoja kabla ya makundi mengine.
IV: UNUNUZI WA MADAWATI SHULE
ZA MSINGI KWA KUTUMIA FEDHA YA FIDIA YA RADA
Mheshimiwa Spika,
40. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipokea fedha zilizotokana
na fidia ya Rada (BAE System Plc Funds)
kiasi cha Paundi za Uingereza 29,542,266, sawa na Shilingi 72,324,609,162. Kulingana na
Mkataba wa Makubaliano (MOU) kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Serikali ya Uingereza kupitia Shirika la Maendeleo - DFID,
ilikubaliwa kuwa Paundi 24,392,266
sawa na Shilingi 59,716,513,062
zitumike katika ununuzi wa vitabu vya kiada, mihutasari na miongozo ya
mihutasari kwa shule za msingi Tanzania Bara; Paundi 5,000,000 sawa na Shilingi 12,240,870,000
zitumike kununulia madawati kwa shule za msingi Tanzania Bara. Aidha, Paundi za
Uingereza 150,000.00 sawa na Shilingi
367,226,100.00 zilipangiwa kazi ya
ukaguzi na ufuatiliaji na udhibiti wa mchakato wa ununuzi.
Mheshimiwa Spika,
41. Kutokana na Mkataba wa Makubaliano hayo ilipangwa kuwa madawati
yanunuliwe kwa ajili ya Halmashauri tisa (9) zenye upungufu mkubwa wa madawati
na matokeo dhaifu katika mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi. Lengo lilikuwa ni
kumaliza uhaba wa madawati katika Halmashauri hizo. Hata hivyo, Bunge katika
kikao chake cha mwaka 2012/2013 ilishauri kwamba Halmashauri zote zipate mgao
wa madawati kwa usawa. Hivyo, Mikoa yote ishirini na tano ya Tanzania Bara
imepata na itaendelea kupata madawati kwa usawa.
Mheshimiwa
Spika,
42. Kikao cha Kamati Tendaji ya matumizi ya fedha za BAE kiliamua kuwa
yatengenezwe madawati ya kukaa mwanafunzi mmoja mmoja ili kukidhi na
kurahisisha ufundishaji kwa kutumia njia shirikishi ambazo huwezesha wanafunzi
kujadiliana zaidi na kuchangiana mawazo ya uelewa wao kuliko kumsikiliza
mwalimu zaidi. Hivyo madawati yatengenezwe na kugawiwa kwa kuzingatia aina za
madawati na umri wa Wanafunzi. Wataalamu wa Ufundi kutoka Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi (WEMU) wakishirikiana na Wataalamu wa Ufundi kutoka DFID
walitoa viwango vya ulinganisho (technical
specifications) vya madawati hayo.
Mheshimiwa Spika,
43. Katika kugawa madawati, Mikoa sita ya ukanda wa Pwani ilipangwa kupata
madawati ya Plastiki Ngumu (Hard Plastic
Desks). Mikoa hiyo ni Dar es salaam, Pwani, Tanga, Lindi, Mtwara na
Morogoro. Mikoa kumi na tisa iliyobaki itapatiwa madawati ya mbao (Steel Framed Desk).
Mheshimiwa Spika,
44. Awamu ya kwanza ya ununuzi wa madawati ilianza mwezi Oktoba 2013 na
ilihusisha ununuzi wa aina mbili za madawati, madawati ya Plastiki Ngumu na
madawati ya Mbao.
Mheshimiwa Spika,
45. Jumla ya madawati 30,996 ya
Plastiki Ngumu (Hard Plastic Desks)
yamenunuliwa kwa ajili ya Mikoa sita ya Ukanda wa Pwani ambao una Halmashauri
41 ambapo kila Halmashauri imepata madawati 756 na usambazaji wake umekamilika na madawati yameanza kutumika.
Aidha, jumla ya madawati 62,992 ya
Mbao yamenunuliwa na usambazaji umekamilika ambapo kila Halmashauri kati ya 124
za Mikoa 19 isiyo ya Ukanda wa Pwani imepata madawati 508.
Mheshimiwa Spika,
46. Awamu ya pili ya ununuzi wa madawati ilianza mwezi Juni 2014. Awamu hii
imehusisha jumla ya madawati 74,897
ya Plastiki Ngumu na ya mbao. Kila Halmashauri ya Mikoa sita ya Ukanda wa Pwani
imepata madawati 617 ya Plastiki
Ngumu. Ilihali kila Halmashauri za Mikoa 19 isiyo ya Pwani itapata madawati 400 ya mbao. Inatarajiwa madawati haya
ya mbao yatakamilika kusambazwa katika Halmashauri kati kati ya mwezi wa Nne
2015.
Mheshimiwa Spika,
47. Madawati ambayo yameshasambazwa mpaka sasa ni 119,285 yakiwemo ya plastic ngumu 56,293. Madawati mengine ya mbao 49,600 yatakamilika kusambazwa kati kati ya mwezi April 2015.
