Monday, November 9, 2015

BAVICHA YAIPA SERIKALI SAA 72 KUTOA MIKOPO KWA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU.




Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), limetoa saa 72 kwa Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB) kuhakikisha inawapa mikopo wanafunzi wote waliobaki wa Vyuo Vikuu na wakishindwa kufanya hivyo wataitisha mgomo nchi nzima.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa BAVICHA, Julias Mwita, alisema Serikali ya CCM iliamua kuiga ilani ya CHADEMA bila kujipanga na matokeo yake wanafunzi wa Elimu ya Juu zaidi ya asilimia 82 wamekosa mikopo.

Alisema wanafunzi wengi waliokosa mikopo wanatoka katika familia maskini jambo ambalo haliwezi kukubalika hivyo wao wameshafanya maandalizi yote ya migomo kwa wanafunzi wote waliokosa mikopo nchi nzima hivyo wanachosubiri ni kumalizika saa 72 walizotoa kama jambo hilo lisipotekelezwa wachukue hatua.

"Sisi tuna mitandao ya wafunzi wa Elimu ya Juu nchi nzima, licha ya kufanya mgomo tutawafundisha njia nyingine ya kudai haki yao bila uvunjifu wa amani... mimi nilikwenda rumande siku tisa tangu Oktoba 25, mwaka huu, nilikuwa naongoza kundi la watu 40 kukusanya matokeo ya Uchaguzi Mkuu nchi nzima.

"CCM nao walikuwa wakifanya hivyo pale Mlimani City na Golden Tulip lakini cha ajabu, sisi ndio tuliokamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kusambaza taarifa wakati wenzetu walikuwa wakifanya kazi kama hiyo," alisema Mwita.

Aliongeza kuwa, aliyekuwa mgombea urais wa CHADEMA anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa alidhalilishwa kwa kutukanwa kila aina ya matusi na viongozi wa CCM na wengine walifikia hatua ya kusema hawaiachi Ikulu au kukabidhi nchi kwa makaratasi.

"Pamoja na maneno haya kuzungumzwa na wana CCM, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na polisi lakini ingekuwa sisi, tungekuwa rumande," alisema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Uhamasishaji Taifa wa BAVICHA, Edward Simbeye, alisema wao wanaamini aliyekuwa mgombea wao wa urais alishinda lakini ameporwa ushindi wake.

"CCM wana Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu ambao na wao wamekosa mikopo, wanafunzi wote waliokosa mikopo wataandamana hadi Bodi ya Mikopo kutoka nchi nzima kwani hili ni jambo kubwa lisiloweza kufumbiwa macho," alisema.

0 Responses to “BAVICHA YAIPA SERIKALI SAA 72 KUTOA MIKOPO KWA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU.”

Post a Comment

More to Read