Tuesday, October 18, 2016

MKUU WA WILAYA AAGIZA KUWEKWA NDANI KWA MHANDISI WA MANISPAA




Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Ally Hapi ameagiza kuwekwa ndani kwa Mhandisi wa manispaa ya Kinondoni na baadhi ya viongozi wengine wa Kata ya Mikocheni akiwemo mtendaji wa kata ya mikocheni kwa muda wa saa 24 kutokana na kukiuka baadhi ya maagizo ambayo serikali imekuwa ikiyatoa ikiwemo ujenzi wa barabara ambazo zimekuwa mbovu kwa muda mrefu.

Katika ziara ya kutembelea kata zilizopo katika wilaya ya Kinondoni kwa lengo la kutambua kero ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kwa muda mrefu na wananchi.

Mkuu wa wilaya amefikia uamuzi huo wa kumuweka ndani mhandisi wa manispaa ya Kinondoni Abdul Digaga ambaye hakuwepo katika ziara hiyo kitendo ambacho mkuu wa wilaya amekitafsiri kama dharau na kisha atoe maelezo ya kwa nini barabara mbovu zimekuwa hazitengenezwi kwa muda mrefu na kusababisha kero kubwa kwa watumiaji ikiwemo barabara ya viwandani na ile ya viongozi katika mtaa wa Sewa zilizopo kata ya Mikocheni.

Mbali na hilo mkuu wa wilaya ametoa mwezi mmoja kwa uongozi wa kata ya Mikocheni kutafuta eneo na kuanza ujenzi wa zahanati ya kata hiyo ambao haujatekelezwa kwa miaka miwili sasa licha ya serikali kutoa fedha zilizoombwa na viongozi wa kata hiyo kwa ajili ya ujenzi wa zahanati kiasi cha shilingi Mil. 42 kwa madai kuwa wamekosa eneo la kujenga.

0 Responses to “ MKUU WA WILAYA AAGIZA KUWEKWA NDANI KWA MHANDISI WA MANISPAA”

Post a Comment

More to Read