Wednesday, June 29, 2016
SERIKALI YAKANUSHA KUPIMA UKIMWI NYUMBA KWA NYUMBA.
Do you like this story?
Kumekuwepo
na taarifa mbalimbali zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii zinazotokana na
habari iliyoandikwa na kuchapishwa kwenye gazeti la Jambo leo la tarehe 24
Juni, 2016, toleo namba 2482 yenye kichwa cha habari "Sasa ukimwi
kupimwa nyumba kwa nyumba".
Ofisi ya
Taifa ya Takwimu (NBS) inapenda kutoa ufafanuzi kwamba UKIMWI HAUTAPIMWA NYUMBA
KWA NYUMBA bali itafanya utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania
kuanzia mwezi Septemba 2016 ambapo UKIMWI utapimwa kwenye kaya chache ambazo
zimechaguliwa kitaalam nchi nzima ili ziweze kuwakilisha kaya nyingine nyingi
ambazo hazitahusika moja kwa moja katika utafiti huu.
Utafiti
huu utajumuisha kaya zipatazo 16,000 ambazo ni sampuli iliyochaguliwa kisayansi
kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar na utahusisha watu wazima
wasiopungua 40,000 wakiwemo watoto takribani 8,000.
Aidha,
katika utafiti huu kutakuwa na kupima homa ya ini, kupima wingi wa chembechembe
za damu yaani CD4, kupima wingi wa virusi katika damu na kupima kiwango cha
ufanisi wa dawa za kufubaza VVU kwa watu wanaotumia dawa hizo.
Ifahamike
kwamba, utafiti huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI wa mwaka 2016 unafanyika
nchini kwa mara ya 4 ambapo utafiti wa kwanza ulifanyika mwaka 2003, wa pili
ulifanyika mwaka 2007 na wa tatu ulifanyika mwaka 2011.
Hivyo,
Ofisi ya Taifa ya Takwimu inapenda kuwatoa hofu wananchi kwakuwa utafiti huu
sio mpya katika nchi yetu na watanzania ambao wamekuwa wakipitiwa na utafiti
huu, wamekuwa wakitoa ushirikiano kwa zaidi ya asilimia 90.
Utafiti
huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utaendeshwa na Ofisi ya Taifa ya
Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto kwa Tanzania Bara, Wizara ya Afya kwa Tanzania Zanzibar, Ofisi
ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar (OCGS), Tume ya Taifa ya Kudhibiti
UKIMWI (TACAIDS) na Tume ya UKIMWI Zanzibar (ZAC).
Imetolewa
na:
Mkurugenzi
Mkuu,
Ofisi ya
Taifa ya Takwimu (NBS),
Dar es
Salaam,
28 Juni,
2016.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “SERIKALI YAKANUSHA KUPIMA UKIMWI NYUMBA KWA NYUMBA.”
Post a Comment