Monday, October 10, 2016

WANAOFANYA BIASHARA KIENYEJI BILA KUSAJILI BRELA WAPEWA MIEZI 2 KUZIRASIMISHA




Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umetoa muda wa miezi miwili kwa wafanyabiashara wanaotumia majina ya biashara pasipo kusajiliwa wafanye hivyo haraka.

Akizungumza na waandishi wa waandishi wa jijini Dar es salaam  jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Frank Kanyusi alisema katika zoezi la kutoa elimu na kurasimisha majina ya biashara na kampuni linaloendelea katika mikoa mbalimbali imebainika kuwa wafanyabiashara wengi wanatumia majina ya biashara pasipo kuyasajili.

“Sheria ya majina ya biashara inamtaka mfanyabiashara kusajili jina la biashara yake ndani ya siku 28 toka aanze kulitumia,” alisema Bw.Kanyusi na kuongezea kuwa kinyume na hapo atakuwa amevunja sheria ya majina ya biashara.

Alisema baada ya muda huo kupita, patakuwa na msako nchi nzima ili kuwabaini wale wote wanaotumia majina ya biashara pasipo kusajili na kuwafikisha katika vyombo vya sheria au kuwatoza faini.

Alisema kuwa sasa usajili wa majina ya biashara umerahisishwa kwani unafanywa kwa njia ya mtandao kwa kutembelea tovuti ya wakala huo ambayo ni www.brela.go.tz ili kupata maelezo yote ya namna ya kusajili jina la biashara.

Aliwataka wafanyabiashara wasiishie kusajili tu jina la biashara bali pia waende katika Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa ajili ya kupata namba ya Mlipa Kodi (TIN) pia waendele katika halmashauri zao kupata leseni ya biashara.

“Kwa kurasimisha biashara serikali itapata mapato kwani wigo wa walipa kodi utaongezeka na pia itakuwa faida kwa wafanyabiashara katika kujengewa mazingira bora ya kufanya biashara,” alisisitiza Bw.Kanyusi.

Alisema BRELA imejipanga kuzunguka mikoa yote nchini ili kutoa elimu juu ya urasimishaji wa majina ya biashara na makampuni kwani imeonekana wananchi hawana uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa urasimishaji.

Hadi sasa BRELA imefanya ziara katika mikoa ya Mwanza, Mara, Geita na Simiyu na wiki hii watakuwa mkoani Shinyanga kwa muda wiki moja katika kuhamasisha wafanyabiashara kurasimisha biashara zao.

Alisisitiza kuwa ni lazima kuhakikisha kuwa biashara zinarasimishwa ili serikali iweze kuwatambua walipa kodi wake ambao watachangia pato la taifa na kuiwezesha Tanzania kuwa ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

0 Responses to “WANAOFANYA BIASHARA KIENYEJI BILA KUSAJILI BRELA WAPEWA MIEZI 2 KUZIRASIMISHA”

Post a Comment

More to Read