Thursday, October 6, 2016

AZAM FC YAMTEUA ADBUL MOHAMED KUWA MENEJA WA TIMU




Katika taarifa ambayo wameitoa kupitia tovuti ya klabu ya Azam FC, Klabu ya Azam imeufahamisha umma kuwa ndugu Abdul Mohamed ameteuliwa Meneja Mkuu wa timu hiyo, uteuzi ulioanza Oktoba Mosi mwaka huu.

Katika taarifa hiyo klabu ya Azam imesema kuwa “Uteuzi huo ni sehemu ya mikakati ya Azam FC ya kuendesha timu kiueledi na tunaamini ujio wa Mohamed utaongeza nguvu kwenye eneo la uongozi na hatimaye kufikia malengo tuliyoyakusudia.

Azam FC inaamini katika uendeshaji mambo kiueledi ndani ya klabu na ndio maana imekuwa na safu ya uongozi iliyosheheni watu wenye taaluma mbalimbali.

Hivyo tunaamini kwa uzoefu aliokuwa nao Mohamed huko alikotoka akiwa kama mwandishi wa habari kwenye Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na nguvu kazi ya viongozi wengine utaweza kutufikisha kwenye mafanikio.
Majukumu ya kuendesha klabu kila siku yamekuwa na changamoto mpya zinazohitaji kutatuliwa kupitia nguvu kazi ya watu na Azam FC hatutasita kuboresha mfumo wetu wa uendeshaji wa klabu kwa kuuongezea nguvu pale inapohitajika ili kufikia mafanikio.

Mbali na kufanya kazi kwa muda mrefu kwenye sekta ya habari akipita IPP Media, Clouds Media na BBC, Mohamed pia amesomea masuala ya Uhasibu na Fedha. Azam FC inamtakia kila la kheri kwenye majukumu yake mapya hayo katika ngazi ya soka”.

Fahari News inamtakia kila la Kheri Ndg Abdul Mohamed katika majukumu yake mapya ya Kuiongoza klabu ya Azam FC.

0 Responses to “AZAM FC YAMTEUA ADBUL MOHAMED KUWA MENEJA WA TIMU ”

Post a Comment

More to Read