Monday, October 5, 2015

SIMBA SASA YAKATA MISHAHARA YA WACHEZAJI




Nicodemus Jonas na Khadja Mngwai
Simba imechunguza tabia na nidhamu ya wachezaji wa Kibongo na kubaini kuwa wengi wao hufanya mazoezi kwa sababu tu ni sheria na siyo kwa utashi wa mioyo yao, hivyo imeamua kuja na mkakati wa kuhakikisha kila mmoja anaitumikia timu kwa moyo mkunjufu.


Uongozi wa Simba umeanzisha mfumo wa kuwakata mishahara wachezaji wote watakaoshindwa kufanya mazoezi pasipo sababu ya msingi wala kutoa taarifa sehemu husika, jambo ambalo linamaanisha inataka kila mmoja kili yake iwepo kwa ajili ya kuisaidia timu.

Ni wazi kuwa Simba bado inajijenga baada ya kupotea kimataifa katika misimu mitatu mfululizo, hivyo inahitaji kuwa na wachezaji wenye ari ya ushindi kwa timu nzima na wenye nidhamu ya kufanya mazoezi.

Mratibu wa klabu hiyo, Abass Suleiman Ally, Ijumaa aliwaweka kikaoni nyota wote na kuwaeleza utaratibu huo na kuwataka kila mmoja anapokuwa na udhuru ni lazima atoe taarifa sehemu husika na kwamba siyo jukumu la kiongozi kumuuliza mchezaji kwa nini hajafika mazoezini, vinginevyo wasilaumiane mwisho wa mwezi wakikuta akaunti zao zinapungukiwa.

“Nilitaka kuwaweka wazi, kila mchezaji atambue kuwa asipokuja mazoezini, hakuna tena kiongozi kuanza kumtafuta mchezaji kumuuliza sababu za kutofika, badala yake mchezaji ndiye atoe taarifa kama atakuwa na udhuru.

Tumepanga yeyote ambaye atakosa mazoezi pasipo taarifa sehemu husika, wajibu wangu ni kurekodi watoro na mwisho wa mwezi tusije kulaumiana akikuta amekatwa mshahara,” alisema Ally bila kufafanua watakuwa wakikata asilimia ngapi kila mchezaji anapokosa mazoezi.

0 Responses to “ SIMBA SASA YAKATA MISHAHARA YA WACHEZAJI”

Post a Comment

More to Read