Wednesday, December 23, 2015
WAZIRI LUKUVI ASITISHA ZOEZI LA BOMOA BOMOA DAR
Do you like this story?
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi imesimamisha kazi ya bomoabomoa kwa siku 15 kwa wavamizi waliojenga
katika Bonde la Mto Msimbazi, Dar es Salaam na kuwataka wavamizi hao kubomoa
wenyewe na kuondoka maeneo hayo, kabla ya kazi hiyo kuanza tena Januari 5,
mwakani.
Aidha, wale wote waliojenga kwenye maeneo ya
wazi, wavamizi wa maeneo ya watu, maeneo ya shughuli za kijamii kwenye fukwe,
kingo za mito na vyanzo vya maji nchi nzima, kazi ya ubomoaji itaanza mapema
Januari mwakani na kwamba hakuna atakayefidiwa.
Hayo yalibainishwa jana Dar es Salaam na
Waziri wa Wizara hiyo, William Lukuvi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa
Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba, wakati wakizungumza na waandishi
wa habari.
Lukuvi alisema wameamua kusimamisha kwa muda
kazi hiyo ili kutoa nafasi kwa wavamizi hao kubomoa wenyewe nyumba walizojenga
kinyume cha sheria ili waambulie vitu vyao na baada ya muda uliotolewa
kumalizika, kazi ya ubomoaji itaendelea na hakuna atakayelipwa fidia.
Alisema katika eneo hilo la Bonde la Mto
Msimbazi, nyumba 8,000 zimejengwa isivyo halali na hadi sasa nyumba 395,
zimebomolewa kwa siku tatu kuanzia Desemba 17 na kwamba wavamizi hao
wasitegemee kulipwa fidia.
“Hakuna fidia kwa wavamizi hao, kama huku
nyuma kuna watu walionewa huruma kwa sababu ya maafa na kupewa viwanja, ilikuwa
ni huruma tu, hakuna sheria inayomruhusu mtu kujenga kwenye eneo hatarishi,
hivyo tutakuondoa tu na hakuna fidia,” alifafanua Lukuvi.
Alisema hakuna nyaraka zilizotolewa kwa
wavamizi hao kujenga maeneo hayo, na kama kuna mtu ana kibali cha ujenzi kwenye
eneo hilo hatarishi au kingo za mto, sheria ya mazingira itamuondoa na hakuna
watakaoachwa.
Kwa upande wake, January alisema Sheria ya
Mazingira iko wazi na inakataza watu kufanya shughuli kwenye maeneo
yasiyoruhusiwa kwa sababu za kulinda mazingira na vyanzo vya maji.
Amesema kuanzia mwakani, wizara hiyo
itaendesha operesheni ya kuwaondoa watu wanaoishi na kufanya shughuli kwenye
maeneo ya kingo za mito na maziwa, fukwe za bahari, maeneo oevu na maeneo ya
wazi. Kwa Dar es Salaam, maeneo ya wazi 180 yamevamiwa, kati ya hayo 111 yapo
Halmashauri ya Kinondoni, 50 yapo Ilala na Temeke yapo 19.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
.gif)



0 Responses to “ WAZIRI LUKUVI ASITISHA ZOEZI LA BOMOA BOMOA DAR”
Post a Comment