Saturday, November 22, 2014
UTAFITI WA POLISI JAMII UMEONYESHA MAFANIKIO MAKUBWA
Do you like this story?
Na. Tamimu Adam -
Jeshi la Polisi.
Jeshi la Polisi nchini limetakiwa
kutumia matokeo ya utafiti wa tathmini ya Polisi Jamii uliofadhiliwa
na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kupitia Tume ya taifa ya
Sayansi na teknolojia( COSTECH) katika kuboresha mkakati wa Polisi jamii ili
kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao kwani matokeo hayo yana
manufaa makubwa katika kubaini, kuzuia, na kutanzua uhalifu na kero mbalimbali
katika jamii.
Hayo yalisemwa na
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Bi. Selina Lymo kwa niaba
ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano,
Sayansi na teknolojia wakati wa hafla ya kukabidhi chapisho la utafiti wa
matokeo ya tathmini ya Polisi jamii nchini kwa Katibu Mkuu wa Wizara
ya Mambo ya Ndani ya nchi Bw. Mbaraka Abdulwakili .
Kwa upande wake Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi Bw. Mbaraka Abdulwakili
alisema atahakikisha utafiti huo unafanyiwa kazi ipasavyo na amewataka
watendaji wa Jeshi la Polisi kutumia utafiti huo katika kuimarisha usalama wa
raia na mali zao kwa kuwa askari waliopo hawatoshi na Polisi jamii
imeonyesha mafanikio makubwa katika kuzuia vitendo vya uhalifu na
wahalifu.
Naye, Mtaalum
Mwelekezi wa Utafiti wa Tathmini ya Polisi Jamii ambaye pia ndiye Mtafiti
Mkuu Dkt Haji Semboja alisema kuwa utafiti huo
ulifanyika katika kanda saba ambapo matokeo ya utafiti huo yanaonesha kuwa
uhusiano wa kiutendaji baina ya wananchi na Jeshi la Polisi umeboreshwa kwa
kiwango kikubwa kupitia dhana ya Polisi jamii.
Alisema kuwa jambo
hilo linasaidia katika kutengeneza mazingira ya amani na hivyo shughuli
nyingine za kiuchumi na kijamii zinaweza kuendelea kufanyika bila
hofu na kwa uhakika wa ulinzi na usalama.
Aliongeza kuwa,
utafiti huo umeonyesha kwamba, watu wengi wanaamini kuwa, matokeo ya kuanzishwa
kwa Polisi jamii katika maeneo yao kuna mafanikio makubwa katika
kuhimiza na kutia moyo uvumbuzi wa njia mpya za kukabiliana na vitendo vya
uhalifu ambapo wananchi wamekuwa wakihimizwa utoaji wa taarifa za uhalifu
kupitia njia mbalimbali ikiwemo njia ya ujumbe mfupi.
Naye, Naibu
Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki aliipongeza timu
nzima iliyofanya utafiti huo na kusema kuwa Jeshi la Polisi kama watekelezaji
wakuu wa Programu ya maboresho yaliyojikita katika mihimili mikuu
mitatu ambayo ni Weledi, Usasa na Polisi jamii, wanatambua na
kuthamini kazi nzuri iliyofanywa na watafiti hao na amewaomba kuangalia namna
wanavyoweza kufanya utafiti katika mihimili mingine miwili iliyobaki
ambayo ni Usasa na Weledi ili Jeshi Polisi liweze kuwa na
tathimini halisi ya Maboresho yake.
Kwa upande wake,
Mwakilishi wa Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia
(COSTECH) Dr. Flora Tibazarwa alisema kuwa madhumuni ya mpango wa utafiti huo
yalikuwa ni kuimarisha uhusiano baina ya Jeshi la Polisi na wananchi
katika kuzuia na kutatua matatizo ya jamii, msisitizo ukiwa kuzuia uhalifu
kabla haujatokea.
Aliongeza kuwa matokeo
ya utafiti huo yatawasaidia watunga sera na watoa maamuzi kutoa maamuzi na
kutunga sera mbalimbali za usalama wa raia na mali zao kwa faida ya taifa
letu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “UTAFITI WA POLISI JAMII UMEONYESHA MAFANIKIO MAKUBWA ”
Post a Comment