Saturday, May 14, 2016
MAPATO HOSPITALINI YANUKA UFISADI.....VIFAA VYA KIELRKTRONIKI VYA KUYAKUSANYA VYAIDUWAZA SERIKALI
Do you like this story?
Ufungaji
wa vifaa vya kielektroniki katika hospitali za Serikali katika mikoa
mbalimbali, umeibua fukuto la ufisadi mkubwa, uliokuwa ukifanywa katika
makusanyo ya fedha wanazolipa wagonjwa kwa ajili ya huduma.
Akizungumza
bungeni mjini Dodoma jana katika kipindi cha maswali na majibu, Naibu Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani
Jafo, alisema tangu mfumo huo wa kielektroniki uanze kutumika katika hospitali
nyingi nchini, mapato yameongezeka.
Jafo
alisema mafanikio hayo ya ukusanyaji wa mapato kwa mfumo wa elektroniki,
yamesababisha katika sekta ya afya kwa sasa ajenda kuu iwe kuongezea mapato ya
hospitali zote nchini, kuendane na utoaji wa huduma bora.
Hospitali
ya Rufaa Mbeya
Akitoa
mfano wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Jafo alisema kabla ya kufungwa kwa vifaa
hivyo, ilikuwa ikikusanya Sh milioni 70 kwa mwezi, lakini baada ya kufungwa
vifaa hivyo, mapato yameongezeka zaidi ya mara saba na kufikia Sh milioni 500
kwa mwezi.
Taarifa
zinaonesha pamoja na ongezeko hilo la mapato, bado hospitali hiyo iliendelea
kukosa vifaa muhimu vya tiba, ikiwemo mashine ya CT-Scan, kiasi cha kusababisha
mwanzoni mwa mwaka huu Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Dk Hamis Kigwangalla kuwajia juu watendaji wake.
Dk
Kigwangalla alielezea kushangazwa kuona hospitali hiyo ikikusanya Sh milioni
500 kwa mwezi, huku ikidai kukosa CT-Scan na kutoa siku 60 kifaa hicho
kifungwe.
Katika
maelezo aliyopewa, Dk Kigwangalla alielezwa kuwa ingawa ni kweli hospitali hiyo
inakusanya Sh milioni 500 kwa mwezi, lakini mahitaji ya dawa pekee yanachukua
zaidi ya Sh milioni 300, kabla ya gharama nyingine ikiwemo za usafiri wa
magari.
Alielezwa
kuwa hospitali hiyo imejipanga kuchukua mkopo kutoka Mfuko wa Bima ya Afya ya
Taifa (NHIF), kwa kuwa ili kupata mashine hiyo, wanapaswa kuwa na kuanzia Sh
milioni 800 mpaka Sh bilioni 1.2.
Sekou
Toure
Mbali na
Mbeya, katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure kwa mujibu wa Jafo,
kabla ya kufungwa kwa vifaa hivyo, ilikuwa ikikusanya kati ya Sh 150,000 mpaka
200,000 tu kwa siku.
Jafo
alisema baada ya kufungwa vifaa hivyo, mapato hayo yaliongezeka mpaka karibu
mara 21 na kufikia Sh milioni 3.2 kwa kila siku.
Hospitali
ya Tumbi
Mbali na
Mwanza, Naibu Waziri huyo wa Tamisemi, alisema mkoani Pwani katika Hospitali ya
Tumbi, nako kabla kufungwa vifaa hivyo, makusanyo yalikuwa Sh 200,000 kwa siku
lakini baada ya kufungwa, mapato yakaongezeka mara 20 na kufikia Sh milioni nne
kwa siku.
Kutokana
na mafanikio ya hospitali hizo, Jafo aliwataka wabunge wote kufuatilia kwa
makini hospitali katika halmashauri zao za wilaya, ili kila moja iweke mfumo wa
kielektroniki kwa ajili ya kukusanya mapato katika huduma ya afya.
Aliwataka
wabunge hao kuweka kipaumbele katika kuhakikisha hospitali zote katika maeneo
yao, zinafungwa mifumo hiyo ya kielektroniki, ili fedha zikusanywe kusaidia
katika kuboresha huduma za afya katika maeneo hayo.
“Tusipozingatia
haya, hata tukipeleka fedha bado tutakuwa na matatizo, ndio maana ajenda yetu
kuu ni kutumia mifumo ya kielektroniki, ili kuongeza mapato katika sekta ya
afya,” alisisitiza.
Awali
Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi (CCM), alitaka kufahamu kama Serikali
haioni umuhimu wa kuiongezea fedha Hospitali ya Mji wa Mafinga, ili ihudumie
kwa ufanisi idadi kubwa ya wagonjwa wanaohudhuria hospitali hiyo.
Pia Mbunge
huyo alitaka kufahamu kama Serikali iko tayari kuiongezea hospitali hiyo
watumishi mara mbili zaidi ya kiwango inachopata, ili iwe na uwezo wa kutosha
kukabiliana na mzigo wa kazi.
Akijibu
maswali ya mbunge huyo, Jafo alisema Serikali imekuwa ikiipatia Hospitali ya
Mji wa Mafinga Sh milioni 90 kwa ajili ya maendeleo na Sh milioni 90 kwa
matumizi mengineyo ; na kwamba inaweza kuongezewa fedha hizo kulingana na wigo wa
upatikanaji wa fedha.
Kuhusu
watumishi, alisema hospitali hiyo ina watumishi 209 na upungufu uliopo ni wa
watumishi 95, sawa na asilimia 31.3 na kwa mwaka wa fedha 2016/17
imeidhinishiwa kuajiri watumishi 18.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ MAPATO HOSPITALINI YANUKA UFISADI.....VIFAA VYA KIELRKTRONIKI VYA KUYAKUSANYA VYAIDUWAZA SERIKALI”
Post a Comment