Thursday, October 8, 2015

HASSAN MWASAPILI: MBEYA CITY TUKO TAYARI KWA MCHEZO WETU NA SIMBA




Nahodha wa Mbeya City  Fc, Hassan Mwasapili amesema  wachezaji wote ndani ya kikosi chake wako tayari kwa mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara dhidi ya Simba Sc  ya Dar es Salam uliopangwa kucheza Oktoba17 mwaka huu kwenye uwanja wa Sokoine jijini  hapa.

Akizungumza na mbeyacityfc.com mapema jana,  Mwasapili ameweka wazi kuwa  huu ni mchezo ambao City inautizama kwa macho matatu ili kufufua upya matumaini yaliyofifia kutokana na matokeo mabaya kwenye michezo mitatu iliyopita.

“Tumejiandaa vizuri, tunataka kushinda mchezo huu dhidi ya Simba ili kufufua upya matumaini yetu kwenye ligi, tumekuwa na matokeo mabaya kwenye michezo mitatu iliyopita, tulipoteza dhidi ya Azam Fc na pia Stand United na tukapata pointi moja  dhidi ya Toto Africans kufuatia sare ya bao 1-1 kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, ndiyo maana nadiriki kusema huu ni mchezo ambao tunataka kushinda ili kulinda heshima yetu kabla ya kutizama michezo mingine” alisema.

Akiendelea zaidi nahodha huyo wa City alisema kuwa ligi ya msimu huu inachangamoto nyingi kuliko ya msimu uliopita kufuatia kuwepo kwa ushindani mkubwa kwenye kila mchezo unaochezwa  dimbani akiwa na maana kuwa timu nyingi zimefanya maanadalizi makubwa kuukabili msimu huu.

“Msimu umekuwa na changamoto nyingi, timu zimejiandaa sana kuukabili ligi, sisi hatukuwa na muda mrefu wa maandalizi lakini sasa tumeimarika, nina imani kubwa mpaka mwisho ligi tutakuwa katika nafasi nzuri ya juu kwenye msimamo, bado nia yetu ni kucheza mashindano ya CAF, na hili linawezekana licha ya kuwa tumepoteza michezo  minne hivi sasa”. alimaliza.

City inakuatana na Simba  ukiwa ni mchezo wa tano kwa timu hizi  huku kikosi cha Msimbazi kikiwa kimeambulia kichapo mara mbili na sare mbili kwenye michezo minne ya awali, mchezo wa mwisho kwa timu hizi kukutana ilikuwa ni kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ambapo Simba ilikubali  kichapo cha mabao 2-0, mabao yaliyofungwa na Rafael Daud na Peter Mwalyanzi ambaye kwa sasa anacheza kwenye kikosi cha timu hiyo ya Msimbazi.

Wakati huo huo daktari mkuu wa City, Dr Joshua Kaseko amethibitisha kuwa nyota wote ndani ya kikosi wako na afya njema  na hakuna majeruhi yeyote na kuweka wazi kuwa  kwa ujumla hali ya kambi ya City kuelekea mchezo huo wa tarehe 17 ni nzuri kabisa.

0 Responses to “HASSAN MWASAPILI: MBEYA CITY TUKO TAYARI KWA MCHEZO WETU NA SIMBA ”

Post a Comment

More to Read