Mchakato huu wa ununuzi wa madawati ukikamilika bado tatizo la upungufu wa
madawati litakuwa halijaisha. Kuna uhitaji wa madawati 3,302,678, na madawati yaliyopo shuleni ni 1,837,783 na kuna upungufu wa madawati 1,464,895. Baada ya kukamikisha usambazaji wa madawati 168,885 kwa kutumia fedha hizi za fidia
ya rada kutakuwa na upungufu wa madawati 1,296,010.
Hivyo, bado kuna ulazima wa kuendelea kutenga fedha zaidi katika kupunguza na
hatimaye kumaliza kabisa tatizo la upungufu wa madawati ili kuboresha mazingira
ya kujifunza na kujifunzia na kuendana na mahitaji ya Mpango wa Matokeo Makubwa
sasa (BRN).
Mheshimiwa Spika,
48. Nachukua fursa hii kuwashukuru sana wote walioshirikiana
katika harakati hizi za kuondoa upungufu wa madawati Nchini. Napenda kuwakumbusha Viongozi na Wananchi
kuwa bado tunayo kazi kubwa. Kila mmoja
awe mbunifu katika eneo lake na kushirikiana
pamoja katika kuweka na kutekeleza mipango endelevu ya kuongeza idiadi
ya madawati. Halmashauri ziendelee
kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya Madawati na nawaomba Wadau wa Maendeleo
kuendelea kusaidia katika eneo hili. Ninaamini wote tukishirikiana kwa pamoja tutafanikiwa.
V: MAUAJI YA WATU WENYE ULEMAVU WA NGOZI
(ALBINO)
Mheshimiwa Spika,
49.
Hivi karibuni yameibuka tena mauaji ya Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi
(Albino). Ninasema yameibuka tena kwa kuwa yalikuwa yamekoma hususani mwaka
2011 na tukaishi kwa amani kidogo. Hata hivyo, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akihutubia Taifa katika
hotuba yake ya mwisho wa mwezi Februari 2015 alilieleza Taifa kuwa mauaji hayo
yameibuka tena. Mauaji haya kwa taarifa zilizopo yalianza mwaka 2006 ambao
ulikuwa na tukio moja (1). Idadi ya
matukio ya mauaji iliendelea kupanda hadi kufikia saba (7) mwaka 2007 na 18
mwaka 2008. Mwaka 2009 matukio yalianza kupungua kutokana na juhudi za Serikali
na Wananchi. Mwaka huo ulikuwa na matukio Tisa
(9), mwaka 2010 ulikuwa na tukio moja
(1) na mwaka 2011 kama nilivyosema haukuwa na tukio. Hata hivyo, kwa miaka
iliyofuata kulikuwa na tukio moja (1)
mwaka 2012, tukio moja (1) mwaka
2013 na kufikia matukio manne (4) mwaka 2014. Mwaka huu wa 2015 limeshatokea
tukio moja (1) na kufanya jumla ya matukio ya mauaji kuwa 43 hadi sasa (Mwaka 2006 – 2015). Matukio haya hayahusishi yale ya
kujeruhi.
Mheshimiwa Spika,
50.
Kwa upande
wa Watuhumiwa takwimu za watuhumiwa kati ya mwaka 2006 -2015 zinaonesha kuwa:
i)
Jumla ya
watuhumiwa 181 wakiwemo Wanaume 171 na Wanawake 10 walikamatwa na kuhojiwa. Kati yao watuhumiwa 133 walifikishwa mahakamani na
kufunguliwa kesi za mauaji na 46 kwa makosa ya kujeruhi.
ii)
Kesi 10 bado zinaendelea katika hatua
mbalimbali za uchunguzi;
iii)
Watuhumiwa 15 wamehukumiwa katika Mahakama, 13 kati yao wamehukumiwa kunyongwa hadi
kufa.
iv)
Watuhumiwa
wawili waliuawa na Wananchi kabla ya kufikishwa Polisi.
v)
Mtuhumiwa
mmoja alihukumiwa kifungo cha miaka 20
jela kwa kosa la kujeruhi;
Mheshimiwa
Spika,
51.
Chanzo
kikubwa cha mauaji hayo ni imani za kishirikina. Aidha, Matukio
41 kati ya 43 yametokea katika
Ukanda wa Ziwa na Magharibi, kwani hadi sasa yametokea matukio 13 ya Mauaji Mwanza, Kagera matukio
sita (6), Tabora matukio matano (5), Mara matukio manne (4), Geita matukio
manne (4), Kigoma matukio Manne (4) Simiyu matukio matatu (3) na Shinyanga
matukio mawili (2). Hali hii inayoonesha
dalili kuwa imani hizi za kishirikina zimejikita zaidi katika eneo hili la
Nchi. Wakati akihutubia Taifa katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Februari
2015 Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ameweka wazi msimamo wa Serikali kwamba Serikali itafanya kila
jitihada kukomesha mauaji haya. Aidha, Serikali haitaacha hali iwe mbaya kama
ilivyokuwa huko nyuma.
