Thursday, October 1, 2015
BUHARI AWATAKA RAIA NIGERIA WAACHE UTUNDU
Do you like this story?
Rais wa Nigeria
Muhammadu Buhari amewahimiza raia wa nchi hiyo waache “tabia ya utundu” ndipo
taifa hilo liweze kustawi.
"Ili kuleta mabadiliko, lazima
tubadilike na kuwa raia wanaotii sheria,” alisema akihutubu wakati wa sherehe
za kuadhimisha miaka 55 tangu uhuru wa taifa hilo.
Bw Buhari alikuwa kiongozi wa kijeshi 1984 na
1985, na aliagiza wafanyakazi wa serikali waliochelewa kazini kuruka juu kama
vyura, akijaribu kusisitiza nidhamu.
Alirejea uongozini Mei baada ya kushinda
uchaguzi.
Nigeria ndiyo nchi yenye watu wengi zaidi
Afrika, na pia ndiyo huzalisha mafuta kwa wingi zaidi barani.
Hata hivyo, wengi wa raia wake huishi maisha
ya umaskini, na taifa hilo hukumbwa na uhaba wa mafuta na umeme kupotea mara
kwa mara.
"Mabadiliko hayafanyiki hivyo tu,”
Buhari alisema akihutubia taifa hilo mara ya kwanza kabisa tangu aingie
mamlakani.
“Lazima tubadilishe tabia yetu ya utundu
katika shule, hospitali, sokoni, maegesho ya magari, barabarani, nyumbani na
afisini,” akaongeza.
Hakutoa maelezo yoyote kuhusu ni sera gani
ataanzisha kubadili tabia ya wananchi.
Miaka ya 1980, pamoja na kuaibisha
wafanyakazi wa serikali wasiokuwa na nidhamu, pia alituma wanajeshi kulazimisha
watu kupiga foleni wakisubiri magari ya uchukuzi wa umma.
Nigeria ina watu zaidi ya 166 milioni.
Bw Buhari, aliyesema majuzi kwamba atakuwa
waziri wa mafuta, pia ametetea vikali hatua yake ya kushindwa kuteua baraza la
mawaziri miezi minne baada ya kuchukua hatamu, akisema hataki kufanya uteuzi
huo bila kumakinika.
"Lakini msijali, hamtasubiri zaidi.
Kundi la kwanza la majina limetumwa kwa seneti,” alisema.
Majina hayo hayajatolewa hadharani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ BUHARI AWATAKA RAIA NIGERIA WAACHE UTUNDU”
Post a Comment