Wednesday, December 28, 2016

AAMUA KUUZA FIGO APUNGUZE UMASIKINI




LICHA ya sheria za nchi kutoruhusu biashara ya viungo vya binadamu, mwenye ulemavu wa viungo, Vikta Komba ambaye anafahamika zaidi kwa jina la Zambia, anasema mpango wake wa kuomba kibali cha kuuza moja ya figo zake, unaendelea.
Komba ni mkazi wa kijiji cha Nkali, kata ya Liuli wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma ambaye tangu mwaka 2009 amekuwa anaishi katika mazingira duni kutokana na mradi wake wa kuotesha miti kufa baada ya wateja wake kushindwa kumlipa fedha zake.
Nilifanya mahojiano kwa mara ya kwanza na Komba mwaka 2015 ambapo alidai anatarajia kuomba kibali cha kuuza moja ya figo zake ili kukabiliana na matatizo yanayomkabili hali inayosababisha kushindwa kuendesha maisha yake.
Nimezungumza naye tena wiki iliyopita alipofika kwenye msiba wa mama yake katika Mtaa wa Ruhuwiko Manispaa ya Songea ambapo anasisitiza kuwa mpango wake wa kuomba kibali Wizara ya Afya ili kuuza moja ya figo zake upo palepale, kwa kuwa matatizo yanayomkabili hayajapatiwa ufumbuzi hadi sasa.
Anasema mwaka 2016 amejaribu kuanzisha bustani ndogo ya mboga katika bonde la Kijiji cha Nkali, hata hivyo kutokana na kukosa mtaji wa kutosha bado bustani hiyo imeshindwa kumsaidia badala yake mboga zinamsaidia kwa matumizi ya familia tu.
Zambia bado anaishi katika maisha duni baada ya mradi wake wa kuotesha miche kukwama kwa kile ambacho anadai wateja wake wakiwemo watu binafsi na serikali kushindwa kumlipa deni lake tangu mwaka 2011.
“Mradi wangu wa kuotesha miche ya miti tangu mwaka 2009 umekufa, kwa miaka mingi niliweza kuotesha miche na kuuza katika maeneo mbalimbali ikiwemo ofisi za serikali, shule, taasisi za kidini na watu binafsi, sasa nimebakia kuwa masikini baada ya wateja wangu kushindwa kunilipa karibu Sh milioni kumi,’’ anaelezea Komba.
Anasema hivi sasa anakabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi katika familia yake ikiwemo kushindwa kukamilisha ujenzi wa nyumba yake na watoto wake wanashindwa kusoma kwa sababu anashindwa kuwalipia ada.
“Mikakati yangu ya kutaka kuzalisha miche ya miti zaidi ya 20,000 kila mwaka imekwama. Kwa sasa kitalu kina miche isiyozidi 1,000. “Hali hii imenifanya nikabiliwe na madeni mengi, mimi ni mwenye ulemavu na sasa nimeongezewa ulemavu wa kisaikolojia na imefikia mahali hata malapa tunachangia katika familia naomba serikali inisaidie’’, anasisitiza.
Komba, baba mwenye mke na watoto watano, licha ya ulemavu wa viungo alionao ni mkulima na mwanamzingira hodari katika kijiji chake. Nimeweza kutembelea bustani yake ambapo amepanda mboga mbalimbali zikiwemo kabichi, maharage, miwa, mboga za majani.
Hata hivyo kutokana na kukosa mtaji wa kutosha eneo ambalo amezalisha mboga hizo ni dogo hivyo hawezi kuvuna mapato ya kutosha ili aweze kupata fedha za matumizi na ada kwa ajili ya watoto wake wanaosoma sekondari.
“Nimepania kwenda kuomba kibali cha kuuza moja ya figo zangu ili niweze kupata fedha zinakazoniwezesha kutatua matatizo yangu, sina namna nyingine, nyumba inaanguka, watoto wangu watatu wanadaiwa ada ninaishi kwa shida kubwa,’’anasema Komba.
Mwenyekiti wa Chama cha Wenye Ulemavu wa Viungo Mkoa wa Ruvuma, Samwel Mapunda anathibitisha kupata taarifa za Zambia kuwadai wateja wake wakiwemo watu binafsi na taasisi za serikali na kwamba chama hicho kimejitahidi kuchukua hatua za kumsaidia mwanachama wao ili aweze kupata haki yake yote.
Hata hivyo Mapunda anasema, licha ya jitihada kubwa ambazo wamezifanya hadi sasa Komba amelipwa sehemu tu ya madai yake, hivyo anatoa rai kwa viongozi wa serikali na wanasheria kuangalia namna wanavyoweza kumsadia ili apate haki zake zote hatimaye aweze kuendesha maisha yake.
Komba ni miongoni mwa watanzania ambao kutokana na ugumu wa maisha wameanza kuwa na wazo la biashara ya kuuza figo zao kwa watu wenye mahitaji ya kiungo hicho muhimu mwilini.
Komba anasema anatarajia kuuza figo yake kati ya Sh milioni 30 hadi 40, ingawa kuna taarifa kuwa kuna baadhi ya watu nje ya nchi wanauza figo kati ya Sh milioni 80 hadi sh milioni 100.
Mahitaji ya watu kuhitaji figo hapa nchini na nje ya nchi yanazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka, ambapo inakadiriwa kuna wagonjwa 470,000 nchini ambao figo zao zimeshindwa kufanya kazi na wanahitaji upandikizaji.
Sheria ya nchi inabainisha wazi kuwa uuzaji wa figo ni kosa la jinai kwa sababu kisheria hairuhusiwi kuuza kiungo chochote cha binadamu kwa gharama yoyote na kwamba kutoa figo ni lazima kufuata taratibu za kisheria na za kitabibu.
Hata hivyo, mwongozo wa sera za Wizara ya Afya hazikubaliani na biashara ya uuzaji wa figo kama ambavyo hairuhusiwi kisheria uuzaji wa damu kwa mtu yeyote.
Sheria, sera, mwongozo na kanuni za kuzuia uuzaji wa viungo vya binadamu sio unapigwa marufuku hapa nchini pekee bali hata katika nchi nyingine duniani hazikubaliana na biashara ya kuuza viungo vya binadamu.
Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Habari la Uingereza (BBC) imewahi kuripoti mwaka huu kuwa polisi nchini India wamewashtaki madaktari watano kwa makosa ya kufanya biashara ya figo ya binadamu.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Asia Kusini inaongoza duniani kwa upandikizaji viungo vya binadamu, huku India ikiwa miongoni mwa wasafirishaji wakubwa zaidi wa figo ambapo kila mwaka raia zaidi ya 2,000 wa India huuza figo zao huku nyingi zikienda kwa wageni.
Ongezeko ya maradhi ya figo, kisukari na shinikizo la damu kumesababisha ongezeko la mahitaji ya figo duniani, hivyo kuibua biashara haramu ya figo kuenea kwa kasi. Hata hivyo kimataifa kuuza kiungo cha binadamu ni kosa la jinai na kwamba imepigwa marufuku biashara ya viungo vya binadamu ikiwemo figo.
Inakadiriwa figo moja huuzwa kati ya Sh milioni 100 hadi 240.
Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti la habarileo, mawasiliano baruapepe:albano.midelo@gmail.com, simu 0784765917

0 Responses to “AAMUA KUUZA FIGO APUNGUZE UMASIKINI”

Post a Comment

More to Read