Wednesday, June 3, 2015

POULSEN ANUKIA SIMBA




ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Mdenmark Kim Poulsen, yuko katika hatua ya mwisho ya mazungumzo na Klabu ya Simba kwa ajili ya kuja kuifundisha timu hiyo ya jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jijini jana, uamuzi wa mwisho wa Kim kuja nchini kuifundisha Simba utajulikana keshokutwa Alhamisi.

Chanzo hicho kilisema kwa upande wa maslahi tayari wameshakubaliana na kinacholeta ugumu ni mkataba aliokuwa nao na timu moja ya kwao Denmark anayoifundisha.

"Sio kama tumekaa kimya, katika mchakato wetu Kim ndiye kocha ambaye jina lake limependekezwa namba moja, na kwa upande wa maslahi kocha huyo hajaweka mbele tamaa, ameonekana wazi bado ana mapenzi ya kufanya kazi Tanzania," kilisema chanzo chetu.

Kiliongeza kuwa Kim amekubali kuja kufanya kazi kwa mshahara wa Dola za Marekani 8,000 ambazo ni sawa na Sh. milioni 16.6 za Tanzania.

"Hatutaki kukurupuka, amesema hadi Alhamisi itajulikana kama anakuja au la, sasa anapambana kuvunja mkataba kibusara na viongozi wake," aliongeza.

Hata hivyo, Rais wa Simba, Evans Aveva, alikataa kusema lolote kuhusiana na mazungumzo na kocha huyo ambaye kwa mara ya kwanza alitua nchini na kuifundisha timu ya vijana ya Taifa ya umri chini ya miaka 20 ( Ngorongoro Heroes).

Aveva alisema wanafanya mchakato huo kwa umakini kwa sababu msimu ujao wamepania kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Simba kwa sasa haina kocha mkuu baada ya kuamua kuachana na Mserbia Goran Kopunovic, ambaye alitaka kulipwa mshahara wa Dola za Marekani 14,000 (Sh. milioni 29.1 za Tanzania) kwa mwezi na ada ya kusaini mkataba ambayo ni Dola za Marekani 50,000 (Sh. milioni 104).

Katika kuboresha kikosi chake cha msimu ujao tayari Simba imeshawasajili Mohammed Fakhi, Samir Haji Nuhu, Peter Mwalyanzi, Musa Hassan Mgosi na Mohammed Abrahamu huku pia ikiwaongeza mikataba Hassan Isihaka na Said Ndemla.

CHANZO: IPP MEDIA

0 Responses to “POULSEN ANUKIA SIMBA”

Post a Comment

More to Read