Wednesday, April 12, 2017

Cuf ya Lipumba Yamcharukia Maalim Seif ..Wamwambia Kama Hamtaki Lipumba Aunde Chama Chake..!!!


CHAMA cha CUF kimemtaka Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad kutafuta chama kingine kama hawezi kufanya kazi na Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chama hicho, Abdul Kambaya alimsihi Maalim kutambua kuwa CUF si kampuni yake bali chama cha siasa, hivyo hana mamlaka ya kuwachagulia wanachama mwenyekiti.

Alisema ni muhimu Maalim Seif akatambua kwamba wahuni ni wanaofanya kazi za chama hicho kwenye hoteli na mitandao ya kijamii na viongozi halali wa kitaifa wa CUF wako ofisi za Buguruni.

“Anapaswa kutambua kuwa CUF ni taasisi, ni chama cha siasa, si kampuni yake, wala si mali yake, hivyo hana uamuzi na hawezi kutuchagulia kiongozi. Yeye na Mwenyekiti wamechaguliwa na Mkutano Mkuu, kwa hiyo kama anasema hawezi kufanya kazi na Mwenyekiti wake, atafute pa kwenda yeye na wapambe wake,” alisema.

Akifafanua masuala yaliyozungumzwa na Maalim Seif juzi, ambaye alimtaja kwa jina Sultan wa Pili wa Zanzibar, alisema kuhusu vyombo vya Dola kumzuia kufanya ziara Lindi na Mtwara mwishoni mwa mwaka wa jana,  jambo hilo alishalizungumza na makamanda wa Polisi wa mikoa ya Mtwara na Lindi nao walishaeleza sababu za uamuzi huo. 

Alisema kimsingi kwenye jambo hilo palikuwa na ukiukwaji wa Seif mwenyewe alipomtumia Katibu wa Jumuiya ya Vijana kumwandalia ziara hiyo badala ya kutumia viongozi wa wilaya ya Mtwara Mjini.

Alifafanua kwamba jambo hilo lilifanya viongozi hao wa wilaya kujiona wamedharaulika na kuamua kulijulisha Jeshi la Polisi kuwa hawana taarifa ya ziara hiyo.

Alisema Jeshi la Polisi lilikubali kumzuia Profesa Lipumba na hata alipokwenda Sultan wa Pili wa Zanzibar, Jeshi hilo pia lilimzuia kwa kigezo kile kile kilichomo ndani ya barua ya Barwan.

Alisema hoja kuhusu ushirikiano wa Profesa Lipumba na vyombo vya Dola, nayo ni hoja dhaifu isiyo na mashiko, kwa kuwa ni  Mwenyekiti wa CUF, ni kiongozi katika jamii na ni daktari wa uchumi anayetambulika hata nje ya nchi.

Kuhusu madai ya njama za kumwengua Maalim kwenye nafasi ya Katibu Mkuu, alisema hakuna mwenye njama hizo bali amejiengua kwa mujibu wa Katiba ya CUF ya mwaka 1992 Toleo la 2014. 

“Ndiyo maana hakutaja ibara wala kifungu cha Katiba kilichokiukwa katika anachokiita njama za kumwengua. Ibara ya 93 kifungu cha 3 kiko wazi, kwa hivyo asilete blah blah aoneshe ibara au kifungu kilichokiukwa, vinginevyo itakuwa hadithi za Mfalme Juha,” alisema.

Aliongeza kuwa walio ofisini Buguruni ndio viongozi na wanaoshinda wakifanya mikutano hotelini kwa fedha za mafisadi, ndio wahuni na ni muhimu kwa Maalim kutambua kuwa muda si mrefu ubinafsi wake utamdhuru.

0 Responses to “Cuf ya Lipumba Yamcharukia Maalim Seif ..Wamwambia Kama Hamtaki Lipumba Aunde Chama Chake..!!! ”

Post a Comment

More to Read