Wednesday, October 19, 2016

PANYA ROAD" AFUFUKA MOCHWARI




MKAZI wa Buza wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam Isaack Ernest (16), miongoni mwa wahalifu wa kundi la ‘Panya Road’ amefufuka katika Chumba cha Kuhifadhi Maiti cha Hospitali ya Temeke siku chache baada ya kufikishwa hapo kama maiti.

Tukio hilo la aina yake lililotokea siku chache baada ya kijana huyo kufikishwa hospitalini hapo kutokana na kupata kipigo kutoka kwa wananchi wenye hasira kali baada ya kuhusika matukio ya kuiba, kujeruhi na kuharibu mali.

Oktoba 15 mwaka huu katika maeneo ya Sabasaba, Mbagala vijana sita walikamatwa na kushambuliwa na wananchi kwa tuhuma za kupora watu waliokuwa wakipita maeneo hayo.

Kikundi hicho cha vijana kilichojitambulisha kwa jina la Taifa Jipya kilianza kufanya uhalifu huo baada ya kumalizika kwa Tamasha la Kuinua Vipaji vya Muziki liliandaliwa na Clouds FM katika viwanja vya Zakheim jijini hapa.

Katika tukio hilo mkazi wa Yombo na mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Nuruakim Kelvin Nyambocha (14), aliuawa kwa kuchomwa moto huku watano wakijeruhiwa vibaya kutokana na kipigo hicho.

Aidha miongoni mwao mkazi wa Kilungule Seleman Hamis (16), alifariki dunia akiwa katika chumba cha upasuaji mdogo katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke huku mkazi wa Buza kwa Lugenge ambaye ni fundi gereji Faraji Suleiman (19) alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi ambako yupo hadi sasa.
Akisimulia mkasa huo jana jijini hapa katika Kituo cha Polisi cha Chang’ombe Isaack (miongoni mwa waliopokea kichapo na kudhaniwa kuwa amekufa kisha kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Wilaya ya
Temeke) akiwa mikononi mwa polisi jinsi alivyoshawishiwa kujiunga na ‘Panya Road’ hadi kukutwa na masahibu hayo
anasimulia kuhusu namna ‘Panya Road’ walivyomshawishi kujiunga nao.

“Mimi nakaa Buza, Jumamosi tulikuwa Zakheim kulikuwa na shoo tulikwenda na wenzangu wakati wa kuondoka, wakaniambia kama kula tunakula mimi nikawaambiaje, kula mi sijiwezi kama kula kuleni,” alisema Isaack kuongeza
“Wakaanza kuniambia kuwa mimi nina under fear (ninaogopa), na wakasema na tukila hatukugei mali nikwaambia kama kula kuleni mi sijiwezi…mi nikapita njia nyingine na wenyewe kivyao, kila walipopita walikuwa wanaiba.”

Pia kijana huyo mwanafunzi wa kidato cha tatu katika sekondari ya Lumo jijini hapa anaendelea kusema, “Walivyopita njia nyingine mmoja wakamwitia kelele za mwizi, akapigwa asa mi nikawa nipo ng’ambo nyingine, nikamwona mwingine wengine wakavuka ng’ambo nilikuwapo mimi na kutangulia wengine wakaangukia bondeni, sasa nikaonekana mimi wakaniitia kelele za mwizi kustuka nikajikuta nipo mochwari.”
Isaack anahitimisha kwa kusema, “Mpaka dakika hii nipo hapa…sitarudia vitendo vya wizi kwani nilishawakataa na kwasababu mimi bado mwanafunzi…bado napenda maisha yangu.”

Kwa upande wake mzazi wa Isaack ambaye ni mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Buza anasema hakuwahi kumuona kijana wake akijihusisha na masuala ya wizi kwani katika mtaa wao wamekuwa wakishirikiana na Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi mkoa wa Temeke Gilles Muroto alisema kijana alizindukia mochwari yupo mikononi mwao na baada ya mahojiano ya muda mrefu amewasaidia kujua mtandao wa kundi lao.

“Kijana huyu ametusaidia kuwapata vijana wengine kumi na tunao tunatarajia kuwapandisha mahakamani kujibu mashtaka yao,” alisema Muroto.

Aidha Muroto alisema katika msako walioufanya wamewakamata vijana 16 wakiwa na mapanga na bendera ya kundi lao iliyochorwa na kuandikwa ‘Taifa Jipya…Makali yanaendelea…”

Hata hivyo kamishna huyo alisema wamewaita wazazi wa watoto hao na wamefika katika makao makuu ya Kipolisi Temeke jana ambao watapandishwa mahakamani muda wowote wiki hii kutokana na kukiuka sheria ya watoto ya mwaka 2009 kifungu cha saba hadi tisa.

Aidha Muroto alisema kifungu cha 14 cha sheria hiyo kinatoa adhabu kwa mzazi atakayeshindwa kutekeleza hayo atafikishwa mahakamani na akitiwa hatiani atapewa adhabu ya kifungo cha miezi sita jela au faini ya Sh. Milioni 5.

0 Responses to “PANYA ROAD" AFUFUKA MOCHWARI”

Post a Comment

More to Read