Thursday, October 8, 2015

WANAOMCHAFUA ZITTO KABWE MITANDAONI KUSHITAKIWA.




CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeliomba Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kufuatilia na kumchukulia hatua mtu aliyesambaza ujumbe katika mitandao ya kijamii, kuuchafua uislamu na kiongozi mkuu wa chama hicho, Kabwe Zitto.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na chama hicho jana, ilieleza kuwa, ujumbe huo kupitia mitandao ya kijamii ikiwamo Whatsapp, ilieleza Zitto ni mdini na kwamba ni jukumu la waislamu katika jimbo analowania la Kigoma Mjini, kuhakikisha wanamchagua kwa sababu ya Uislamu wake.

“Kama chama tumepokea ujumbe huo kwa masikitiko makubwa huku tukishindwa kuelewa nia halisi ya mwandika ujumbe katika kulinda amani ya nchi yetu, hasa wakati huu tunapoelekea katika uchaguzi mkuu wa madiwani wabunge na rais,” ilieleza taarifa hiyo iliyotolewa na Ofisa Habari wa chama hicho, Abdallah Khamis.

Aliziomba mamlaka husika, kufuatilia suala hilo kwa kina na kuchukua hatua za kisheria kwa muhusika kwani ACT-Wazalendo inatambua uadilifu wa kiongozi wao Zitto katika kusimamia misingi ya haki kwa watanzania wote hivyo si haki kuchafuliwa kwa misingi ya dini.

 

0 Responses to “ WANAOMCHAFUA ZITTO KABWE MITANDAONI KUSHITAKIWA.”

Post a Comment

More to Read