Monday, October 10, 2016

MGOGORO,CUF KUWAWEKA REHANI WABUNGE WAKE 9




Licha ya Chama cha Wananchi (CUF) kujivunia uzoefu wa migogoro, huu wa sasa umeweka rehani majimbo yake tisa ya ubunge yaliyopo Bara na hatari ya kupoteza mvuto na wafuasi kama ilivyotokea kwa vyama vingine huko nyuma.

Vyama ambavyo vimewahi kupita kwenye kipindi kigumu kama inavyopita CUF sasa ni NCCR-Mageuzi, UDP na TLP. Lakini zaidi mgogoro wa NCCR-Mageuzi ndiyo unaotaka kufanana na CUF japo kwa mazingira tofauti.

Chama cha UDP kilichopata umaarufu kwa kauli yake ya ‘kuwajaza mapesa watu’ kwenye Uchaguzi Mkuu wa 1995 kilipata wabunge wanne ambao ni wengi kulingana na mvuto wa chama kwa wakati huo.

Lakini, chama hicho kilikumbwa na mgogoro wa uongozi baada ya mwenyekiti wake, John Cheyo kupinduliwa mkutanoni na nafasi yake kuchukuliwa na Nzugule Amani Jidulamabambasi, ambaye hata hivyo hakudumu kwenye nafasi hiyo kutokana na Msajili wa Vyama vya Siasa kutomtambua.

Pamoja na msajili kulipinga kundi lililofanya mapinduzi, chama hicho kilianza kudhoofu na kupoteza mvuto hasa Kanda ya Ziwa ambapo kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2005 kilipata mbunge mmoja- John Cheyo- aliyedumu hadi 2010, kwa sasa chama hicho hakina mbunge na kimepoteza ule mvuto wake wa ‘kuwajaza mapesa watu’.

Augustine Mrema mwanzoni mwa miaka ya tisini alipojiunga na NCCR-Mageuzi baada ya kutoka CCM alikwenda na wafuasi wengi na kukiimarisha chama hicho kilichokuwa hakina nguvu ikilinganishwa na vyama vingine.

Nguvu ya NCCR-Mageuzi ilionekana kwenye Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi  mwaka 1995, ambapo Mrema aliyegombea urais kwa chama hicho alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 1,808,616 na kupata wabunge katika majimbo 19 Tanzania Bara.

Matokeo hayo yalimuonyesha Mrema kuwa tishio kwa chama tawala cha CCM, lakini, baada ya uchaguzi huo mgogoro wa uongozi ndani ya chama hicho ulianza.

Aliyekuwa mwenyekiti wa chama Mrema alianza kupambana na katibu mkuu wake Mabere Marando, hadi chama kuwa na ofisi mbili tofauti, kugawana wajumbe wa baraza la wadhamini, wajumbe wa sekretarieti na kamati kuu.

Mazingira hayo yanataka kufanana na mgogoro wa CUF uliopo sasa kati ya Profesa Ibrahim Lipumba kwa upande mmoja na katibu mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.

Katika mgogoro wa NCCR wakati huo, Msajili wa Vyama vya Siasa wa wakati huo, Jaji George Liundi (sasa marehemu), aliutambua upande wa Marando kiutendaji kwa kuwapa ruzuku bila kutamka hadharani kwamba anaunga mkono kundi lipi.

Nguvu ya msajili ilimdhoofisha Mrema na kundi lake kwa kuwa hawakuwa na fedha za kuendesha shughuli za chama, ndipo akaamua yeye na wafuasi wake kuhamia Tanzania Labour Party (TLP), huku aki tamka ofisi zote mikoani zilizokuwa za NCCR-Mageuzi zibadilike kuwa za TLP.

Licha ya waliobaki NCCR-Mageuzi kuonyesha kufurahishwa na uamuzi wa Mrema wa kuondoka, chama hicho kilichokuwa kikijivunia majimbo 19 ya ubunge, kilianza kudhoofika kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, kwanza hakikusimamisha mgombea urais, pili kilipoteza majimbo 18 ya ubunge na kubaki na jimbo moja tu la Kifu Gulamhussein Kifu (Kigoma Kusini) ambalo nalo lilipotea kwa njia ya mahakama.

NCCR-Mageuzi, mbali na kupoteza wabunge, pia chama hicho kilipoteza wafuasi na umaarufu iliyokuwa nao, hali ambayo CUF inaonekana kuwa nayo kwa kuwa inapita kwenye njia zile zile.

Hata hivyo, Mrema aliyekuwa akijivunia mtaji wa kura milioni 1.8 alijikuta akipiga mwereka kwenye uchaguzi mkuu wa 2000 alipogombea urais kupitia TLP alikoambulia kura 637,115 na wabunge watano.

Kuonyesha kwamba CUF inapita njia ya NCCR-Mageuzi katika kudhoofika, sasa chama hicho kimegawanyika lakini mbali na hivyo Msajili wa Vyama vya Siasa ameibuka hadharani kuunga mkono kundi moja na sasa ameonyesha dalili za kuwapa nguvu ya fedha.

Hata hivyo, kundi la Profesa Ibrahim Lipumba linaloungwa mkono na msajili likifanikiwa kupata ruzuku litakuwa na nguvu, lakini kwa wananchi chama hicho kitapoteza mvuto na kuweka rehani wabunge wa majimbo tisa wa Bara na madiwani.

Huu ni mgogoro wa tano wa kiuongozi ndani ya CUF baada ya kupitia katika kipindi kigumu wakati wa James Mapalala, aliyekuwa mwenyekiti wake wa kwanza, Naila Jidawi, Michael Nyaluba, aliyeanzisha chama hicho upande wa Bara na Hamad Rashid Mohamed.

Uzoefu wa migogo kwa CUF siyo kigezo kwamba chama hicho hakiwezi kuwa kama vyama vingine vilivyopoteza mvuto na kupoteza wabunge na madiwani waliowapata katika uchaguzi uliopita.

Kesi ya wadhamini
Katika hatua nyingine, mchakato wa Bodi ya Wadhamini wa Chama cha Wananchi (CUF), kupata kibali cha kufungua kesi dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na wenzake unaanza rasmi leo wakati maombi yaliyofunguliwa na bodi hiyo yatakapotajwa.

Bodi hiyo ya wadhamini CUF imefungua maombi hayo Mahakama Kuu Masjala Kuu dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Msajili, Profesa Ibrahim Lipumba pamoja na wanachama wengine wa chama hicho waliosimamishwa uanachama wao.

Katika maombi hayo namba 75 ya mwaka 2016, bodi hiyo inaomba kibali cha kufungua kesi dhidi ya Msajili, Profesa Lipumba na wenzake kadhaa, pamoja na mambo mengine, kupinga uamuzi wa Msajili kumtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti halali wa chama hicho.

0 Responses to “ MGOGORO,CUF KUWAWEKA REHANI WABUNGE WAKE 9”

Post a Comment

More to Read