Thursday, April 3, 2014
NDEGE WA AJABU WAANZA KUTEKETEZWA BUKOBA.
Do you like this story?
Wananchi katika Kisiwa cha Musira mkoani
Kagera wameanza kuteketeza ndege waliodaiwa kutoa kinyesi chenye sumu, huku
Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii ikiendelea kukalia majibu ya utafiti kuhusu
ukweli wa madai hayo.
Wizara iliahidi ingetoa majibu ya utafiti huo
mapema.
Gazeti hili lilishuhudia idadi kubwa ya viota
vilivyokuwa na vifaranga na mayai ya ndege hao waliodaiwa kuwa wa ajabu vikiwa
vimeharibiwa.
Awali ilielezwa kinyesi chao kilidaiwa kuwa
na sumu kali iliyohusishwa na vifo vya mifugo.
Mmoja wa wananchi katika kisiwa hicho Jackson
Robert ambaye alikutwa akikata matawi yenye viota ili kuharibu mazalia ya ndege
hao alisema wananchi walikubaliana kuwaangamiza ndege hao ili kuepuka madhara
yaliyojitokeza.
“Hawa ni viumbe wa ajabu sana, kinyesi chao
kina sumu kali kwani kikianguka kwenye bati zinatoboka baada ya muda mfupi,
lakini pia wanyama wakila kinyesi hicho hufa,” alisema mkazi huyo.
Awali, Mkuu wa Mkoa huo Kanali Mstaafu Fabian
Massawe alithibitisha ndege hao kuvamia kisiwa hicho na baadaye Wizara ya Afya
kutuma watafiti kuchunguza ukweli wa madai ya ndege hao kutoa kinyesi chenye
sumu.
Ilidaiwa ndege hao pamoja na kinyesi chao
kutoboa mabati pia kuku 516 na mbuzi 12 walikufa katika mazingira
yaliyohusishwa na ukali wa kinyesi chenye sumu kilichosababishwa na ndege hao.
Hata hivyo gazeti hili lilipomtafuta Dk.
Munda Elias ambaye aliongoza utafiti huo kutoka Wizara ya Afya kutaka kupata
majibu ya utafiti huo, mtaalamu huyo alikata simu na kuendelea kufanya hivyo
kila alipotafutwa.
Hata baada ya kutumiwa ujumbe mfupi wa
maandishi kwa njia ya simu kuhusu nia ya kufahamu matokeo ya utafiti huo,
hakuna jibu lolote lililotolewa pamoja na kuwa ndiye aliyefika katika kisiwa
hicho na kuchukua sampuli za ndege hao kwa ajili ya chunguzi zaidi wa
kimaabara.
Pia mtafiti huyo wa wanyama na ndege baada ya
kufika katika kisiwa hicho wiki chache zilizopita aliwaeleza wananchi kuwa
wamefika kuangalia ukubwa wa tatizo na kuwataka watoe ushirikiano ili kupata
ufumbuzi wa madai yao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “NDEGE WA AJABU WAANZA KUTEKETEZWA BUKOBA.”
Post a Comment