Wednesday, April 12, 2017
Kuhusu PF3 Kutolewa na Serikali za Mitaa Badala ya Polisi Tu
Do you like this story?
SERIKALI
imesema itaangalia uwezekano wa kuanzisha utaratibu wa viongozi wa
serikali za mitaa kutumiwa kutoa fomu za polisi kwa ajili ya matibabu
(PF 3) panapotokea majeruhi, badala ya kutegemea Jeshi la Polisi pekee.
Hayo
yamesemwa bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mwigulu Nchemba alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti
Maalumu, Mwanne Mchemba (CCM) aliyetaka kufahamu kama utolewaji wa fomu
hizo unaweza kurahisishwa.
Mbunge
huyo amesema watu wengi na hasa wanawake wamekuwa wakiogopa kwenda
vituo vya polisi zinapotolewa fomu hizo za PF 3 na hivyo kusababisha
majeruhi kuteseka na wengine kupoteza maisha.
Amesema,
serikali inapaswa kutoa kama itaweza kurahisisha mlolongo wa utoaji wa
fomu hizo ili ikiwezekana zianze kutolewa katika ngazi za wenyeviti wa
vijiji, mitaa na vitongoji.
Mwigulu
akijibu alisema ushauri uliotolewa na mbunge huyo ni mzuri na hivyo
serikali itawasiliana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
ili kuangalia namna mpango huo unavyoweza kufanyiwa kazi.
Amesema
uamuzi wa kuruhusu fomu za PF3 kutolewa katika ngazi za wenyeviti wa
mitaa, vijiji na vitongoji umekuwa unakwama kutokana na ukweli kuwa
utaratibu wa kutolewa polisi hutumika pia katika kuwanasa watu
wanaojeruhiwa wakiwa katika matukio ya uhalifu wakiwemo majambazi.
"Pale
inapotokea watu wamejeruhiwa halafu hawajafika polisi kuchukua PF 3
tunajua fika kuwa ni wahalifu na tunajua namna nzuri ya kuweza kuwanasa.
Hata
hivyo, ushauri huu wa mbunge wa kuangalia jinsi wenyeviti wa vijiji,
mitaa na vitongoji wanavyoweza kutumiwa katika kurahisisha utolewaji wa
PF3 tutaufanyia kazi, hasa kwa wale wanaopata majeraha wakiwa katika
ngazi za familia ambao wanafahamika kuwa hawana rekodi za uhalifu basi
wapatiwe fomu hizo," ameongeza.
Akijibu
swali la msingi, waziri huyo alisema serikali iliweka utaratibu wa mtu
anapokuwa ameumia apate PF3 kwa mujibu wa kifungu cha 170 cha Kanuni za
Kudumu za Jeshi la Polisi (PGO) ili aweze kupokewa na kupewa matibabu
katika hospitali.
Amesema msingi mkubwa wa fomu hiyo ni kutaka kujua mazingira ya mtu huyo aliumia wapi na alikuwa anafanya nini.
Alisema
PF 3 inatumika pia kama kielelezo mahakamani kama mtu ameshambuliwa ama
amepigwa ili mahakama ijue ameumia kiasi gani na kuwa rahisi kutoa
adhabu stahiki.
Amesema
hata hivyo kuna matukio mengine yaliyo wazi PF 3 hupelekwa hospitali
kwa urahisi wa matibabu na kwa msingi huo fomu hiyo bado inakidhi
matakwa yaliyokusudiwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “Kuhusu PF3 Kutolewa na Serikali za Mitaa Badala ya Polisi Tu ”
Post a Comment