Thursday, October 8, 2015
SIRI YA MGAWO WA UMEME HII HAPA
Do you like this story?
Wakati
watu mbalimbali wakiwamo wanasiasa wakilishutumu Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco) kutokana na hali mbaya ya kukatika ovyo kwa umeme, imebainika kuwa
chanzo cha tatizo hilo ni uzalishaji duni wa nishati hiyo katika mabwawa na
vyanzo vingine vyote vinavyotegemewa na shirika hilo.
Kadhalika,
imeelezwa kuwa maamuzi mbalimbali ya kisiasa ndiyo yanayochangia kwa kiasi
kikubwa kuwapo kwa mgawo wa umeme na kusababisha kero kwa watumiaji wake huku
pia shughuli za kiuchumi zikiathiriwa kwa kiasi kikubwa.
Nipashe
inatambua kuwa kabla ya kuwapo kwa mitambo mipya ya kuzalisha umeme itokanayo
na utekelezaji wa miradi mbalimbali, Taifa lilikuwa likitegemea vyanzo vikuu
vitatu vya nishati hiyo, ambavyo kwa ujumla wake vilikuwa na uwezo wa kuzalisha
Megawati 1,226. Vyanzo hivyo vitatu ni umeme utokanao na maji uliokuwa
ukichangia asilimia 45.8 kwa kutoa Megawati 561; Megawati 435, sawa na asilimia
35.9 kutoka umeme wa gesi na chanzo kingine ni cha mafuta, chenye Megawati 230
(asilimia 18.8) ya umeme wote unaozalishwa nchini.
Katika taarifa
yake kwa umma ambayo Nipashe inayo nakala yake, Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa
Tanesco inaeleza kwa kina juu ya hali halisi ya upatikanaji wa umeme nchini,
ikisema kuwa inafanya hivyo kwa nia ya kuondoa minong’ono, uzushi na kuwapo kwa
taarifa nyingi za kubuni, hasa kwenye mitandao ya kijamii.
Taarifa hiyo
inafichua ukweli kuwa kwa ujumla, uzalishaji wa nishati hiyo katika mabwawa
yote nchini ni wa kiwango cha chini ya asilimia 20, huku hali ikiwa mbaya zaidi
katika Bwawa la Mtera ambalo hivi sasa halizalishi kabisa. Kadhalika, hali siyo
nzuri katika vyanzo vingine vya kuzalisha umeme vya gesi na mafuta.
UMEME WA MAJI
Inaelezwa kuwa
hivi sasa, mabwawa karibu yote yanayotegemewa kuzalisha umeme wa maji yamekuwa
hayazalishi ipasavyo kwa sababu ya kukosekana kwa maji na kwamba, baadhi ya
mabwawa hayo hivi sasa yanaelekea kukauka.
Kwa ujumla
wake, taarifa hiyo inaonyesha kuwa kiwango cha juu cha uzalishaji wa umeme
kinachotarajiwa kutokana na mabwawa sita ya Mtera, Kidatu, Pangani, Nyumba ya
Mungu, Hale na Kihansi ni Megawati 561.
Hata hivyo,
hadi kufikia Oktoba 4, mwaka huu, uzalishaji wa umeme katika mabwawa hayo yote
ulikuwa ni Megawati 105 (asilimia 18.7) ya kiwango kinachotarajiwa.
“Kwa lugha
sahihi, uzalishaji umeme katika mabwawa ya maji umeshuka kwa 81.3%,” inasema
sehemu ya taarifa hiyo ya Mkurugenzi wa Tanesco.
Taarifa
inafafanua kwa kina hali ya uzalishaji katika kila bwawa, ikieleza kuwa Mtera
lenye uwezo wa kuzalisha Megawati 80, hivi sasa halizalishi kabisa kutokana na
maji yake kupungua hadi kiwango cha mwisho kinachotakiwa kuzalisha nishati
hiyo.
Bwawa la Kidatu
linaloongoza kwa kuzalisha umeme mwingi kulinganisha na mengine wa Megawati
204, hivi sasa limepungukiwa maji kiasi cha kuzalisha Megawati 27 tu (asilimia
13.2) ya uwezo wake wa juu.
Katika Bwawa la
Kihansi lenye uwezo wa juu wa kuzalisha Megawati 180, uzalishaji wake hivi sasa
umeshuka hadi Megawati 51.5 (asilimia 28.6) tu ya uwezo wake.
Upungufu wa
maji umelikumba pia Bwawa la Nyumba ya Mungu lenye uwezo wa juu wa kuzalisha
Megawati 8, lakini bado linazalisha Megawati 5.5 tu (asilimia 68.8) ya uwezo
wake wa juu; Bwawa la Hale lenye uwezo wa kuzalisha Megawati 21 hivi sasa
linazalisha Megawati 4 (asilimia 19) na maporomoko ya maji ya Pangani (New
Pangani Falls) yenye uwezo wa kuzalisha Megawati 68, yameathiriwa na kupungua
kwa kiwango cha maji hadi kuzalisha Megawati 17 tu (asilimia 25).
UMEME
WA GESI
Baada ya
kuporomoka kwa kiwaango cha uzalishaji wa umeme utokanao na chanzo cha maji,
ilitarajiwa kuwa vyanzo vingine kama uzalishaji wa nishati hiyo unaotegemea
gesi kuokoa jahazi.
Hata hivyo,
taarifa inafichua kuwa hadi sasa, Tanesco inashindwa kupata ahueni
inayotarajiwa kutoka katika chanzo hiki kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni
hatua ya wazalishaji wa gesi ya Songosongo inayotoa umeme huo, kampuni ya Pan
Africa, kushindwa kutoa kiwango kinachotakiwa cha Megawati 340 kilichokuwa
kikizalishwa awali na sasa kuzalisha Megawati 260 tu (asilimia 76.5).