Mheshimiwa
Spika,
52.
Wito
wangu ni kuomba ushirikiano wa Wananchi na Viongozi wa Dini zote, Mashirika ya
Serikali na Yasiyo ya Serikali na Wadau wote wa Maendeleo katika vita hii.
Aidha, niwaombe watu wote walio wazalendo na wenye kupenda amani katika Taifa
letu la Tanzania kuendelea kulaani kwa nguvu zote vitendo hivi vya kikatili na
visivyokubalika na kuendelea kutoa taarifa zozote zinazohusu vitendo hivi kwa
vyombo vya Serikali ili kusaidia kukomesha vitendo hivyo. Niwaombe tena Taasisi
zote za Dini kusaidia katika kuondoa au kubadili imani hizi za kishirikina
miongoni mwa jamii na Mahakama kusaidia katika kuharakisha kesi za mauaji ya
Walemavu wa Ngozi na kutoa adhabu kali kwa watakaothibitika kushiriki katika
vitendo hivyo. Vyombo vya Dola vitumie kila ujuzi na mbinu kutekeleza maelekezo
ya Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kukomesha
mauaji haya. Ninaamini tukiunganisha nguvu zetu kwa pamoja dhidi ya fedheha hii
tutashinda.
VI: KURA YA MAONI KUHUSU KATIBA INAYOPENDEKEZWA NA
UCHAGUZI MKUU
a)
Kuboresha Daftari la Wapiga Kura
Mheshimiwa
Spika,
53.
Zoezi la
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linaendelea katika Mkoa wa
Njombe chini ya Usimamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Sambamba na Uboreshaji wa Daftari la Wapiga
Kura, Tume inaendelea pia na maandalizi ya utekelezaji wa Upigaji Kura ya Maoni
na Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Jukumu
kuu la Tume kwa sasa ambalo limekwisha anza ni ukamilishaji wa Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura kwa haraka ili kuwezesha kufanyika kwa Kura ya Maoni kuhusu
Katiba Inayopendekezwa na baadaye Uchaguzi Mkuu. Uandikishaji unafanyika kwa
kutumia vifaa maalum vinavyojulikana kama “Biometric
Voters Registration (BVR)”. Vifaa hivi vina uwezo wa kumtambua mtu na kumtofautisha na mwingine kama vile
alama za vidole, sura, mpangilio wa mikono,
saini ya mtu n.k. Hivyo vifaa hivi vinatumika katika
Uandikishaji wa Daftari la kudumu ili kuwa na Daftari sahihi na linaloaminika
zaidi.
Mheshimiwa Spika,
54.
Katika
kutekeleza uboreshaji wa zoezi hili, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imelenga
kuandikisha Wapiga Kura milioni 21. Vituo vya Kuandikishwa vimesogezwa karibu
na Wapiga Kura katika ngazi za Vijiji, Vitongoji na Mitaa; na inakadiriwa
kutakuwa na Vituo 36,164. Kila Kituo kitaandikisha kwa siku 7 hadi 11 kufuatana
na idadi ya watu na vituo vitafunguliwa kuanzia saa 2 hadi saa 12 jioni.
Mheshimiwa Spika,
55.
Katika
zoezi zima la kuboresha Daftari la Wapiga kura Tume inategemea kutumia BVR Kits
8,000 katika uboreshaji huu. Tayari BVR 250 zilitumika katika zoezi la
majaribio kwa mafanikio makubwa. Uboreshaji wa awamu hii utahusisha Wapiga Kura
wote, wapya na wa zamani na wale wote waliozaliwa kabla ya Septemba 1997.
Aidha, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeanza Uandikishaji katika Mkoa wa Njombe
tarehe 16 Machi, 2015 na unatarajiwa kukamilika tarehe 18 Aprili 2015 ambao ni
takriban muda wa Mwezi mmoja.
56.
Tarehe 24
Februari, 2015 nilifanya uzinduzi Kitaifa wa Zoezi la Uandikishaji wa Wapiga
Kura katika Daftari la Wapiga Kura, hafla iliyofanyika Mjini Makambako katika
Mkoa wa Njombe. Taarifa tulizopata ni kwamba uandikishaji huo umekuwa wa
mafanikio makubwa; kwani watu wanajitokeza kwa wingi sana. Kwa mfano, katika
Halmashauri ya Mji wa Makambako, Tume ilipanga kuandikisha Wastani wa Wapiga
Kura 1,850 kwa siku ya kwanza lakini walioandikishwa 3,014 ambao ni mara 2 ya
waliotarajiwa.
Mheshimiwa
Spika,
57.
