Tuesday, April 18, 2017

WAZIRI MWIGULU NCHEMBA : HATUTAMVUMILIA ATAKAYETUMIA KISINGIZIO CHA KUWA NA IMANI KUWASHIKIA PANGA WENGINE


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amesema Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayetumia kisingizio cha kuwa na imani iliyopitiliza kuwashikia wenzake panga ili kuwalazimisha wahamie katika imani yake.

Amesema mtu wa aina hiyo atachukuliwa kama mhalifu yeyote na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Mwigulu aliyasema hayo alipokuwa akizungumza katika Tamasha la Pasaka lililofanyika katika Uwanja ya Uhuru jijini Dar es Salaam.

Alisema kumcha Mungu si udini, lakini kama mtu atakuwa mlokole aliyepitiliza na kuwashikia panga wengine ili kila mtu awe mlokole, hatavumilika.

Alisisitiza kuwa, kila mtu anapaswa kumcha Mungu na kutambua kuwa kumcha Mungu si udini bali udini unatokea pale mtu anapodharau wengine na kutumia njia zisizokubalika kisheria na kiutaratibu kuumiza wengine.

Akitoa mfano alisema ndugu zake wengi ni Waislamu, na yeye amekuwa kiongozi wa Umoja wa Kikristo wa Wanafunzi Tanzania (Ukwata) na ameishi vizuri na ndugu na jamaa wa imani tofauti.

“Katika nchi hii utakuwa na ndugu wa imani tofauti, misimamo iliyopitiliza kudhuru maisha ya wengine serikali itashughulika na watu wa namna hii kama waovu wengine,” alisisitiza Mwigulu.

Alisema amewaelekeza watu walio chini yake wizarani wanaohusika na usajili wa taasisi za kidini (nyumba za ibada) kuhakikisha wanasimamia hilo.

“Ninyi watu mnaosimamia nyumba za ibada, hatuwaheshimu kwa kuwaona usoni, tunawaheshimu kwa kuwa majina mlioweka yanaheshimika. Tutakuheshimu kwa sababu ya jina la Yesu mlilolibeba, ukiliacha jina hilo hutapata heshima hiyo,” alisema Mwigulu.

Akitoa mfano, Mwigulu alisema punda aliyembeba Yesu Kristo pale Yerusalemu aliheshimika kwa kumbeba Yesu lakini kesho yake alitupiwa mawe asiwasogelee watu.

“Mkimuacha Yesu mkija kwetu mtatulazimu tuwatume vijana maana mtakuwa sehemu ya wahalifu kama wengine,” alisema Mwigulu.

Katika tamasha hilo, Waziri Mwigulu aliyekuwa mgeni rasmi alizindua albamu mbili, ya Kwaya ya Kinondoni Revival ya kanisa la TAG iitwayo Ngome Zimeanguka na ya Rose Muhando ya Jitenge la Luthu.

Baada ya kuzizindua, alisema nafahamu kilio cha wasanii kuhusu wizi wa kazi zao na kuahidi ataendelea kutetea haki zao.

0 Responses to “WAZIRI MWIGULU NCHEMBA : HATUTAMVUMILIA ATAKAYETUMIA KISINGIZIO CHA KUWA NA IMANI KUWASHIKIA PANGA WENGINE”

Post a Comment

More to Read