Monday, November 9, 2015
MWAKALEBELA ATINGA KORTINI KUMPINGA MSIGWA
Do you like this story?
Aliyekuwa
mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini (CCM), Frederick Mwakalebela amefungua
kesi kupinga ushindi wa Mchungaji Peter Msigwa (Chadema).
Naibu Msajili
wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Ruth Massama alisema juzi kuwa kesi hiyo namba
5 ya mwaka 2015 ya kupinga matokeo, imesajiliwa rasmi Oktoba 30.
Katika shauri
hilo, Mwakalebela anawatuhumu Mchungaji Msigwa na msimamizi wa uchaguzi wa
jimbo hilo, Ahmed Sawa kukiuka taratibu kanuni na Sheria ya Uchaguzi na
kuchangia yeye kupata matokeo mabaya.
Mshtakiwa wa
kwanza katika kesi hiyo ni Mchungaji Msigwa anayedaiwa kufanya kampeni siku ya
uchaguzi kwa kuvaa kofia yenye nembo ya M4C ikiwa na picha za vidole viwili,
alama zinazotumiwa na Chadema.
Pia,
Mwakalebela anamtuhumu msimamizi wa uchaguzi kwa kuanza kujumlisha matokeo
akiwa na mtuhumiwa wa kwanza pamoja na mawakala wa mtuhumiwa huyo, bila yeye
kujulishwa wala kushirikishwa.
Katika dai lake
la tatu, Mwakalebela analalamikia kuzuiwa kuingia kwenye kituo cha kupigia kura
kilichopo Mtaa wa Dabodabo, Kata ya Ilala wakati mgombea mwenzake wa Chadema
aliruhusiwa kuingia bila pingamizi.
Mwakalebela
ameambatanisha madai hayo pamoja na barua yake ya Oktoba 25 aliyoituma kwa
msimamizi wa uchaguzi akizuia kazi ya kutangaza matokeo kuendelea, huku akitoa
sababu tano zilizomsukumu kufanya hivyo.
Akitoa
ufafanuzi wa kesi hiyo, Massama alisema taratibu zinawataka baada ya kufungua
kesi za uchaguzi, kuwajulisha walalamikiwa na kuweka maelezo kwenye mbao za
matangazo kwa siku 14 ili kusubiri kama kutakuwa na pingamizi.
Pia, chama
hicho kinajipanga kufungua kesi ya kupinga ushindi wa madiwani wa Chadema wa
kata zilizopo kwenye jimbo hilo kwa kuwa kuna kasoro zinazolalamikiwa.
Katika Uchaguzi
Mkuu, Mchungaji Msigwa alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 43,154 dhidi ya
32,406 alizopata Mwakalebela.
Wagombea
wengine ni Chiku Abwao wa ACT Wazalendo aliyepata kura 411, Daudi Masasi wa ADC
(123), Paulina Mgimwa wa Chausta (66) na Robert Kisinini wa DP (56).
Wakati huohuo,
katibu wa Chadema wa Mkoa wa Njombe, Alatanga Nyagawa amesema chama chake
kinakamilisha utaratibu wa kisheria wa kukata rufaa kupinga matokeo ya uchaguzi
katika majimbo ya Njombe Kusini na Makambako.
Nyagawa alisema
hatua hiyo inakuja baada ya kutoridhishwa na mwenendo mzima wa uchaguzi katika
majimbo hayo kwa kile alichodai kuwa kulikuwa na hujuma zilizofanywa na
wapinzani wao, hivyo kukosa ushindi.
“Siyo kwamba
maeneo mengine hatukufanyiwa uhuni, lakini katika majimbo hayo tunatarajia
kukata rufaa mahakamani kwa kuwa tumefanyiwa hivyo mchana kweupe,” alisema
Nyagawa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MWAKALEBELA ATINGA KORTINI KUMPINGA MSIGWA ”
Post a Comment