Serikali
kwa upande wake imehakikisha fedha yote kwa ajili ya ununuzi wa BVR 8,000
zimelipwa kwenye Tume ya Uchaguzi ya Taifa. Matarajio ni kwamba kazi ya kuandikisha
katika Mikoa mingine itaanza na kuendelea kwa kasi. Aidha, tunatarajia Tume itatoa taarifa ya Ratiba
itakayotumika kutuwezesha kukamilisha zoezi la uandikishaji. Tume itatoa
taarifa siku za hivi karibuni kuhusu upigaji wa Kura ya Maoni. Ni dhahiri muda uliobaki kuanzia sasa ni
mfupi lakini Tume ndiyo itakayotujulisha Ratiba kamili. Wakati Tume inajitahidi kufikia malengo hayo,
Serikali inaendelea na mipango ya kuelimisha Wananchi kupitia Raido,
Televisheni, Magazeti mbalimbali kuhusu umuhimu wa Katiba Inayopendekezwa ili
kila Mwananchi aielewe vizuri na kuweza kuipigia kura kwa matakwa yake mwenyewe
bila kurubuniwa muda utakapofika.
b)
Usambazaji wa Nakala za Katiba Inayopendekezwa na Hatua iliyofikiwa.
Mheshimiwa Spika,
58.
Wakati huo
huo zoezi la kusambaza Nakala za Katiba Inayopendekezwa linaendelea. Kama mtakumbuka Serikali ilipanga kuchapisha
nakala 2,000,000 za Katiba
Inayopendekezwa. Usambazaji wa nakala za Katiba hiyo kutoka Bohari kuu kwenda
Mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar kuanzia tarehe 3 Januari, 2015 hadi tarehe 18 Machi,
2015 ulifikia jumla ya nakala 1,716,010.
Katika Tanzania Zanzibar (Unguja na Pemba) nakala 210,000 zilisambazwa na katika Mikoa 25 ya Tanzania Bara
zilisambaziwa jumla ya nakala 1,141,300.
Nakala hizo zilisambazwa katika Kata zote 3,802
za Tanzania Bara ambapo kila Kata ilipata nakala 300. Viongozi wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri walisambaziwa nakala 40 kila Mkoa.
Mheshimiwa
Spika,
59.
Takwimu za ugawaji
wa nakala za Vitabu vya Katiba Inayopendekezwa katika Taasisi zinaonesha kuwa
jumla ya nakala 346,000 zilisambazwa
kwa Wizara na Taasisi mbalimbali Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Wizara zimepangiwa
kupata nakala 9,700, Taasisi za
Serikali za Tanzania Bara nakala 79,100,
Taasisi za Elimu ya Juu nakala 43,200
na Taasisi za Kidini zitapata nakala 24,000.
Asasi za Kiraia nakala 6,400, Vyama
vya Siasa nakala 170,100, na Taasisi
nyingine kama Tanzania Private Sector Foundation,
TUCTA Media Council of Tanzania na
Chama cha Walimu nakala 3700. Wizara na Taasisi za Zanzibar zimepangiwa nakala
10,000. Matumaini ni kwamba Nakala zote
zitakuwa zimesambazwa kwa wahusika. Wito
wangu ni kuwaomba Wananchi kuhakikisha wanapta nakala ya Katiba Inayopendekezwa
kuisoma vizuri na kuielewa na hatimaye kuipigia kura Katiba hiyo.
VIII: UFAFANUZI
KUHUSU MAHAKAMA YA KADHI
Mheshimiwa Spika,
60.
Katika
Mkutano wa 18 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ilikusudia
kuwasilisha Bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali [The Written
Laws(Miscellaneous Amendments) Act] Na. 2/2014. Sehemu ya Tano ya Muswada
huo ilikusudia kurekebisha Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislam [The Islamic Law (Restatement) Act], Sura ya 375. Hata hivyo, kama
nilivyoeleza hapo awali Muswada huu ni miongoni mwa Miswada mine (4) ambayo
haikupata nafasi ya kujadiliwa na Bunge. Serikali itatumia fursa kuendelea
kushirikisha Wadau mbalimbali kwa lengo la kupanua uelewa juu ya maudhui na
madhumuni ya Muswada huu.
IX: CHANGAMOTO
ZA WAFANYABIASHARA KUHUSU UTOZAJI KODI
Mheshimiwa Spika,
61.
Tarehe 27 Machi, 2015 Serikali ilikutana na Viongozi wa
Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina (Mb.)
ambaye aliongozana na Wafanyabiashara hao
baada ya Kamati yake kuwasikiliza na Mheshimiwa Deo Kasanyenda Sanga
(Mb.) ambaye ni Mjumbe wa Kamati hiyo. Lengo la Kikao hicho lilikuwa ni
kuzungumzia kuhusu kero na malalamiko mbalimbali ya Wafanyabiashara na
kuyatafutia ufumbuzi wa pamoja.
Mheshimiwa Spika,
62.
Katika Kikao hicho, Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara
Tanzania, Mchungaji Silver L. Kiondo alieleza kuwa, malalamiko yao ambayo
wanaomba Serikali iyashughulikie ni yafuatayo:
i)
Changamoto ya Kimfumo ya Matumizi ya Mashine za Kielektroniki za EFD;
ii)
Ongezeko la Makadirio ya Kodi ya Mapato kwa Asilimia 100 kwa
Wafanyabiashara ambao hawana kumbukumbu za biashara zao; na
iii) Maombi ya kuachiliwa
huru kwa Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Bwana Johnson
Estomihi Minja kutokana na kuondolewa kwa dhamana na Mahakama baada ya kesi
inayomkabili kutajwa tarehe 26 Machi, 2015.
