Thursday, October 8, 2015

DR SLAA AANZA KUMPIGIA KAMPENI MAGUFULI





Siku chache baada ya chama cha ACT-Wazalendo kutoa tamko rasmi kuwa hawataweza kumruhusu Dk. Wilbroad Slaa kupanda kwenye jukwaa lao kumnadi mgombea urais wa chama hicho kwa sababu za kiusalama, jana mwanasiasa huyo ameanza rasmi kumpigia kampeni mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli.

Akiongea jana kupitia Star TV , Dk. Slaa aliweka wazi mtazamo wake kuwa Dk. Magufuli ndiye anayefaa kuwa rais wa Tanzania kwa kulinganisha wote waliojitokeza kugombea nafasi hiyo.

Dk. Slaa alisema kuwa amengalia kigezo cha mtu anayeweza kupambana na ufisadi na amempa Dk. Magufuli asilimia 90 katika kigezo hicho.

“Ninasema sitamung’unya maneno, mimi nafikiri, baada ya kusikiliza mikutano michache ambayo nimeweza kusikiliza, na baada ya kuona clips mbalimbali kwa sababu siku hizi unaweza kuishi kwenye mwezi lakini ukapata taarifa ya kila mahali. Kwa hiyo mimi Napata taarifa kokote nilipo.

“Kwa kutazama yote hayo, mimi ambaye nimeendesha mapambano ya ufisadi ninatafuta rais ambaye atatuondoa kwenye ufisadi. Sasa aliyeniridhisha kwenye mapambano hayo baada ya kuona vigezo ni Magufuli. Sina njia nyingine ni lazima nichague mmoja. Na kumbuka tunapochagua rais hatuchagui vyama.. na haina maana kwamba mimi ni CCM, sina chama,

“Na tunapokwenda kwenye chumba cha kura tukumbuke tunamchagua kiongozi wa nchi, tusiangalie huyu ni wa chama gani. Je anatufaa au hatufai, anatufaa kwa nini. Kwenye vigezo vya rushwa, Magufuli nampa asilimia 90.”

Kadhalika, Dk. Slaa alieleza kuwa amekuwa akisikiliza sera za wagombea hao lakini anaona mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa anatoa hotuba isiyozidi dakika 10 bila kufafanua zaidi hivyo anaona hafai kuwa rais.

Dk. Slaa alitangaza kustaafu siasa baada ya kujiuzulu nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Chadema na kuachana na chama hicho kwa kile alichokieleza kuwa ni hakuridhishwa na uamuzi wa chama chake hicho cha zamani kumpokea Edward Lowassa.

Hata hivyo, Dk. Slaa alikiri kuwa yeye ndiye aliyepeleka wazo la kumkaribisha Lowassa kwenye chama hicho baada ya jina lake kukatwa na CCM mjini Dodoma na kunyimwa nafasi ya kugombea urais.

Dk. Slaa alieleza kuwa wazo hilo alilitoa kwa Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, ambaye alimtaja kama ‘mshenga’.

Juzi, akiwa katika jimbo la Karatu, Dk. Magufuli alimsifia Dk. Slaa na kumuita mtu safi na shujaa.

0 Responses to “DR SLAA AANZA KUMPIGIA KAMPENI MAGUFULI”

Post a Comment

More to Read