Thursday, November 3, 2016
RAIS MAGUFULI AISHAURI BENKI YA DUNIA KUTOA MIKOPO KWA WAKATI UNAOFAA ILI UTEKELEZAJI WA MIRADI UFANYIKE KWA HARAKA
Do you like this story?
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 03 Novemba, 2016 amekutana na
Mwakilishi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na
Somalia Bi. Bella Bird na kuzungumzia utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini
Tanzania yenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani Bilioni 1.6 zikiwa ni mkopo
kutoka benki hiyo.
Akizungumza baada ya kumaliza
mazungumzo yake na Rais Magufuli, Bi. Bella Bird amesema mikopo hiyo inalenga
kusaidia juhudi za maendeleo nchini Tanzania na itatolewa katika sekta
mbalimbali zikiwemo nishati, usafirishaji, elimu na maji.
"Miradi hii yote imelenga zaidi
kuharakisha maendeleo na kuleta matokeo katika maisha ya Watanzania, ni miradi
ambayo inahitaji uongozi na msukumo mzuri kutoka Serikalini na tunafurahi
kwamba Rais Magufuli ni kiongozi ambaye ana dhamira ya dhati ya kusimamia
maendeleo" amesema Bi. Bella Bird.
Kwa upande wake Rais Magufuli
ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika
maendeleo na ametoa wito kwa Benki hiyo kuharakisha utoaji wa mikopo kwa ajili
ya kutekeleza miradi.
"Tunataka kuona mambo yanatokea
badala ya kutumia muda mwingi kuzungumza, miradi hii ina manufaa makubwa kwa
watanzania na tungependa utekelezaji wake ufanyike haraka, na ili ufanyike
haraka Benki ya Dunia inapaswa kutupatia mikopo kwa wakati unaofaa" amesisitiza Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amemhakikishia
Bi. Bella Bird kuwa Serikali yake ya Awamu ya Tano imejipanga kusimamia
utekelezaji wa miradi yote inayotekelezwa sasa na itakayoanza kutekelezwa
katika siku zijazo kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Kwa hivi sasa miradi 26 yenye
thamani ya Jumla ya Dola za Marekani Bilioni 4.5 inatekelezwa hapa nchini kwa
mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
IKULU
Dar es Salaam
03 Novemba, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
.gif)


0 Responses to “ RAIS MAGUFULI AISHAURI BENKI YA DUNIA KUTOA MIKOPO KWA WAKATI UNAOFAA ILI UTEKELEZAJI WA MIRADI UFANYIKE KWA HARAKA”
Post a Comment