Mheshimiwa Spika,
63.
Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa, katika jitihada za kuimarisha
ukusanyaji wa mapato Nchini; mwaka 2010 Serikali ilibuni Mfumo rahisi wa kulipa
Kodi unaoendana na mazingira ya sasa ya mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.
Mfumo huo wa Matumizi ya Mashine za Kielektroniki ulianzishwa kwa malengo ya kuboresha utunzaji wa kumbukumbu kwa
Wafanyabiashara; kuongeza uwazi
katika ukadiriaji wa Kodi; kupunguza mianya ya rushwa na kukuza ulipaji Kodi kwa hiari na hivyo
kupunguza malalamiko ya ulipaji Kodi yasiyo ya msingi.
64.
Aidha, Mfumo wa Matumizi ya Mashine za Kielektroniki za EFD;
unarahisisha usimamizi wa Kodi, kwani mauzo yote yanarekodiwa kwenye Mashine za
Kielektroniki na hatimaye kutumwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa njia ya
Mtandao wa moja kwa moja. Utumiaji ipasavyo wa Mashine za EFD huongeza ulipaji
Kodi kwa hiari na hivyo kuongeza Pato la Taifa.
Mheshimiwa
Spika,
65.
Naomba nitumie fursa hii kurejea kwa muhtasari manufaa ya Matumizi ya
Mashine za Kielektroniki (EFD) kwa Wafanyabiashara na Serikali. Kama
mnavyofahamu kutokana na maendeleo makubwa ya Sayansi na Teknolojia ya
Mawasiliano ya Kisasa (ICT); Wataalam wanathibitisha kwamba, Mashine za
Kielektroniki za EDF zinafanya kazi zifuatazo:
Moja: Zinatoa Risiti na Ankara za Kodi kwa urahisi na Mfanyabiashara
huondokana na adha ya kuchapisha au kununua vitabu vingi vya kuandikia risiti
ambavyo utunzaji wa nakala zake unaleta usumbufu;
Pili: Zina uwezo mkubwa wa kutunza kumbukumbu za mauzo, manunuzi na
mali ya biashara (stock) bila
kufutika kwa muda usiopungua miaka mitano;
Tatu: Mtumiaji anaweza kutoa kwa urahisi taarifa za mauzo yake kwa
siku, kwa wiki, kwa mwezi, kwa mwaka na kwa wakati wowote kwa kipindi
kisichopungua miaka mitano;
Nne: Humwezesha Mfanyabiashara kutuma taarifa zake za mauzo moja kwa
moja kwenda Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka nyingine zenye
mahitaji ya taarifa hizo, kama vile Taasisi ya Taifa ya Takwimu, Benki Kuu,
EWURA, na SUMATRA;
Tano: Mashine zinaweza kupokea maelekezo moja kwa moja kutoka kwenye Mfumo wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania, na kumtaarifu Mfanyabiashara taarifa yoyote ya Kodi
inayomhusu;
Sita: Mashine za Kielektroniki zinaweza kutuma na kupokea fedha kwa
njia ya “Mobile Money”. Utaratibu huu
unamwezesha Mtumiaji kutumia Mashine hizi kulipia kodi na huduma nyingine moja
kwa moja kama vile, Ankara za Umeme, Maji, Simu, n.k;
Nane: Mashine za Kielektroniki zinatumia lugha ya Kiswahili na
Kiingereza inayoeleweka kwa Wananchi wengi;
Tisa: Mashine za Kielektroniki zinaiwezesha Mamlaka ya Mapato
Tanzania kutambua mauzo sahihi ya Mfanyabishara na hivyo kuweza kutoza Kodi
halali.
Mheshimiwa
Spika,
66.
Utekelezaji wa Mfumo wa Matumizi ya Mashine za Kielektroniki
unatekelezwa kwa Awamu mbili. Utekelezaji wa Awamu ya Kwanza ulianza rasmi
mwezi Julai, 2010 ukihusisha Wafanyabiashara waliosajiliwa kukusanya Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) na Awamu ya Pili ilianza mwaka 2013 ikihusisha
Wafanyabiashara waliosajiliwa kutozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Mheshimiwa
Spika,
67.
Katika utekelezaji wa zoezi hili, Serikali imelenga kuingiza Walipa Kodi
wapatao 250,000 kati ya Walipa Kodi 1,500,000 ili waweze kutumia Mashine za
Kielektroniki za EFD. Walengwa wa utaratibu huu ni Wafanyabiashara wenye
biashara kubwa zenye Mtaji wa kati
ya Shilingi Milioni 14 na Shilingi Milioni 40. Katika Awamu hizi mbili,
Wafanyabiashara wanaoendesha biashara zisizo rasmi kama vile, Wamachinga na
wale wanaotembeza bidhaa barabarani na Mama Lishe hawahusiki na utaratibu huu.
