Wednesday, December 28, 2016

POLISI WAENDELEA KUMWAGWA KILOSA MOROGORO




BAADA ya kutokea mapigano kati ya wakulima na wafugaji wilayani Kilosa, Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe, ameagiza askari polisi kuongezwa katika maeneo yenye migogoro ya wakulima na wafugaji hasa katika kata 14 zinazotajwa kukithiri kwa migogoro hiyo ili kuimarisha ulinzi na kudumisha amani.
Dk Kebwe alitoa agizo hilo wakati alipotembelea eneo la Kijiji cha Dodoma Isanga, Kata ya Masanze, wilaya ya Kilosa mkoani humo.
Katika ziara hiyo alifuatana na Kamanda wa Polisi wa mkoa, Ulrich Matei ili kwenda kujionea mwenyewe na kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho juu ya tukio hilo la juzi la mtu kuchomwa mkuki mdomoni.
Taarifa zilizopatikana katika mkutano huo, zilieleza kuwa mkuu wa mkoa aliwahakikishia wakulima usalama wao na kuwataka waendelee na shughuli za kilimo na kumtaka RPC kupeleka askari zaidi ili wawe wanazungukia maeneo yenye migogoro ya ardhi.
Mkuu huyo wa mkoa pia aliagiza katika Kata 14 zilizotajwa kuwa na migogoro ya wakulima na wafugaji, ufanyike mchakato wa kuanzishwa vituo vidogo vya Polisi kwa ajili ya kusongeza huduma za kuimarisha ulinzi maeneo hayo .
Kata hizo 14 ni za Kilangali, Ulaya, Masanze , Chanzuru , Rudewa , Msowero, Dumila, Kimamba , Magole , Mabwerebwere, Mikumi, Tindiga , Malolo na Zombo , zenye jumla ya vijiji 29.
Mbali na hayo, pia alimwagiza Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo kuhakikisha sheria ndogo zilizopitishwa na Baraza la Madiwani kuhusiana na masuala ya ufugaji zinasimamiwa na kufanya kazi.
Alimtaka Mwenyekiti wa chama cha wafugaji katika wilaya ya Kilosa kushirikiana na viongozi wa kimila wa kabila la wafugaji wa kimasai ‘Leigwanani’ watambue umuhimu wa kudumisha amani kwenye maeneo yao kwa kukaa vikao vya mara kwa mara.
Pia aliziagiza mamkala za wilaya ya Kilosa kuhakikisha wafugaji wavamizi katika maeneo ya wakulima waondolewe mara moja na kuhakikisha kila kundi linaendesha shughuli zake kwenye maeneo waliyopangiwa na si vinginevyo.
Kwa upande wake , mkuu wa wilaya hiyo, Adam Mgoyi, alimhakikishia mkuu wa mkoa kuwa maagizo yote yaliyotolewa yatasimamiwa na kutekelezwa ipasavyo ili kudumia amani na utulivu.
Kwa mujibu wa wananchi waliozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, walidai kuwa hali imerejea kuwa shwari ingawa bado wafugaji wamekuwa na tabia ya kuchunga mifugo yao nyakati za usiku kuharibu mazao mashambani.
Jumapili Mkulima na mkazi wa Kijiji cha Dodoma Isanga wilayani Kilosa, mkoani Morogoro, Augustino Mtitu, alichomwa mkuki sehemu ya mdomoni na kutokea shingoni na kumjeruhi vibaya na kulazimika kikimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kufanyiwa upasuaji kuondoa mkuki huo na kuokoa maisha yake.
Mtitu na wengine wanane wakijeruhiwa, katika vurugu zililohusisha jamii ya wafugaji wa Kimasai na wakulima wa kijiji hicho kilichopo katika wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro baada ya wafugaji hao kulisha mifugo yao katika mashamba shamba ya maharage na mahindi katika kijiji hicho.

0 Responses to “ POLISI WAENDELEA KUMWAGWA KILOSA MOROGORO”

Post a Comment

More to Read