Sunday, October 23, 2016
WAZIRI MWIJAGE AWATAKA WENYE MALORI KUYAEGESHA MAANA MIZIGO BANDARINI
Do you like this story?
Waziri
wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage jana alitofautiana na
wamiliki wa malori aliposema upungufu wa mizigo ni tatizo la muda duniani,
wakati wafanyabiashara hao wamesema ni vigumu kuwarejesha wenye mizigo
waliokuwa wakitumia Bandari ya Dar es Salam ambao wamehamia bandari za Mombasa
na Beira.
Waziri
Mwijage alisema hayo wakati akifungua mkutano mkuu wa Chama cha Wamiliki wa
Malori (Tatoa), alipowaeleza hali ya kupungua mizigo inaweza kuchukua mwaka na
zaidi na kuwataka wafanyabiashara hao kuwa wavumilivu katika kipindi hiki.
Waziri
Mwijage aliwataka wamiliki hao wa vyombo vya usafirishaji kusitisha huduma hiyo
kwa sasa hadi hali itakapotengemaa.
“Ushauri
wangu kwenu ni kusimamisha malori yenu na kuyatunza vizuri kwa sababu mizigo
haipo hivi sasa, hali ikirejea muendelee kufanya biashara,” alisema. Alisema kukosekana kwa mizigo
ni anguko dogo la uchumi wa dunia ambalo baadaye litaimarika.
“Niwasihi
msiangalie sana muda, inaweza kuchukua mwaka mmoja au zaidi kidogo ya hapo ili
kurudia hali ya zamani, lakini msikate tamaa,” alisema Mwijage.
Waziri
Mwijage alisema kushuka kwa bei ya madini kwenye soko la dunia kumesababisha
nchi kama Zambia na Congo DRC kupunguza mizigo inayopitia kwenye Bandari ya Dar
es Salaam.
Alisema
baadhi ya migodi ya nchi hizo imesitisha uzalishaji na kusababisha mizigo ya
kusafirisha ipungue kwa kiasi kikubwa. Waziri pia alisema mazao ya biashara
yameshuka bei kwenye soko la dunia na hivyo kupunguza uzalishaji na kuleta
athari katika sekta ya usafirishaji.
Lakini
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya NMC Tracking, Natal Charles alisema itachukua
muda mrefu kuwarejesha watumiaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwa sababu
waliondoka kwasababu ya ushindani wa kibiashara uliopo kwenye bandari nyingine.
“Kukosekana
kwa mizigo kwenye Bandari ya Dar es Salaam ni changamoto kwetu wenye malori kwa
sababu wapo waliokopa benki ili kuyanunua magari hayo na sasa wako katika
hatari ya kufilisika,”
alisema.
Alisema
pia wako baadhi ya wamiliki wa malori ambao wameshafilisika kutokana na kukosa
mizigo.
Kwa
mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari vya nje, moja ya sababu inayohusishwa na
kuathirika kwa usafirishaji wa mizigo duniani ni kufilisika kwa kampuni kubwa
ya meli ya Korea Kusini inayoitwa Hanjin, ambayo inashika nafasi ya saba katika
biashara hiyo duniani.
Kufilisika
kwa kampuni hiyo kumesababisha meli za kampuni hiyo kunyimwa kibali cha kushusha
au kupakia mizigo kutokana na kutokuwa na uhakika wa kufikishwa inakoelekea,
limeandika gazeti la The Guardian la Uingereza.
Katika
hotuba yake ya ufunguzi, Waziri Mwijage aliwashauri wamiliki wa malori
kuangalia aina nyingine ya uwekezaji, kama kujenga viwanda.
“Wekezeni
katika viwanda vidogo, vya kati na vikubwa kulingana na uwezo na fursa ya kila
mmoja wenu,” alisema.
Alisema
anawafahamu baadhi ya wanachama wa Tatoa ambao wameanzisha viwanda vya maziwa,
maji, kutengeneza mabomba na kusaga mahindi ili kupata unga.
“Mwekezaji
makini hawezi kung’ang’ania biashara ya aina moja kwani inapoleta hasara
anaachana nayo na kuendelea na ile inayomletea faida,” alisema.
Hata
hivyo, Mwijage aliwataka Tatoa kupeleka mapendekezo yao serikalini ya namna ya
kuboresha sekta ya usafirishaji huku wakitoa mifano halisi ya namna ya
kuiboresha sekta hiyo.
“Wizara
yangu ndiyo yenye dhamana ya kuboresha wepesi wa kufanya biashara. “Nileteeni
masuala yote yanayowakwamisha nami nitayawasilisha kwenye mamlaka husika,” alisema waziri huyo.
Alisema
kama malori ya mizigo hayasafiri, biashara ya vipuri itashuka na matumizi ya
mafuta yatashuka na hivyo kuziathiri sekta nyingi.
Alisema
malori yamekuwa yakisaidia kuongeza mapato ya Serikali na kutunisha mfuko wa
barabara.
Awali,
Mwenyekiti wa Tatoa, Elias Lukumay alisema wamiliki wa malori wanakabiliwa na
tatizo la ukosefu wa maeneo ya kuegesha malori wakati yakisubiri kupakia mizigo
katika Bandari ya Dar es Salaam.
Alisema
mara kwa mara wanapoegesha kwenye maeneo ya barabara jirani na bandari hiyo
wamekuwa wakikamatwa na kutozwa faini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ WAZIRI MWIJAGE AWATAKA WENYE MALORI KUYAEGESHA MAANA MIZIGO BANDARINI ”
Post a Comment