Mheshimiwa
Spika,
68.
Napenda kusisitiza kuwa, Mfumo wa Matumizi ya Mashine za Kielektroniki
ni mzuri na unawasaidia Wafanyabiashara kutunza kumbukumbu na kulipa Kodi
stahiki. Nawasihi Wafanyabiashara wajenge tabia ya kutunza kumbukumbu za
biashara zao ili waweze kulipa Kodi Stahiki badala ya kutumia Mfumo wa
Makadirio ambao umepitwa na wakati. Serikali inaamini kuwa, Matumizi ya Mashine
za Kielektroniki zitaongeza Makusanyo ya Kodi na kupunguza vishawishi vya
Rushwa.
Mheshimiwa
Spika,
69.
Baada ya maelezo hayo, napenda kueleza hatua zilizochukuliwa na Serikali
kushughulikia Malalamiko ya Wafanyabiashara
pamoja na muhtasari wa makubaliano
baina ya Serikali na Wafanyabiashara katika maeneo yanayolalamikiwa kama
ifuatavyo:
Mheshimiwa
Spika,
70.
Serikali ilikwishaanza kushughulikia Malalamiko ya Jumuiya ya
Wafanyabiashara tangu mwezi Januari, 2014, hususan kuhusu kushughulikia
changamoto zinazotokana na Mfumo wa Mashine za Kielektroniki. Aidha, mwezi
Septemba, 2014 iliundwa Kamati ya Taifa ya Uhamasishaji wa Matumizi ya Mashine
za Kielektroniki za EFD na Kamati ya Ndogo ya Kiufundi ya kupitia mfumo wa
uongoshaji wa Mizigo Bandarini. Vilevile, Wizara ya Fedha imeunda Kamati za
Mikoa za kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili Wafanyabiashara ikiwa ni
pamoja na kuelimisha Umma kuhusu Matumizi ya Mashine za EFD. Kutokana na hatua
hizo kwa sasa mshine za kielektroniki za EFD zimeboreshwa zaidi na kuipa
Mamlaka ya Mapato Tanzania uwezo mkubwa wa kusimamia mauzo ya Wafanyabiashara.
Aidha, zoezi la elimu kwa walipa kodi
linaendelea katika Mikoa yote Nchini.
Mheshimiwa Spika,
71.
Katika Kikao cha tarehe 27 Machi, 2015 Serikali pamoja na Viongozi wa Jumuiya
ya Wafanyabiashara tuliafikiana kwamba:
(a) Kamati ya Kitaifa ya
Uhamasishaji wa Matumizi ya Mashine za Kielektroniki (EFD) au Kamati ya pamoja
ya maridhiano baina ya Wafanyabiashara na Serikail kuhusu matatizo ya kimfumo
ya utozaji kodi na yale yanayotokana na mfumo wa Mashine za Kielektroniki za
EFD; ikutane mapema iwezekanavyo kuanza majadiliano ili kuyapatia ufumbuzi
malalamiko, changamoto na kero zinazowakabili Wafanyabiashara na kuwasilisha
mapendekezo yake Serikalini ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuanzia tarehe 28
Machi 2015. Kamati husika ikamilishe kazi yake kabla ya mwisho wa mwezi Aprili,
2015;
(b) Ili kuwepo na
uwakilishi mpana kwenye Kamati ya Taifa ya pamoja ya Wafabiashara na TRA,
Serikali itateua Wajumbe wawili kutoka
Wizara ya Viwanda na Biashara na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge)
wawe sehemu ya Kamati iliyoundwa inayojumuisha Wajumbe Watatu (3) kutoka
Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania na Wajumbe Watatu (3) kutoka Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) pamoja na Mjumbe mmoja (1) kutoka Wizara ya Fedha;
(c) Kwa kuwa suala la
Ongezeko la Kodi ya Mapato la Asilimia 100 linatokana na Marekebisho ya Sheria
ya Fedha ya mwaka 2014/2015 ambayo imepitishwa na Bunge, na linawahusu wale tu
ambao hawatunzi kumbukumbu zozote za mauzo ya bidhaa zao. Hivyo, ufumbuzi wa suala hili unapaswa ufuate
utaratibu wa mchakato wa marekebisho ya Sheria husika kupitia Bunge. Tuliafikiana
kuwa, Jumuiya ya Wafanyabiashara baada ya kujadiliana ndani ya Kamati ya pamoja
iwasilishe mapema mapendekezo ya kurekebisha Mfumo wa Kodi unaolalamikiwa ili
maoni yao yajadiliwe kwenye Kamati ya Maboresho ya Mfumo wa Kodi (Task Force on Tax Reforms) wakati wa
mchakato wa maandalizi ya Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2015/2016 na kufanya
marekebisho stahiki. Hata hivyo, kwa kuwa suala hili litachukua muda
ninawashauri Wafanyabiashara waanze kulipa robo ya kodi ilivyo sasa ili kuepuka
kudaiwa malimbikizo baada ya Sheria kurekebishwa;
(d) Kwa kuwa Mfumo wa
