Wednesday, April 12, 2017

Afisa wa uhamiaji auawa Kinyama


  Simanzi! David Mulungu, 40, (pichani) Afisa Uhamiaji jijini hapa, mwishoni mwa wiki iliyopita aliuawa na majambazi kwa kupigwa risasi nyumbani kwake, Tegeta Shule huku kisasi kikitajwa nyuma ya tukio.
Kwa mujibu wa mtu aliyejitambulisha kwa jina moja la Michael, tukio hilo la kusikitisha lilitokea saa 7 usiku wa Alhamisi iliyopita, baada ya kundi la watu kufika kwa marehemu wakiwa na silaha za moto.
Baada ya kufika, wakiwa getini kwa mfanyakazi huyo wa Wizara ya Mambo ya Ndani, walipiga risasi kadhaa juu kisha baadhi yao wakaenda kuidhibiti nyumba ya jirani ambayo anaishi mwanajeshi, wengine wakaruka ukuta na kuingia ndani.
“Walifungua komeo za geti la kuingilia na kuanza kubomoa milango ya nyumba ya marehemu.
Wakati tukio hilo likiendelea, marehemu, mkewe na watoto walipiga mayowe kuomba msaada, lakini majirani waliogopa silaha za moto walizokuwa nazo watu hao.
“Majambazi walibomoa kwa mawe mlango wa chumba cha watoto na ndugu wengine, lakini hawakuwadhuru, wakaenda kubomoa chumba alichokuwemo marehemu na mkewe,” alisema Michael.
Alisema marehemu alizuia mlango kwa kitanda na kupiga kelele lakini haikuweza kusaidia maana majambazi walifanikiwa kubomoa na kuingia ndani, waliwasha taa tu, wakampiga risasi ya kifuani, akadondoka chini na kufa.
Michael alisema baada ya afisa huyo kufariki dunia, majambazi walimtaka mkewe kutoa pesa, akawaambia hawakuwa wakiweka fedha ndani, hivyo wakachukua pochi ya mumewe na vito kadhaa vya thamani na kutokomea.
“Baada ya majambazi kuondoka ndipo majirani tulifika, wakati huo tulikuwa tumekwisha toa taarifa polisi ambao walifika muda mchache.
Baada ya kukagua walibaini maganda mawili ya risasi, wakauchukua mwili wa marehemu kwenda kuuhifadhi Muhimbili.
“Kutokana na maelezo ya mkewe, Agatha Kisaka, inaonekana nia ya majambazi haikuwa kuiba peke yake.
Kama ingekuwa hivyo, pengine wasingempiga risasi marehemu kabla hawajatimiza azma ya kupata pesa,” alisema Michael.
Ndugu mmoja alikataa kuzunguzia tukio hilo, zaidi ya kusema marehemu ameacha mke na watoto wawili.
“Ndugu yangu tupo katika majonzi, siwezi kuzungumza zaidi, kikubwa marehemu tunamsafirisha Nzovwe, Mbeya kwa ajili ya mazishi,”
alisema ndugu huyo aliyekataa kutaja jina.

0 Responses to “Afisa wa uhamiaji auawa Kinyama ”

Post a Comment

More to Read