Monday, October 31, 2016
ASKARI JWTZ MBARONI KWA TUHUMA ZA WIZI WA MTOTO
Do you like this story?
POLISI mkoani Tabora inamshikilia askari wa Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ),kwa tuhuma za kuiba mtoto mchanga,Razack Kombo,
mwenye umri wa miezi miwili.
Habari za uhakika ambazo MTANZANIA ilizipata
jana na kudhibitishwa na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Tabora,Khamis Issa,
zinasema askari huyo wa Kikosi cha Jeshi Mirambo, anashikiliwa baada ya
kichanga hicho kufariki dunia katika mazingira ya kutatanisha.
“Tunamshikilia askari huyo tangu wiki iliyopita
kwa kosa la wizi wa mtoto mchanga ambaye pia alifariki dunia katika hali
iliyojaa utata ingawa bado tunaendelea kufanya mahojiano naye ili atueleze
namna hali ilivyokuwa.
“Hivi ninavyoongea na wewe niko nje ya
ofisi,lakini wasaidizi wangu wamenijulisha wamemkamata.Haiingii akilini mtu
aibe kichanga hiki alafu kipoteze uhai ndani ya muda mfupi, tena mwili wake
umekutwa kwenye moja ya hospitali ya jeshi,japokuwa taarifa zinaonyesha alikuwa
haumwi.
“Kama ningekuwa ofisini, ningeweza kukutajia
namba za askari huyo pamoja na majina kamili kwa sababu tunayo.
“Lakini, nakuomba univumilie kama nitawahi
kurudi ofisini, tutawasiliana zaidi.
“Katika mahojiano ya awali, askari huyo alisema
alikuwa anakwenda likizo ya uzazi nyumbani kwao,japo hakuwa na ujauzito.
“Inaonekana mama wa mtoto aitwaye Daphina
Matwika, alikuwa anasafiri kutoka Morogoro kwenda Mpanda kule Katavi akiwa na
watoto wengine wakubwa wawili.
“Kwa hiyo, baada ya kutokea wizi huo, mama wa
mtoto alikwenda kutoa taarifa kituo cha polisi cha stendi kuu ya mabasi Tabora ambapo
polisi walianza kuweka mitego iliyosaidia kumnasa askari huyo,” alisema Kamanda
Issa.
Baada ya kumkamata askari huyo, Kamanda Issa
alisema waliwasiliana na mama wa marehemu ambaye tayari aliyekuwa amefika
Mpanda na aliporudi, alimtambua mtoto huyo.
“Baada ya utambuzi wa mwanamke huyo, uliibuka
mvutano kati yake na askari huyo kwani kila mmoja alikuwa akidai mtoto ni wake.
“Tulichokifanya ni kuwafanyia kipimo cha
kuwachukua damu na kutuma vipimo hivyo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali,” alisema.
Mama asimulia
Akizungumza na MTANZANIA jana kutoka Mpanda,
mama wa marehemu alisema ameumizwa na tukio hilo na sasa yupo katika wakati
mgumu.
“Nakumbuka Jumatatu wiki iliyopita nilipanda
basi la Kampuni ya NBS pale Msamvu Morogoro, nikiwa na watoto wangu watatu
akiwamo marehemu nikielekea Mpanda.
“Safari yetu ilianza kupata matatizo tulipofika
Dodoma kwa sababu basi lilikamatwa na dereva aliwekwa ndani karibu saa nne hivi
kwa sababu alipishana lugha na trafiki.
“Baadaye tuliondoka Dodoma kwenda Tabora ambako
tulifika saa 3:30 usiku.
“Wenye basi walituteremshia ofisini kwao badala
ya stendi. Kwa hiyo, nilichukua teksi hadi stendi kuu ambapo nilitafuta nyumba
ya kulala wageni nikakosa.
“Tuliamua tulale pale pale stendi na wakati
wote huo, yule dada alikuwa pembeni yangu ananiangalia tu.
“Ilipofika majira ya saa saba usiku, alinifuata
nilipokuwa nimelala akaniambia niinuke niende alipo lala yeye kwa sababu
ameweka mkeka, lakini nilimkamtalia.
“Cha ajabu ilipofika saa 10 alfajiri, alikuja
tena akaniomba anisaidie kubembeleza mtoto kwa sababu alikuwa analia, lakini
pia nilikataa kisha aliniambia twende uani, pia nikakataa.
“Nilipomkatalia, aliondoka kisha
akarudi,akaniomba tena mtoto nikamkatalia na wakati huo nikamkabidhi mwanangu
mkubwa yule mtoto mimi nikaenda uani.
“Inaonekana nilipokwenda uani tu, alimwambia
mwanangu mkubwa wasogee mbele, ghafla akamwambia arudi aangalie mabegi
yasiibiwe huku akiwa na mtoto, sasa aliporudi ndiyo akatoroka pale na yule mwanangu
mdogo,”alisema Daphina.
Baada ya tukio hilo, alisema alipiga kelele
kuomba msaada na baadaye akaambiwa akatoe taarifa polisi kwa msaaad zaidi.
” Nashukuru kwa ushirikiano nilioupata kutoka
kwa askari kwani walinisaidia kumpata mtuhumiwa pamoja na mwili wa marehemu
mwanangu uliokuwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi Mirambo,” alisema.
Source: Mtanzania
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ ASKARI JWTZ MBARONI KWA TUHUMA ZA WIZI WA MTOTO”
Post a Comment