Matumizi ya Mashine za Kielektroniki
una faida nyingi
na manufaa makubwa kwa Wafanyabiashara
na Serikali; na
kwa kuwa Mfumo huo unatumika
katika Nchi nyingi Duniani;
tumekubaliana kuwa, Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) iendelee
kuwahamasisha na kuwaelimisha Wafanyabiashara wenzao kuhusu umuhimu wa kutunza
kumbukumbu za biashara zao kwa kutumia Mashine za Kielektroniki za EFD na
kulipa kodi stahiki. Serikali inaahidi kuwa itaendelea kushughulikia changamoto
za kimfumo na utawala zilizopo za Matumizi ya Mashine za Kielektroniki za EFD
na tumesisitiza kuwa suala hili lijadiliwe kwenye Kamati ya Kitaifa iliyoundwa
ili kuzipatia ufumbuzi kwa haraka;
(e) Kuhusu suala la
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiasha Nchini, Bwana Johnson Estomihi Minja Kikao
kilielezwa kwamba, Bwana Minja alishtakiwa kwa makosa ya kuendesha Mikutano ya
uchochezi ya kuzuia matumizi ya Mashine za Kielektroniki na kuhamasisha
Wafanyabiashara kufunga maduka yao. Tuliwaeleza Viongozi wa Wafanyabiashara
kwamba suala hilo lipo chini ya Mamlaka nyingine ambayo ni Mahakama; na kwamba Mhusika
alirejeshwa rumande tarehe 26 Machi, 2015 kutokana na kukiuka mojawapo ya
masharti ya dhamana aliyopewa na Mahakama. Hivyo, siyo busara kwa Serikali
kuingilia uhuru wa Mhimili wa Mahakama. Serikali inaamini kuwa Mhusika
atatimiza masharti ya dhamana kesi yake itakapotajwa tena leo tarehe 01 Aprili,
2015; na hivyo kuachiwa huru. Taarifa zilizopatikana mchana wa leo zinaonesha
kwamba, Bwana Johnson Estomihi Minja amepata dhamana na yuko huru jioni ya leo;
(f)
Mwisho, tulikubalina kuwa kwa sababu Serikali imeonesha nia njema ya kushughulikia mapema iwezekanavyo malalamiko na changamoto
zinazowakabili Wafanyabiashara Nchini, ni vyema Viongozi wa Jumuiya ya
Wafanyabiashara baada ya Kikao kile, kwenda kutoa maelekezo kwa Wafanyabiashara
katika Mikoa yote Nchini kusitisha mara moja
mgomo unaoendelea na wawatake Wafanyabiashara kufungua maduka yao ili
Wananchi wapate huduma na bidhaa muhimu.
Mheshimiwa
Spika,
72.
Serikali inathamini sana mchango wa Wafanyabiashara katika Kukuza Uchumi
na kuchangia Mapato ya Serikali. Napenda kuwahakikishia Wafanyabiashara na
Wananchi wote kwamba, Serikali ipo tayari kukaa pamoja na Wafanyabiashara
kuzungumzia changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi wa haraka. Naomba
nitumie fursa hii kutoa Wito kwa Wafanyabiashara wote Nchini kufungua Maduka yao
ili waweze kutoa huduma muhimu za kuuza bidhaa kwa Wananchi. Nasisitiza kwamba,
utaratibu wa kutumia Mashine za Kielektroniki haukuwekwa kwa nia mbaya, bali
unalenga kumrahisishia Mfanyabiashara kutunza kumbukumbu za kila siku za
biashara na kuwawezesha kulipa Kodi Stahiki.
Mheshimiwa
Spika,
73.
Natoa Wito kwa Waheshimiwa Wabunge na Viongozi wa ngazi zote kushirikiana na Serikali kuwaelimisha
Wananchi na Wafanyabiashara kuhusu manufaa ya Matumizi ya Mashine za
Kielektroniki za EFD na kujenga tabia ya kufanya biashara kwa kutunza
kumbukumbu za mauzo ili kwa pamoja tushirikiane kujenga Nchi yetu na kuleta
Maendeleo Endelevu kwa kulipa Kodi Stahiki.
X: MALALAMIKO KUHUSU USAJILI MPYA WA BODABODA
Mheshimiwa
Spika,
74.
Pamoja na malalamiko hayo, yapo pia malalamiko ya Wafanyabiashara wa
Pikipiki na Bajaj ambao wanailalamikia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwamba
inawatoza Shilingi 250,000 hadi 300,000 kwa kusajili upya Pikipiki
moja. Wafanyabiashara ya Bodaboda wamesema Mmiliki mpya wa Pikipiki au Bajaj
anatakiwa kulipia leseni yake ya barabara pamoja na kodi nyingine ambazo ama
Mmiliki wa zamani hakuzilipia; au Makampuni yaliyowauzia Pikipiki na Bajaj hizo
hawajalipa kodi. Tulipokutana na Wafanyabiashara na Wenye bodaboda wanauliza
kwa nini Mamlaka ya Mapato Tanzania, isiwatafute wale Wamiliki wa zamani na
kuwadai Kodi husika.