Tanesco
wanaeleza katika taarifa yao kuwa hivi sasa, wazalishaji hao wa umeme wa gesi
(Pan Africa), wamewaambia kuwa wanaboresha visima vyao na kazi hiyo
ikikamilika uzalishaji utaongezeka.
“Japo ukarabati
huo utatuhakikishia gesi zaidi baadaye, lakini wakati huu wa matengenezo
panakuwa na uhaba wa gesi kutoka Songosongo,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
UMEME
WA MAFUTA
Taarifa ya
Tanesco inafichua vilevile ukweli mchungu kuwa uzalishaji wa umeme kwa mitambo
ya mafuta umeshuka pia, kutoka kiasi cha Megawati 230 kilichokuwa kikipatikana
awali hadi kufikia Megawati 190 (asilimia 82.6). Hata hivyo, haielezwi ni kwa
nini uzalishaji wa umeme wa mafuta umeshuka kwa kiwango hicho.
UZALISHAJI
BOMBA JIPYA LA GESI
Inaelezwa
katika tarifa ya Tanesco kuwa zipo jitihada kadhaa zinazofanywa kuhakikisha
kuwa bomba jipya la gesi lililowashwa linazalisha umeme kwa kiwango
kinachotarajiwa. Inaelezwa kuwa hivi sasa mitambo ya kuzalisha umeme kwa gesi
ya bomba jipya iliyowashwa ni Megawati 90 na mwingine wa Megawati 35.
Taarifa
inafafanua zaidi kuwa mitambo mingine inayotarajiwa kuongeza uzalishaji wa
umeme ndani ya wiki moja hadi mbili ni Symbion (Megawati 20), Ubungo II
(Megawati 35), Songas (Megawati 20) na Kinyerezi Megawati 70.
Inaelezwa
mwisho wa siku, matarajio ni kuona kuwa uzalishaji wa mitambo mipya ikiwamo
miwili ya Kinyerezi inaihakikishia Tanesco Megawati 305 zaidi ya umeme
unaopatikana sasa na ndipo kutakapokuwa na uhakika wa kueleza kuwa tatizo la
umeme nchini limemalizika.
Kadhalika,
taarifa ya Tanesco inaeleza sababu za kutoa taarifa zenye matumaini ambazo
nyingine zimetofautiana na uhalisia.
“Ni muhimu pia
Watanzania watuelewe kwamba kila kitu hakiko katika uwezo wetu. Hii ni kwa
sababu baadhi ya mitambo ya kuzalisha umeme na pia mifumo ya gesi siyo ya kwetu
na inamilikiwa na watu wengine.
Hivyo taarifa
tulizokuwa tunazipokea kutoka kwa makampuni haya ndizo tumekuwa tukiwapatia
wateja wetu na bahati mbaya baadhi yake hazikuwa kama tulivyokuwa tumeelezwa,”
sehemu ya taarifa ya Tanesco inaeleza.
Mbali na
mitambo ya Tanesco, umeme unaopatikana kwa sasa unatoka kwa kampuni za Songas,
Symbion, Aggreko na IPTL huku mfumo wa gesi unahusisha kampuni za Pan Africa
Energy, TPDC na M&P.
WASOMI
WAZUNGUMZIA TATIZO LA UMEME
Dk. Donath
Olomi wa Chuo cha Uongozi na Ujasiriamali, anasema matatizo ya umeme yaliyopo
sasa ni matokeo ya usimamizi mbovu, hasa kwenye suala la mikataba kwani haiko
wazi.
Alisema kuna
athari kubwa katika mgawo huo na ushahidi ni Tanesco kupata hasara ya Sh.
milioni 500 kwa siku kutokana na kukosa mapato. Pia, alisema athari nyingine ni
kwa wenye viwanda ambao sasa hujiendesha kwa gharama kubwa kwa kutumia
majenereta huku viwanda vingine vikilazimika kusimamisha uzalishaji.
Alisema njia
mojawapo ya kuondokana na matatizo ya kupatikana kwa umeme wa uhakika ni
kuipunguzia Tanesco baadhi ya majukumu iliyo nayo sasa.
Makamu Mkuu
mstaafu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa Tolly Mbwete, alisema
Tanesco inatakiwa kutoa maelezo ya kina kuhusiana na tatizo la kukatika kwa
umeme.
“Walisema kuna
mitambo ya gesi inatengenezwa na imemalizika... sasa inakuwaje kuna mgawo na ni
kwa nini wanakaa kimya hadi wanasiasa wanaliingilia,” alisema Profesa Mbwete.
Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Prosper Ngowi, alisema kukosekana kwa umeme wa
uhakika nchini kutaleta madhara makubwa kiuchumi ikiwa ni pamoja na kutovutia
wawekezaji wa uhakika wa ndani na nje ya nchi.
Alisema hata
sasa wawekezaji wengi wamekuwa wakilalamikia kukosekana kwa nishati yenye uhakika
na hivyo, suala hilo linapaswa kutafutiwa suluhisho la kudumu.
Mkurugenzi wa
Sera na Ushawishi wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI), Hussein
Kamota, alisema ni wazi kwamba kuna hasara kubwa imepatikana kwa wanachama wao
na kwamba, wanafanya tathmini na taarifa yao wataitoa kwa umma kesho.
SOURCE: NIPASHE
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “SIRI YA MGAWO WA UMEME HII HAPA”
Post a Comment