Mheshimiwa
Spika,
75.
Nilikutana na Wafanyabiashara husika pamoja na Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), ambapo maelezo ya Kitaalam tuliyopewa ni kwamba tangu tarehe 1
Julai, 2014 Serikali ilifuta Leseni ya barabara kwa Pikipiki na kuwataka
Wamiliki wote kufanya Usajili upya. Katika zoezi hilo, Wamiliki wote wanatakiwa
kuhakikisha kuwa wamelipa ushuru na ada zifuatazo:-
Kwanza:
Kulipa Kodi
ya Usajili (Registration Fees) ambayo
ni Shilingi 10,000/= (kwa Wamiliki
Wapya);
Pili: Kulipia Ada ya
Leseni ya Barabara (Road Licence)
ya Pikipiki mpya ambayo ni Shilingi 50,000
kwa Mwaka;
Tatu: Kulipa Ada ya Zimamoto ambayo Sh.10,000 kwa Mwaka;
Nne: Kulipa Ushuru wa Stampu (Stamp Duty) ambao ni Asilimia moja (1%) ya thamani ya Pikipiki;
Tano: Kwa
wale walionunua Pikipiki kutoka kwa Wamiliki wa zamani wanatakiwa pia kulipa
Kodi ya Uhamisho wa Umiliki ambayo
ni takriban Shilingi 27,000/= pamoja
na ushuru wa Stempu (Stamp Duty) wa
Asilimia moja (1%) ya thamani ya
pikipiki husika.
Mheshimiwa Spika,
76.
Ili kuwezesha Wamiliki wa pikipiki kulipa kodi hizo kwa urahisi, Mamlaka
ya Mapato Tanzania kwa kuzingatia Sheria husika, ilitoa unafuu wa kumruhusu
Mlipa Kodi, kulipia Tozo na Ada hizo nilizozitaja kwa Awamu Nne (4) kwa mwaka. Ukomo wa muda wa kulipia kodi hizo ilikuwa
imepangwa kuishia tarehe 31 Machi, 2015. Baada ya Serikali kutatafakari kuhusu
malalamiko hayo ya Wamiliki wa bodaboda, imeamua kusogeza mbele muda wa ukomo
wa Usajili mpya wa Namba za Pikipiki hadi Mwezi Desemba, 2015.
XI: HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
77.
Kwa
kumalizia na kama ilivyo ada, naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru wote waliosaidia
kufanikisha mkutano huu. Kipekee nikushukuru wewe binafsi Mheshimiwa Spika, kwa
kutuongoza vizuri na kwa busara kubwa.
Niwashukuru Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri wanayofanya kila
wanapopata nafsi ya kukalia kiti cha Spika.
Aidha, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri ya kujadili na
kupitisha Miswada yote iliyowasilishwa wakati wa Mkutano huu.
Mheshimiwa Spika,
78.
Nitumie
nafasi hii pia kumshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake wote kwa kazi nzuri
ya kuhakikisha mkutano huu unakamilisha shughuli zake kama ilivyopangwa. Niwashukuru
Wataalam wote wa Serikali na Taasisi zake ikijumuisha Taasisi za Sekta Binafsi,
kwa misaada ya Kitaalam na huduma mbalimbali za kufanikisha Mkutano huu.
79.
Niwashukuru
pia Waandishi wa Habari kwa kazi nzuri walizofanya kuhakikisha kuwa taarifa za
majadiliano na maamuzi mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia Wananchi. Niwashukuru
Madereva kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuwasafirisha kwa usalama Waheshimiwa
Wabunge, Viongozi mbalimbali, Wataalam na Wasaidizi wote walioshiriki katika
Mkutano huu.
Mheshimiwa Spika,
80.
Nimalizie
kwa kuwatakia wote safari njema mnaporejea kwenye maeneo yenu ya kazi na katika
majimbo yenu. Ninaamini kwamba,
Mwenyezi Mungu atatulinda na kutuweka salama sote kama tulivyo hadi kukutana
tena katika Mkutano wa 20 wa Bunge lako Tukufu ambao ni mkutano wa mwisho
Kikatiba wa Bunge la Kumi na ambao utakuwa mahususi kujadili Bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Spika,
81.
Baada ya kusema hayo, naomba sasa kutoa Hoja
kwamba, Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 12 Mei, 2015 saa 3:00 Asubuhi litakapokutana katika
Mkutano wa 20 kwenye Ukumbi huu hapa
Dodoma.
Mheshimiwa Spika,
82.
Naomba kutoa Hoja.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “HOTUBA YA WAZIRI MKUU PINDA WAKATI AKIHARISHA MKUTANO WA BUNGE,DODOMA”
Post a Comment